29.6 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

Faini Sh mil 20 uingizaji mifuko ya plastiki

Mwandishi Wetu-Dar es Salaam

WAAGIZAJI  na wasafirishaji nje mifuko ya plastiki (rambo), iliyopigwa marufuku na Serikali watapigwa faini ya Sh milioni 20 endapo watakaidi agizo hilo la Serikali.

Akizungumza katika mahojiano maalumu mjini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC), Dk. Samuel Gwamaka, alisema  adhabu za wavunjaji wa amri ya serikali tayari zimeainishwa  katika ‘kanuni za marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki za mwaka 2019’ na kwamba adhabu hizo  zitatumika kupambana na  wakorofi. Kanuni hizo zimetungwa chini ya Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004.

“Uingizaji nchini wa mifuko ya plastiki faini ni Sh milioni 20, usafirishaji nje ya nchi wa mifuko ya plastiki,uzalishaji, uhifadhi na usambazaji wa mifuko hii ni Sh milioni 10, uuzaji ni Sh 10,000 na utumiaji ni Sh  30,000,” alisema Dk. Gwamaka.

Alisema shehena ya mifuko ya plastiki itasalimishwa  kwa viongozi wa wilaya na kwamba kila wilaya itatenga eneo maalumu la kuhifadhi mifuko hiyo na umma utatangaziwa maeneo yaliyotengwa kwa ajili hiyo.

Pia aligusia suala la mifuko mbadala na kuainisha kuwa ni mifuko iliyotengenezwa kwa karatasi, nguo, gunia, vikapu na kadhalika na kufafanua kwamba mifuko ya aina hiyo ni ile ambayo ni rafiki kwa mazingira na ambayo haina madhara kwa afya ya binadamu na mazingira.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka Watanzania kutambua  marukufu ya Serikali imeibua fursa kwa watu wabunifu  kutengeneza mifuko mbadala na kueleza kwamba tayari vipo viwanda vya karatasi 25 nchini na baadhi yake vinatengeneza mifuko mbadala na kueleza kuwa kuna viwanda vinavyotengeneza mifuko ya nguo.

 “Kuna wawekezaji na wamiliki wa viwanda ambao walikuwa wanasubiri tamko la serikali ili wawekeze mara moja katika utengenezaji wa mifuko mbadala,” alisema.

Aliwataka  Watanzania wabunifu  wenye kutaka kutumia fursa hii kuwekeza katika utengenezaji wa mifuko mbadala wasibabaike wala kusumbuka bali wawasiliane mara moja  na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), NEMC, Shirika la Viwango Tanzania (TBS, Shirika la Maendeleo la Viwanda Vidogo (SIDO) na Taasisi za Fedha.

Alisema Serikali imeunda kikosi kazi juu ya suala hili muhimu kitaifa  kinachoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na NEMC na kuongeza kwamba serikali inaandaa mpango kazi wa utekelezaji wa katazo hili kwa manufaa ya wananchi.

“Serikali inatoa wito kwa wadau wote ikiwemo wawekezaji katika viwanda kuzingatia umuhimu wa uchumi wa mbadala wa mifuko ya plastiki kwani  utaibua ajira nyingi zaidi na kukuza kipato cha  wananchi wa kawaida hasa kina mama katika kutengeneza mifuko mbadala ambako kunahitaji teknolojia rahisi na nguvu kazi,” alisema Dk. Gwamaka.

- Advertisement -

Related Articles

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles