25.7 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

Bulaya amtaka Jenista ajiuzulu uwaziri


ANDREW MSECHU – dar es salaam

WAZIRI Kivuli, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Esther Bulaya amemtaka Waziri Jenista Mhagama ajali misingi ya uwajibikaji kwa kujiuzulu wadhifa wake kutokana na kushindwa kusimamia masilahi ya wafanyakazi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Bulaya ambaye ni Mbunge wa Bunda (Chadema), alisema hatua ya Rais  Dk. John Magufuli kutengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Irene Isaka na kuwaacha wengine wanaotakiwa kuwajibika imeibua utata, kwa kuwa mkurugenzi huyo ni mtendaji tu.

Alisema sheria ya mafao ya mwaka 2018 imempa Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu mamlaka ya moja kwa moja ya kutunga na kusimamia kanuni za ukokotoaji wa mafao, hivyo Jenista anatakiwa kuwajibika au laa awajibishwe kwa kutojali maoni ya wadau wakati wa utafutaji na upitishaji wa kikokotoo ambacho Rais Magufuli alikitengua.

“Kutengua uteuzi wa Mkurugenzi wa SSRA na kumwacha waziri si sahihi, kwa sababu utungaji wa kanuni unasimamiwa moja kwa moja na waziri. Katika hili viongozi tuwe na utamaduni wa kuwajibika, haiwezekani huyu waziri aendelee kuwepo tu.

“Katika hili, Rais aingilie kati, amfurumushe au laa ajiuzulu mwenyewe kwa sababu yeye ndiye aliyetunga hizi kanuni. Ni wazi kwamba mchakato wa utungaji wa sheria yoyote huanzia katika Baraza la Mawaziri, nadhani hata mwenyekiti wa baraza hilo anastahili kuomba radhi kwa wananchi, kwa sababu sheria hiyo ilianzia kwenye vikao anavyoongoza na yeye ndiye aliyetia saini ianze kutumika,” alisema.

Bulaya alisema Rais aliainisha wazi pia suala la matumizi mabaya ya fedha za mifuko na kuwekezwa katika miradi isiyolipa, lakini wale wote waliohusika katika matumizi hayo mabaya na uwekezaji huo bado wapo na wanaendelea na nyadhifa mbalimbali serikalini.

Alisema kwa kauli ya Rais ni kwamba wote waliohusika katika uwekezaji na matumizi hayo mabaya wanatakiwa pia wawajibike.

KIKOKOTOO

Kuhusu kikokotoo kipya kilichoanza kutumika Agosti, mwaka jana hadi Rais alipozuia Desemba, Bulaya alisema kilikuwa kibaya zaidi kwa kuwa kilinuia kuwapunja wafanyakazi stahili zao.

Alisema hata kikokotoo cha zamani ambacho Rais alielekeza kiendelee kutumika, bado kina upungufu mkubwa kwahiyo ipo haja ya kukaa chini na kutafuta kanuni mpya zitakazowanufaisha wafanyakazi wanapostaafu.

SHERIA KUREJESHWA BUNGENI

Bulaya alisema hata kabla ya kupitishwa kwa sheria mpya ya mafao ya mwaka 2018 walipinga baadhi ya mambo ambayo yanaifanya iwe dhaifu, hivyo ni vyema irudishwe bungeni kwa hati ya dharura iweze kufanyiwa marekebisho kwenye maeneo muhimu.

Alisema kwa kutambua nia njema ya Rais, ni vyema Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), atumie nafasi yake kuirejesha bungeni kwa hati ya dharura ili kufanya mabadiliko katika suala la mamlaka ya waziri, mafao ya kujitoa ambayo sheria hiyo inayazuia, kuweka idadi ya wajumbe wa bodi wanaowakilisha wafanyakazi na mengine yatakayoainishwa.

“Tunaona sasa hivi hali ya maisha ni ngumu, kampuni kila siku zinapunguza wafanyakazi kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji. Hapa kuna suala la fao la kujitoa ambalo hata wawakilishi wa wafanyakazi walilizungumzia vizuri katika kikao chao na Rais. Hili kwa sheria hii mpya halipo, imekataza, kwa hiyo hili nalo linatakiwa libadilishwe,” alisema.

Alisema iwapo hayo hayatafanyika, ni wazi kwamba suala hilo litakuwa limefanywa kisiasa kulainisha wapigakura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 na si vinginevyo.

“Kilichofanywa na Rais ni hatua ya awali kumtoa mgonjwa kwenye ajali. Sasa anatakiwa apatiwe matibabu. Suala hili lazima lije bungeni lisiishie tu kwa tamko la Rais, kwa sababu hii ni sheria. Liletwe bungeni kwa hati ya dharura ili liweze kubatilishwa, na hii ndiyo kazi ya Bunge ili liweze kutekelezwa,” alisema.

Akitoa mapendekezo kuhusu wajumbe wanaowakilisha wafanyakazi kwenye vikao vya uamuzi, alisema wanaona ni vyema angalau wawe theluthi mbili (2/3) ili wawe na nguvu katika kutetea maamuzi yanayozingatia masilahi ya wafanyakazi.

Bulaya alisema wanatambua kuwa hatua ya kuunganisha mifuko hiyo ilichukuliwa ili kuhakikisha mfuko wa PSPF ulioanzishwa mwaka 1999 na kupewa jukumu la kuwalipa mafao wafanyakazi ambao hawakuwa katika mfumo haufi na Serikali ilijipa jukumu la kutoa Sh trilioni nne ambazo hata hivyo haikuzitoa.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,897FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles