20.5 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Idara Forodha TRA yapambana vilivyo kufikia malengo

KOKU DAVID-DAR ES SALAAM

IDARA ya Forodha ni sehemu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambayo inahusika na ukusanyaji wa kodi katika mizigo inayoingia na kutoka kupitia bandarini.

Katika mwaka wa fedha wa 2018/19 idara ya forodha inatakiwa kukusanya kiasi cha sh. trilioni 9.9 na kwamba hadi sasa imeshakusanya sh. trilioni 4.5.

Hadi Machi 31 idara hiyo ilikuwa imejiwekea lengo la kukusanya sh. trilioni 5.6 lakini kutokana na changamoto mbalimbali lengo hilo halikufikiwa na badala yake imekusanya sh. trilioni 4.5.

Katika kuhakikisha lengo la kukusanya trilioni 9.9 linafanikiwa, TRA kupitia idara la forodha mwishoni mwa wiki iliyopita ilikutana na mawakala wa foroda ili kujadili changamoto zinazojitokeza kwa pande zote mbili na kuangalia namna nzuri ya kuzitatua ili waweze kufikia lengo lao katika makusanyo.

Kaimu Naibu Kamishna wa Forodha wa TRA, Juma Hassan anasema kuwa katika idara ya forodha, mawakala wa forodha ni wadau muhimu kutokana na kuwa bila ya uwepo wao hakuna ukusanyaji unaoweza kufanyika katika forodha.

Anasema hivi karibuni wamekutana na wadau wa Chama cha Mawakala wa Forodha (TAFFA) na kujadili changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika uwasilishaji na ufanyiaji taratibu wa nyaraka za kutolea mizigo bandarini.

Anasema sambamba na changamoto hizo pia walijadili changamoto zinazohusiana na usafirishaji wa bidhaa baina ya Tanzania Bara na Zanzibar ikiwa ni pamoja na changamoto zinazojitokeza wakati wa kusafirishaji mizigo inayoenda nchi za jirani za Afrika Mashariki.

Hassan anasema kuwa usafirishaji wa mizigo inayokwenda nchi za jirani zina utaratibu wake maalumu na kwamba walijadili changamoto zake ambazo wanatarajia kuzitafutia ufumbuzi wa haraka ili kuweza kufanikisha malengo yao katika ukusanyaji mapato.

Anasema idara ya forodha ni sehemu ya TRA na kwamba katika mwaka wa fedha imepangiwa kukusanya sh. trilioni 9.9 huku Machi 31 ili imejipangia lengo la kukusanya sh. trilioni 5.6 ambalo halikuweza kufikia kutokana na changamoto ambazo hivi sasa wanazitafutia ufumbuzi.

Anasema hadi sasa wameshakusanya sh. trilioni 4.5 ambazo ni sawa na asilimia 84 na kwamba kutokana na jitihada na mikakati mbalimbali waliyojiwekea wanaamini watafanikiwa kufikia lengo.

Anasema kuwa kutofikia lengo la makusanyo kunatokana na changamoto mbalimbali zikiwemo za misamaha ya kodi, ukwepaji wa kodi unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara ambao sio wazalendo.

Anaongeza kuwa kodi zinakusanywa kutokana na mizigo na kwamba kodi ya forodha inatokana na thamani ya mizigo.

Hassan anasema katika mkutano wao na mawakala hao wa forodha waliwaeleza majukumu yao pamoja na kuwaelekeza  wanayotakiwa kuyafanya ikiwa ni pamoja na kuwaeleza yale ambayo TRA inakusudia kuyafanya.

Anasema baada ya kuzibaini changamoto na kuzitatua, wanatarajia kuwatoza penati mawakala watakaokutwa na makosa ambayo yalishatafutiwa ufumbuzi.

Anaongeza kuwa kutokana na mkutano huo changamoto kutoka pande zote mbili wataziandalia mikakati ya utekelezaji ambayo itazitatua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,058FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles