29.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mengi aacha pengo sekta ya michezo

SOSTHENES NYONI-DAR ES SALAAM

TASNIA ya michezo nchini imepata pigo  baada ya mdau wake, Dk. Reginald Mengi, kufariki usiku wa kuamkia jana Dubai Umoja wa Falme za Kiarabu.

Taarifa ya kifo cha mfanyabiashara huyo  ilitolewa na vyombo mbalimbali vya habari alivyokuwa anavimiliki.

Enzi za uhai wake, Mengi ambaye anafahamika kama mfanyabiashara  mkubwa, pia alikuwa mdau mkubwa wa michezo nchini.

Zaidi alikuwa mpenzi mkubwa wa klabu ya soka ya Yanga.

Mwaka 1996 aliibuka na kuamua kuisaidia Yanga, wakati huo ikiwa kwenye mgogoro mkubwa, ambao alishauri klabu hiyo igeuzwe kuwa kampuni ili iweze kujitegemea badala ya kutegemea misaada ya Watanzania wenye asili ya Kiasia.


Hata hivyo, ushauri wake huo ulipuuzwa, hivyo akaamua kujitenga na klabu hiyo.

Aliwahi kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa Stars, akishirikiana na aliyekuwa mfadhili wa klabu ya Simba, Azim Dewji.

Lakini hivi karibuni alikuwa mlezi wa timu ya Taifa ya vijana walio na umri chini ya miaka 17, Serengeti Boys iliyoshiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon U-17) zilizofanyika hapa nchini jijini Dar es Salaam.

Mengi aliahidi kumpa kila mchezaji Sh milioni 20 kama kikosi cha Serengeti Boys kingefanikiwa kutwaa taji hilo.


Hata hivyo, Serengeti Boys haikufanya vizuri katika patashika hiyo, baada ya kufungwa mechi zote tatu za hatua ya makundi ikichapwa mabao 5-4 na Nigeria, ikalazwa mabao 3-0 na Uganda kabla ya kutunguliwa mabao 4-2 na Angola.

Inaelezwa kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa na utajiri wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 560.

Mengi aliyezaliwa mwaka 1944 mkoani Kilimanjaro, amefariki dunia ikiwa imepita miezi sita tangu kufariki kwa mkewe wa kwanza, Mercy Anna Mengi, usiku wa Novemba 1, mwaka 2018 katika Hospitali ya Mediclinic Morningside Afrika Kusini, alipokuwa akipatiwa matibabu.
Mbali na Mercy, mama wa watoto wake watatu, Regina, Mutie (marehemu pia) na Abdiel, mke mwingine wa Mengi ni mwanamitindo na Miss Tanzania wa mwaka 2000 aliyewahi pia kuwa mwanamuziki, Jacqueline, ambaye amezaa naye watoto wawili pacha. Mungu ampumzishe kwa amani Mzee Reginald Mengi. Amina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles