24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

CAG ameonyesha ukomavu aigwe

Na LEONARD MANG’OHA

KITENDO cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kuitikia wito wa Spika wa Bunge, Job Ndugai na kujieleza mbele ya Kamati ya Maadili ya Bunge ni ukomavu katika uwajibikaji.

CAG na Spika waliingia katika mvutano baada ya CAG kudai kuwa Bunge ni dhaifu kwa kushindwa kuchukua hatua juu ya mambo mbalimbali yanayowasilishwa bungeni na ofisi yake, madai ambayo CAG aliyaeleza alipoulizwa na mwandishi wa habari wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.

Profesa Assad alilazimika kufika mbele ya Kamati hiyo kujieleza kuhusu kauli yake hiyo iliyodai kuwa imelidhalilisha Bunge.

Mijadala mingi na mkali iliibuka katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuhusu hatua iliyochukuliwa na Ndugai na hata kuhoji kuhusu mamlaka inayoweza kumwajibisha CAG kwa kutumia vifungu mbalimbali vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Uamuzi wa CAG unatoa taswira ya burasa iliyo ndani ya kiongozi huyu wa umma, kiongozi ambaye amekuwa muwazi hata kwa mambo magumu ambayo pengine miongoni mwetu tusingethubutu kuyasema.

Pamoja na msukumo mkubwa kutoka kwa watu mbalimbali wakiwamo wanasiasa pasi kujali ukuu wa nafasi ya ofisi yake wala kinga aliyonayo kikatiba, aliona ni busara kuitikia wito wa Spika.

Katika kile ninachoweza kukiita kuwa ni ukomavu katika uongozi, Profesa Assad, hakutaka kuwa mbishani tangu Spika alipoutangazia umma kumwita katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, bali alibaki kuwa mkimya hadi hapo apoamua kuita vyombo vya habari na kueleza kuitikia wito huo.

Taswira inayopatikana kupitia uamuzi huu wa CAG umeonyesha kile tunachokiita uongozi bora unaohusisha kujinyenyekeza badala ya kujikweza na kutaka kujionesha miongoni mwa wengi.

Kwa kuzingatia kuwa Katiba ndiyo sheria mama ya sheria zote katika nchi hii, ambayo pia imetoa namna ambavyo kiongozi huyo anaweza kuwajibika ni wazi kuwa angeweza kususia wito wa Spika.

Nimpongeze CAG kwa kutambua umuhimu wa Bunge katika utekelezaji wa majukumu ya ofisi yake. Kama tunavyofahamu Bunge ndilo linalopaswa kupitia na kuchambua hoja mbalimbali zinazowasilishwa na ofisi ya CAG hivyo ni lazima taasisi hizo ziwe na uelewano ili kuhakikisha zinatenda kazi katika ufanisi kwa manufaa mapana ya Taifa.

Ikumbukwe kuwa tayari Spika ameeleza kutoendelea kufanya kazi na CAG jambo ambalo si la afya katika ustawi wa Taifa letu, kwa sababu kutofanya hivyo ni wazi kuwa kutawanyima wananchi haki ya kushuhudia mambo yanayoibuliwa na ofisi ya CAG yanashughulikiwa na chombo hicho kinachowawakilisha.

Tunakumbuka jinsi ambavyo kashfa mbalimbali kama vile Escrow na EPA zilizoibuliwa katika taarifa mbalimbali za ukaguzi na kuwezesha wahusika kuchukuliwa hatua stahiki. Hivyo kutokana na umuhimu huo ni wazi kuwa ofisi ya CAG inahitaji huduma ya Bunge ili kufikia ufanisi wa kazi zao kwa kuhakikisha hatua zinachukuliwa kama inavyoelekezwa.

Hakiwezi kufikia ufanisi unaoridhisha kama ripoti na utendaji wake hazitafanyiwa kazi ya kuridhisha na kwa wakati na Bunge.

“Tumekuwa tukifanya kazi vizuri kwa kuaminiana na wenyeviti na wajumbe wa kamati za Bunge, uhusiano huu ni muhimu  katika kutekeleza majukumu yetu,” alisema Profesa Assad.

Tunachopaswa kutambua ni kwamba, kinacholengwa na CAG ni kuwapo kwa uelewano kati ya taasisi hizi na si baina ya Spika na CAG, kwa sababu kutokuwapo ushirikiano baina ya vyombo kuna athari kwa Taifa kuliko athari ambazo zinaweza kupatikana endapo wawili hao hawatakuwa na uelewano.

Hivi karibuni Spika Ndugai alikaririwa na vyombo mbalimbali vya habari akisisitiza kuwa msimamo wao uko pale pale na kwamba katu hawezi kukubali ofisi yake iitwe dhaifu.

Sitaki kusema kuwa msimamo huu wa Spika ni mbaya, bali kama kiongozi wa chombo kikubwa na muhimu cha uamuzi anapaswa kuwa mstahimilivu na mwenye busara zaidi katika kushughulikia jambo lolote linalohusisha ofisi yake dhidi ya taasisi nyingine za umma.

Kwa kuzingatia nafasi ya viongozi na heshima zao katika jamii viongozi wote akiwamo Spika kutanguliza hekima zaidi katika kushughulikia mambo wanayoona yanakwenda kinyume cha yale wanayoyaamini.

Kwa mfano katika utaratibu ambao Spika aliutumia kumwita CAG, haukuwa wa kufurahisha na wenye fedheha kwa kiongozi huyo kwa sababu zilikuwapo njia nzuri za kumwita kwa barua badala ya kwenda mbele ya vyombo vya habari na kutamka bayana kuwa anamtaka kufika mbele ya Kamati ya maadili.

Kama viongozi ilikuwapo nafasi ya kuwasiliana japo kwa simu kupata ufafanuzi wa jambo lenyewe, ili kuepusha hali inayoweza kuzua taharuki katika jamii na kuibua maswali yanayowafanya wananchi kujiuliza mivutano hii inalenga nini.

Kwa kutumia mfano wa hatua iliyochukuliwa na CAG, inaonyesha wazi kuwa wako viongozi wanaotambua umuhimu wa nafasi zao katika Taifa.

Wanaweza kuwapo baadhi ya watu wanaoweza kuona hatua ya CAG unaashiria kushindwa kwake. Bali binafsi ninaitazama hatua kama kioo kwa watendaji na viongozi mbalimbali wa umma kujipima kama wanayoyafanya yanaendana na matakwa ya utawala bora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles