23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

Brahim Diaz muokota mipira tegemeo jipya Real Madrid

BADI MCHOMOLO

WACHEZAJI wengi wa soka wana historia kubwa ya maisha yao, wapo ambao walikuwa wauza mitumba mtaani, lakini baada ya muda maisha yao yakabadilika na kuwa mastaa wa soka duniani.

Wapo ambao walikuwa wagonjwa wakiwa na umri mdogo, magonjwa ambayo wengi hawakutarajia kuwaona wakija kuwa wachezaji wakubwa duniani kama ilivyo kwa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Brahim Diaz, nyota mpya ndani ya kikosi cha mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19, amejiunga na mabingwa hao wa Ulaya akitokea klabu ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Manchester City.

Maisha yake ya soka yalianza mwaka 2010, alipojiunga na klabu ya Malaga ya vijana, akiwa hapo alikuwa na melengo ya kuja kucheza soka la kulipwa katika klabu kubwa duniani. Alikuwa mmoja kati ya wachezaji wa timu ya vijana ambao walikuwa wanaokota mipira wakati wa michezo mbalimbali ya Ligi kwenye uwanja wao wa nyumbani La Rosaleda.

Wakati Diaz anaokota mipira ile inayotoka nje wakati wa mchezo, baadhi ya mastaa ambao walikuwa kwenye kikosi hicho cha Malaga ni pamoja na aliyekuwa kiungo wa Arsenal, Santi Cazorla na kiungo wa sasa wa Real Madrid, Isco.

Kinda huyo amejiunga na Madrid wiki iliopita kwa mkataba wa miaka sita na nusu, huku uhamisho wake ukikamilika kwa kitita cha pauni milioni 22, zaidi ya bilioni 64 za Kitanzania na mshahara wa pauni 60,000 ambazo ni zaidi ya milioni 175 za Kitanzania kwa wiki.

Novemba 2016, Diaz, aliwahi kuposti picha akiwa ameshika mpira mkononi huku akiwa anawaangalia Isco na Cazorla wakiwa wanafurahia moja ya jambo katika mchezo, hivyo kinda huyo aliandika; “Siku zote nimekuwa na lango la kuwa mchezaji wa kulipwa,” aliandika Diaz.

Ndoto hizo zilitimia tangu mwaka 2016, aliposajiliwa na mabingwa wa England, Manchester City. Kwa nafasi ya kiungo ambayo alikuwa anacheza, alikuwa na wakati mgumu wa kupata namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza, kwa kuwa alikuwa anakutana na ushindani kutoka kwa Raheem Sterling, Leroy Sane, Bernardo Silva na Riyad Mahrez.

Mbali na kuwa na wachezaji hao, aliweza kucheza jumla ya dakika 49 za Ligi Kuu England kwa kipindi chake, lakini alicheza jumla ya dakika 414 kwa jumla ya michezo yote kwenye Ligi mbalimbali.

Wiki iliopita wakati anatambulishwa na Real Madrid, mbele ya rais wa timu hiyo Florentino Perez, alisema kwamba, maamuzi ya kuondoka Manchester City na kujiunga na Real Madrid yalikuja na namna tatu kichwani mwake.

“Naweza kusema hii ni siku ya pekee katika furaha ya maisha yangu, sina zawadi maalumu ya kuizawadia siku hii, wakati nafanya maamuzi ya kuja kujiunga na Real Madrid nilikuwa na mambo matatu kichwani.

“Moja ni kucheza Real Madrid, mbili ni kucheza Real Madrid na tatu ni kucheza Real Madrid, hivyo ilikuwa ngumu kwangu kuweza kwenda klabu nyingine, najua jukumu la kuvaa jezi ya Real Madrid, nitahakikisha ninafanya kila kitu kwa ajili ya kutimiza malengo ya timu tangu siku ya kwanza,” alisema mchezaji huyo.

Kwa nafasi anayocheza kinda huyo, bado ana wakati mgumu wa kupigania namba ndani ya kikosi cha Real Madrid, baadhi ya wachezaji ambao atakuwa anapigania namba ni pamoja na Gareth Bale, Isco, Marco Asensio, Lucas Vazquez na Vinicius Junior,hivyo lazima aonesha ushindani wa hali ya juu.

Madrid msimu huu wamekuwa na wakati mgumu tangu kuandoka kwa aliyekuwa kocha wao Zinedine Zidane pamoja na mshambuliaji wake bora Cristiano Ronaldo ambaye amejiunga na Juventus ya nchini Italia. Rais wa Madrid, Perez, anaamini mchezaji huyo mpya anaweza kuwa na msaada mkubwa ndani ya kikosi hicho kutokana na kipaji alichonacho.

Huo ni usajili mpya ambao Real Madrid wanaamini wanazidi kuboresha kikosi chao kwa ajili ya kulinda heshima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles