28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Bunge kusimamisha mshahara wa Lissu

*Spika Ndugai adai hana taarifa za mahali alipo wala ripoti ya dakktari

*Atangaza uamuzi huo baada ya mwongozo wa Mbunge Msukuma, Kangi amtaka arudi kukamilisha upelelezi

RAMADHANI HASSAN-DODOMA

SPIKA wa Bunge Job Ndugai,  amesema atasimamisha Mshahara na Malipo yote ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), kutokana ana ofisi yake kutokuwa na taarifa sahihi ya mahali alipo kwa sasa na anachokifanya huko.

Uamuzi huo aliutoa jana bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu mwongozi wa Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma (CCM),  ambapo alisema mbunge huyo hayupo hospitali, Bunge na hayupo Tanzania wala hajulikani anafanya kitu gani huko aliko hivyo hana sababu ya kuendelea kulipwa.

Katika mwongozo huo Musukuma,  alihoji ni lini Bunge litasitisha mshahara wa Lissu,  kwa kuwa ameshapona na anazurura huku Bunge likiendelea kumlipa mshahara.

“Kwa kuwa leo (jana), tunajadili taarifa ya kamati na tunajadili taarifa ya Wizara ya Afya na kwakuwa zipo sheria zinazoweza kumruhusu mtu kuitwa mgonjwa lakini tunaona Mheshimiwa Tundu Lissu , anazunguka kwenye nchi mbalimbali lakini huku anasomeka kama mgonjwa.

“Sasa Mheshimiwa Spika nilikuwa naomba mwongozo wako ni lini Bunge litasitisha mshahara wake kwakuwa ameshapona anazurura na Bunge linaendelea na yeye hayupo na mnaendelea kumlipa mshahara.

“…na anazunguka nje anatukana Bunge, anatukana viongozi, nilikuwa naomba mwongozo wako Mheshimiwa Spika,” alihoji Musukuma

Akijibu Spika Ndugai,  alisema ipo haja ya kusimamisha malipo ya aina yoyote ile ya Lissu, mpaka hapo ambapo ofisi ya Bunge itakapopata taarifa rasmi yupo wapi na anafanya nini.

“Ni kweli jambo hili kwa ndugu yetu, Mbunge mwenzetu Tundu Antipas Lissu, linahitaji kuangaliwa kipekee kwa maana ya kwamba mbunge hayupo jimboni kwake, hayupo hapa bungeni anapofanyia kazi, hayupo hospitalini, hayupo Tanzania.

“Na taarifa zake Spika hana kabisa, wala hajishughulishi hata kumwambia niko mahali fulani au nafanya hivi na kama ni mgonjwa hakuna taarifa yoyote ya daktari halafu unaendelea kumlipa malipo mbalimbali,” alisema

Spika Ndugai alisema hoja ya Musukuma ni ya msingi na kuna haja ya kusitisha malipo yake.

“Nadhani hoja yako ina msingi kwamba ipo haja ya kusimamisha malipo ya aina yoyote ile, mpaka hapo ambapo tutapata taarifa rasmi za yupo wapi na anafanya nini.

“Kwa sababu hatuna reference (kumbukumbu),  na tulikuwa tunafahamu yupo hospitali na tunamwona yupo duniani kwa maneno ya Mheshimiwa Musukuma anazurura, kwa hiyo nikuhakikishie Mheshimiwa Musukuma yale yaliyo ndani ya uwezo wangu nitayafanya asante kwa ushauri,” alisema Spika Ndugai.

KANGI AMTAKA LISSU

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Kangi Lugola amemtaka Lissu aje Tanzania ili awasaidie upelelezi kwani wameshindwa kuendelea na kesi kutokana na kukosa ushahidi.

Akihitimisha mjadala wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Lugola alisema mara baada ya kukosa ushirikiano wameshindwa kuendelea na kesi hiyo.

“Niendelee kutoa maelezo kwanini kesi zinachelewa Mheshimiwea Tundu Lissu mara baada ya kutoka hospitali tulitarajia kwamba angekuja kutokana na uchungu wa kesi yake ili kulisaidia Jeshi la Polisi ili tuweze kupeleka kesi mahakamani.

“Tunashindwa kuendelea kwa sababu wanaohusika wanatelekeza kesi ni matarajio yangu Watanzania wote wanaokuwa na kesi za jinai lazima watoe ushirikiano ili kuondoa lawama, ilihali mnatelekeza kesi zenu.

“Nimalizie kwamba katika mazingira ambayo wasitumie mbinu zao kwamba Serikali inahusika ilihali hawataki kutoa ushirikiano,” alisema Lugola

Hivi karibuni Lissu, alianza ziara barani Ulaya  ambapo hadi sasa amekwenda kwenye nchi za Uingereza ambako ambapo alifanya mahojiano na Shirika la Utangaza la Uingereza (BBC),  ambapo alieleza kuhusu kupigwa kwake risasi na hali ya kisiasa nchini.

Ziara ya Lissu ilinza baada ya kuhitimisha safari ya matibabu aliyoanza Septemba 7, 2017 baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana kwa zaidi ya risasi 30 mjini Dodoma muda mfupi baada ya kutoka kuhudhuria kikao cha mchana cha Bunge.

Lissu alikwenda Ubelgiji Januari 6 mwaka jana kuendelea na matibabu akitokea Hospitali ya Nairobi, Kenya na katika kipindi chote cha matibabu, amefanyiwa upasuaji mara 22.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles