31.9 C
Dar es Salaam
Sunday, January 16, 2022

Akili za Ruge na muziki wa Bongo Fleva

RAMADHAN MASENGA

MWISHONI mwa miaka ya tisini na mwanzoni mwa miaka ya elfu mbili, muziki wa Dansi na Taarabu ulitawala kwenye redio, matamasha na akili za wapenda burudani Bongo.

Kama mtu alitaka kufanikiwa kupitia sanaa ya muziki, basi haraka angeshauriwa kujiingiza katika aina hiyo ya muziki.

Hiyo yote ilitokana na hamasa kubwa iliyokuwapo katika Dansi. Vijana wengi wa Kitanzania walianza kuiga kuanzia staili za nywele, mavazi hata lafudhi za kikongomani.

Ungeweza kupishana na Mhehe maeneo ya Kinondoni, Dar es Salaam na akajitambulisha kama mzaliwa wa Kivu nchini Kongo.

Hali hiyo ikaenea hadi kwa watangazaji wa vipindi vya muziki redioni ambao wengi wao walikosea kwa makusudi maneno ya Kiswahili ili waonekane ni wakongomani.

Wakati huo kina Defao na Awilo Longomba waliingia Tanzania kuchota fedha kwenye matamasha makubwa ya muziki na kipindi hicho vijana wa uswahilini walikuwa wanapambana na muziki ulioitwa wa kizazi kipya.

Walijitahidi kuimba usiku na mchana, walibadili mitindo ya kuimba kila siku, walitunga mashairi ya kila aina lakini hawakueleweka. Wazee na vijana wenzao wa makamo waliwaita wahuni.

Muziki gani hauna gitaa, hauna wacheza shoo, waimbaji wake hawaimbi kwa mitindo tuliyozoea? Vijana hao walidharauliwa sana na muziki wao ukapachikiwa jina la muziki wa wavuta bangi.

Hata redio nazo hazikuwapa nafasi lakini vijana hao hawakuchoka, walijitahidi kuandaa matamasha ila hawakupata watu. Walipoomba kutumbiza katika matamasha yaliyohusisha shughuli nyingine waliambiwa walipie fedha ndiyo waimbe.

Walilipa wakiamini siku moja muziki wao ungekuwa biashara. Ilikuwa ni ndoto ya kijasiri iliyoonekana ina upuuzi mwingi.

Ila baadaye mwanaume mmoja akatokea. Ni kijana Mtanzania aliyezaliwa Brooklyn nchini Marekani ila ni Muhaya wa Bukoba anaitwa Rugemalila Mutahaba.

Tulipenda kumuita Bosi Ruge au ‘Scofield’ mwenye tabia ya kusikiliza kuliko kuongea ambaye neon lake moja lilikuwa na thamani kubwa kila aongeapo. Muda ambao angeamua kufunua mdomo wake na kusema kitu, kila mmoja angependa kusikiliza ile sauti ya upole yenye kutia ujasiri, nasaha na mawazo makini.

Mwanaume huyu aliona fursa katika muziki wa kizazi kipya na kuamua kupambana ili uwe biashara. Wakiwa ndiyo kwanza wamefungua Clouds FM, waliamua kupambana ili muziki wa kizazi kipya uwe na taswira njema kwa jamii ili baadaye uwe biashara na kubadili maisha ya vijana wengi.

Haikuwa rahisi, ilikuwa ngumu lakini Ruge hakuishia kutaka redio aliyokuwa akiifanyia kazi ipige muziki huo tu hivyo alijitahidi kuwa karibu na wanamuziki ili kuweza kuwapa mbinu na mikakati ya kukabiliana na changamoto za muziki na maisha.

Ni mwanamuziki gani aliyefanya vizuri kwenye anga la Kimataifa ukasema Ruge hausiki katika mafanikio yake?

Japo huu ni ukweli mchungu kwa baadhi ya watu ila huwezi kuandika historia ya mafanikio ya muziki wa Bongo Fleva bila kumtaja Ruge Mutahaba ambaye alikuwa moyo wa mafanikio kwa wanamuziki wengi wa kizazi kipya.

Ile kuwapa nafasi vijana wa kizazi kipya ambao kwa mfumo rasmi wangeshindwa kutusua ni jambo litakaloendelea kuishi. Alifikiria kuanzisha nyumba ya vipaji THT, ambayo imesaidia vipaji vingi vya wasanii wenye majina makubwa sasa kwenye Bongo Fleva.

Ikumbuke stori ya Mrisho Mpoto ambaye alitengenezwa na Ruge aliyemwambia ili awe tofauti siyo dhambi kutembea peku bila kuvaa viatu kitu ambacho mpaka leo kimemfanya awe tofauti.

Mpoto, baada ya kuanza kupata mafanikio ya muziki na kufanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi 50,000,000 akamkimbilia Ruge ili amshauri anunue gari gani kama ilivyo kwa wasanii wengi wanadhani mafanikio ni kumiliki magari.

Wazo hilo Ruge alilikataa na akamshauri anunue shamba na kwa shingo upande alikwenda kununua shamba.

Leo hii lile shamba siyo tu limempa fedha za kununua gari la gharama analotembelea sasa hivi bali benki zipo tayari muda wowote kumpa mkopo wa milioni 500 kwaajili tu ya zile mboga mboga na matunda anayolima.

Vipi kama angekimbilia kununua gari? Pumzika kwa amani Ruge. Ulikuwa mwanga katika maisha ya wengi. Japo sina uhakika sana na utajiri wako ila hakika uwekezaji mkubwa uliofanya katika nafsi na mioyo ya watu utaendelea kuishi milele japo kuwa mwili wako utazikwa ardhini.

Kutokana na uchapakazi, ubunifu na malengo yake ilifikia kipindi wimbo wa msanii usipochezwa Clouds Fm, mwimbaji huyo anajiona siyo mwanamuziki.

Ruge, aliweza kugundua kipaji cha mtu hata kabla mtu mwenyewe hajajua na akampa njia ambayo akiifuata lazima afanikiwe jambo lililomuwezesha kugusa maisha ya kila mmoja wetu kuanzia kwenye sanaa, utamaduni, michezo, ujasiliamali, jamii, siasa na mengineyo.

Unaweza kuona watu wa ngazi zote kuanzia Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Magufuli mpaka watu wa chini kabisa wameguswa kwa namna moja aama nyingine na maisha ya miaka 48 ya Ruge kuishi duniani.

Mwili wa jasiri huyo mwonyesha njia ambao ulifika jana nchini ukitokea Afrika Kusini, unatarajia kuagwa leo katika viwanja vya Karimjee kuanzia saa 5 asubuhi na kuendelea kisha kesho kusafirishwa kwenda Bukoba mkoani Kagera kabla ya kuzikwa kijijini kwao siku ya Jumatatu.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
174,603FollowersFollow
530,000SubscribersSubscribe

Latest Articles