26.2 C
Dar es Salaam
Friday, December 3, 2021

IGP, RPC waitwa mahakamani kujieleza


 MASYENENE DAMIAN

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mwanza imewataka  viongozi wa Jeshi la Polisi nchini akiwamo Mkuu wa Jeshi hilo (IGP), aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufika mahakamani kujieleza kwa nini hawakumlipa askari waliyemfukuza kazi.

Askari huyo  mwenye namba EX F 5421 D/C, Manga Msalaba alifukuzwa kazi  na baadaye alifungua kesi ya madai namba 6 ya mwaka 2017 Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza na kushinda ambapo iliamriwa alipwe stahili zake Sh milioni 21,382,380 ndani  ya siku 30.

Mahakama hiyo ilimuaru IGP, RPC na mwanasheria wa Serikali kumlipa askari fedha hizo ambazo ni malimbikizo ya mishahara ya miezi 33 aliyokuwa anadai kabla ya kufukuzwa kazi.

Askari huyo aliyekuwa akilitumikia jeshi hilo mkoani Mwanza alifungua kesi ya madai ambapo shauri hilo lilitajwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Mei 30, mwaka jana chini ya Jaji Joaquine Demello.

Kutokana na kesi hiyo mahakama ilitoa hukumu Agosti 30, 2018 na kuwataka IGP na RPC kumlipa askari huyo kabla ya Oktoba 10 mwaka jana.

Hata hivyo hadi  Januari 4, mwaka huu  hakuna malipo yaliyokuwa yametolewa hatua iliyosababisha deni kuongezeka kutoka Sh milioni 21,382, 380 za awali  hadi Sh milioni 22, 882, 380.

Kutokana  kutolipwa  fedha hizo, wakili wa upande wa  mlalamikaji, Alfred Sotoka aliamua kurudi Mahakama Kuu kupeleka maombi kuwauliza wadaiwa kwa nini hawajalipa na kuomba mahakama itoe hati ya kuitaka hazina kulipa fedha hizo.

Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo Desemba 17, mwaka jana na kupewa ‘execution’ namba 37 ya mwaka huu, ambapo hati hiyo iliombwa chini  ya kifungu namba 16 kifungu kidogo cha 1 na 2 cha sheria ya mashauri dhidi ya Serikali  iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Wakili Sotoka alilieleza MTANZANIA kuwa  mteja wake anadai malimbikizo ya mshahara wa miezi 33 Sh milioni 22 ikiwemo posho ya chakula na malipo mengine ya uhamisho akiwa mtumishi wa jeshi hilo.

Kwa mujibu wa  hati ya wito iliyosainiwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza Desemba 21, mwaka jana kwenda kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza na wenzake iliwataka kufika mahakamani Januari 9, mwaka huu  kwa ajili ya kusikilizwa kwa marejeo ya maombi hayo.

Kwa upande wake, Msalaba alisema akiwa mtumishi wa jeshi hilo alisitishiwa mshahara wake Aprili, 2014, madai mengine ni kutopewa stahiki zake kama posho za usumbufu na gharama za kufunga mizigo baada ya kuhamishwa kituo cha kazi kutoka Mwanza kwenda Ukerewe mwaka 2015 na baadaye Kisesa na Magu mwaka 2016.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,875FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles