24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

‘Chui wa Asia’ sawa – wapi ‘Simba wa Afrika?’

HILAL K SUED

MAENDELEO ya kweli siyo kitu cha kubahatisha kama jinsi wanasiasa wengi wanavyofikiri. Maendeleo ya kweli hasa katika nchi za Ulimwengu wa Tatu (Third World) yanapatikana kwa jitihada za kimakusudi za kiongozi mwenye dhamira halisi ya kuendeleza watu wake zikiambatana na mipango madhubuti, na si kitu kingine.

Lakini kwa bahati mbaya kabisa katika ulimwengu huu wa tatu wanasiasa wenye dhamira ya kweli ninayozungumzia hawapo wengi – au tuseme huwa hawaji wawili wawili. Hata hivyo eneo la Asia ya kusini na kusini mashariki wamejaliwa kuwa na viongozi wa namna hii.

Mfano ni Malaysia na Singapore ambazo pamoja na nchi nyingine tatu – Taiwan, Korea ya Kusini na Hong Kong – zinaunda kundi la nchi zinazojulikana kama Asian Tigers (Chui wa Asia) kutokana na hatua kubwa ya maendeleo yao kiuchumi ambayo wameyapata katika kipindi cha takriban nusu karne tu iliyopita.

Hapa Barani Afrika wachunguzi wa mambo hujiuliza – lini tutapata kundi letu la nchi tunaloweza kulilinganisha na hilo la Asia Tigers na tuliite ‘African Lions’ – yaani ‘Simba wa Afrika?’

Unapozungumzia, kwa mfano, maendeleo makubwa ya kiuchumi ya Malaysia na Singapore, kamwe huwezi kuacha kuwataja viongozi wao wa zamani – yaani Dk Mahathir Mohamad (Malaysia) ambaye sasa karudia tena uongozini ingawa kwa muda tu na Lee Kuan Yeu (Singapore). Viongozi hawa wamefanya makubwa sana katika maendeleo ya kiuchumi katika nchi zao tangu zilipojipatioa uhuru mwishoni mwa miaka ya 50.

Andishi langu la leo ni kuhusu huyu wa pili, Lee Kuan Yew wa Singapore ambaye alifariki dunia miaka minne iliyopita (2015) akiwa na umri wa miaka 91. Alistaafu Uwaziri Mkuu wa Malaysia mwaka 1990.

Hata wenyewe watu wa Singapore hawakuwa wanajua mustakabali wa nchi yao kiuchumi pale mwaka 1959 mwanasheria kijana, mkakamavu, na kiongozi wa chama chake cha Action Party (AP) angeweza kuibadili sehemu ndogo ya ardhi iliyokuwa koloni la Uingereza.

Eneo hilo halikuwa na chochote bali kituo kimoja kidogo cha wafanyabiashara wa Kichina na pia kuwa kituo cha kijeshi cha askari wa Uingereza waliobakia baada ya Vita vya Pili vya Dunia – lakini aliweza kuibadili na kuwa nchi tajiri yenye maendeleo makubwa ambayo sasa hivi mgawanyo wa mapato yake kwa kila mwananchi (per capital income) ni ya juu kabisa Barani Asia baada ya Japan na ni ya juu kuliko nchi zote Kusini mwa Asia.

Lakini Lee Kuan Yew, Baba wa Taifa la Singapore aliweza kufanya muujiza huo, na hii ilitokana na si kingine bali imani yake kwamba miujiza hutokea, na pia imani kwamba ili Singapore idumu kama taifa huru linalojitegemea ilihitaji uchumi madhubuti, aliaanzisha mkakati wa kuiendeleza nchi hiyo hususan katika sekta ya viwanda.  

Ili kupata mafanikio, alihimiza ushirikiano, nidhamu na pia hali ya kujinyima, hata kama katika hayo alionekana, mara nyingine kuongoza kiimla – yaani kukandamizaji haki za raia na kuingilia uhuru wa vyombo vya habari. Lee alilea muundo wa serikali wa kuthibiti nyanja ya siasa lakini kwa kutumia mahakama.

Ari kubwa iliyompelekea Lee Kuan Yew kuibadilisha Singapore kiuchumi inaelezwa katika nukuu hii yake moja aliyoitoa mwaka 2007 – miaka 17 baada ya kustaafu kama Waziri Mkuu wa nchi hiyo:

“Ili kuelewa kwa nini Singapore ilivyo sasa hivi, lazima uanze na kukubali kwamba haikutakiwa kuwapo na kwamba isingeweza kuwapo katika uso wa dunia. Kwanza kabisa hatukuwa na nyenzo kuwa kama taifa isipokuwa tu uzalendo wa wananchi, lugha moja, utamaduni mmoja na hatima moja. Hivyo historia ni kitu cha muda mrefu, nami nimetimiza wajibu wangu.”

Hivyo basi utawala wake ulijumuisha vitu vingi – kama vile kuwa na serikali kuu ya kati na uchumi huria na iliyokuwa ikikemea ufisadi na maovu mengine kwa vitendo.

Namna hii ya utawala uliozaa mafanikio makubwa kiuchumi pia ulianza kuigwa katika nchi nyingine Barani Asia, pamoja na China na Vietnam, na umekuwa ni mojawapo ya mafundisho kwa wanazuoni katika nyanja za uchumi na maendeleo katika nchi nyingine nyingi za Ulimwengu wa Tatu.

Lee Kuan Yew alikuwa muumini mkubwa wa falsafa ya ‘Mazuri ya Asia’ (Asian Values) kwanza, ambapo mazuri ya jamii yanakuja kwanza kuliko haki za raia. Hata hivyo raia wengi wa Singapore hawatilii sana maanani namna walivyoifikia hiyo ‘pepo’ waliyo nayo sasa – hususan ikizingatiwa mkono wa chuma aliotumia.

Kuna baadhi wanasema huenda alifanikiwa kutokana na Singapore kuwa eneo dogo tu la ardhi na watu wachache, wasiozidi milioni 2 wakati anachukua uongozi wa nchi.

Lee Kuan Yew pia alisifika katika kampeni zake za kuleta mabadiliko ya kiutamaduni na kitabia, aliwahimiza wananchi katika mikutano yake, kutabasamu wakati wote, kuongea Kiingereza kizuri, kusukuma maji ya chooni baada ya kwenda haja, kutotema mate hovyo, kutotafuna pipi ubani (yaani Big G) na kutotupa takataka kutoka magorofani.

Katika kitabu cha kumbukumbu zake kiitwacho “From Third World to First: The Singapore Story 1965-2000” aliandika: “walikuwa wanatucheka kwa kampeni zetu hizi, lakini tulikuwa tunaamini kabisa kwamba tungekuwa taifa la hovyo, jeuri na lisilostaarabika iwapo tungeacha kuchukuwa jitihada hizo.”

Baada ya kustaafu kwa Lee Kuan Yew mwaka 1990, na taifa la watu wapatao 5.6 milioni, na utawala kushikwa na kizazi cha uliberali, wachunguzi wa mambo wanadadisi iwapo taifa hilo linaweza kuhimili mtikisiko wowote unaoweza kutokea.

Kuna baadhi wana wasiwasi iwapo mazuri yote yaliyopatikana kiuchumi yanaweza kudumu au kuzidishwa. Ni muda tu ndiyo utakaoamua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles