EVANS MAGEGE – DAR ES SALAAM
BALOZI wa Mamlaka ya Palestina nchini, Hamdi Mansour AbuAli pamoja na mwanaharakati wa haki za binadamu Mashariki ya Kati, Dk. Uri Davis wamekipongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa msimamo wake wa kuunga mkono jitihada za Wapalestina katika kupigania haki zao.
Pongezi hizo zilitolewa Dar es Salaam katikati ya wiki wakati wa mkutano baina yao na wanahabari.
Kwa nyakati tofauti alisema wanatambua jitihada za Tanzania katika kuunga mkono haki za Wapalestana.
Kwa mara kadhaa Balozi AbuAli alisema CCM imekuwa alama muhimu inayoitambulisha Tanzania katika kuunga mkono harakati za utetezi wa haki za Wapalestina.
Alisema tangu Tanzania ilipopata uhuru, chama hicho tawala kimekuwa kwenye misingi ya kutetea haki za binadamu na kwa muktadha huo hakijawatenga wananchi wa Palestina wanaopita katika kipindi kigumu cha haki zao.
Aliongeza kwa kupongeza pia juhudi zinazofanywa na jumuiya ya kimataifa katika kupigania haki za wananchi wa taifa lake.
“Wananchi wa Palestina wapo kwenye kipindi kigumu, lakini nchi kama Tanzania hususani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakituunga mkono mara zote na leo mimi na Dk. Uri Davis tutakutana na uongozi wa CCM,” alisema.
Aliongeza kwamba mgogoro uliopo kati ya taifa lake na Israel si wa kidini bali ni wa kutafuta haki.
Aliomba mataifa mbalimbali kuendelea kushirikiana na Palestina ili kuhakikisha wananchi wa taifa hilo wanapata haki zao.
Mataifa mbalimbali ikiwamo Tanzania wameweka misimamo yao wazi juu ya kutaka wananchi wa Palestina wapate haki zao na kuheshimika kwa mikataba ya kimataifa iliyowekwa baina ya mataifa ya Israel na Palestina.
Kwa upande wake, mwanaharakati wa haki za binadamu Mashariki ya Kati, Dk. Davis ambaye ni raia wa Palestina mwenye asili ya Kiyahudi, alisema ndani ya mamlaka ya taifa hilo hakuna ubaguzi wa aina yoyote na Wapalestina kwa umoja wao pasipo kuangalia dini au kabila, wamekuwa wakipigania haki yao dhidi ya vitendo ovu vinavyofanywa na Israel.
“Mgogoro wetu na Israel si wa kidini wala jambo lolote, ila tunachokitaka ni haki tu, ulimwengu usidanganywe na suala la udini, ndani ya Palestina wapo Wakristo, Waislam na hata Wayahudi, vivyo hivyo kwa upande wa Israel, lakini kinachosababisha mvutano ni haki ya Wapalestina wanaokandamzwa na Waisraeli,” alisema Davis.