31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

ZITTO: BUNGE LIMEKOSA MSHAWASHA

Na MWANDISHI WETU -DODOMA

MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT –Wazalendo), amesema Bunge limekosa mshawasha ambao Watanzania wameuzoea.

Alisema hayo jana mjini Dodoma mbele ya Kamati ya Bunge ya  Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge wakati akijibu tuhuma dhidi yake.

Zitto ambaye alikamatwa juzi akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar e Salaam alisafirishwa jana saa 10 hadi Kituo Kikuu cha Polisi Dodoma na baadaye kufikishwa mbele ya kamati hiyo inayongozwa na Mbunge wa Newala Mjini, George Mkuchika.

Akiwasilisha utetezi wake uliobebwa na hoja 10, ambao baadaye ulisambazwa na chama chake kwa vyombo vya habari, Zitto alikiri kupata wito wa kamati Septemba 13, mwaka huu ili kujitetea.

Zitto anadaiwa kuandika kwenye mtandao wa Twitter kuwa “Bunge siku hizi ni  Idara ya Tawi la Utawala yanadhalilisha mhimili wa Bunge”. Zitto alikiri maneno hayo kuwa nia yake  na ameyatoa kama raia wa Tanzania.

“Ninaamini  kwa dhati kuwa Bunge la 11 limekuwa likifanya kazi kwa kuingiliwa na Serikali chini ya ndugu Rais John Magufuli.  Maneno na vitendo vya Rais yanaashiria kuwa Bunge halina uhuru wake na mimi kama mbunge nina wajibu wa kuonesha kutopendezwa kwangu na hali hiyo.

“Nina mifano kumi (10) kuthibitisha maelezo yangu hayo kama; Kuzuiwa kwa “Bunge Live” kwa kisingizio cha kupunguza gharama za uendeshaji wa mhimili wa Bunge.

“Wakati mikutano yote ya mhimili wa  Serikali, hasa ya Rais ikirushwa Live (mubashara) ni dalili ya wazi ya kufifisha sauti ya Bunge na kupandisha sauti ya Serikali.

“Hata vituo binafsi ambavyo  vilipanga kurusha Bunge Live bila malipo (na hivyo kutokuwa na  gharama) vilizuiwa, lakini vinarusha Live mikutano ya Rais.

“Kitendo cha uongozi wa Bunge kurudisha serikalini shilingi bilioni 6 bila ridhaa ya wabunge kwa kisingizio kwamba zimebaki kutokana na kubana matumizi, hii ni dalili ya wazi ya Bunge “kujipendekeza” kwa Serikali.

“Wakati uongozi wa Bunge ukirejesha kiwango hicho cha fedha, kuna taarifa  kwamba kamati nyingi za Bunge zinashindwa kutekeleza wajibu wake kwa sababu ya ukata.

“Sababu nyingine ni maelekezo ya mhimili wa Serikali kwa mhimili wa Bunge, kupitia maagizo  ya Rais Magufuli kwa Spika Ndugai kuwa “Awashughulikie wabunge” (kwa kuwafukuza bungeni) aliowaita “waropokaji” ili waje wazungumze nje ya Bunge na yeye Rais (Serikali) apate nafasi ya kuwashughulikia. Kauli hii ya Rais aliyoitoa wakati akipokea Ripoti ya Prof. Osoro kuhusu mikataba ya madini, Juni 12, 2017.

“Hii inaonesha picha iliyo dhahiri kuwa Bunge linapokea maelekezo kutoka serikalini ya kuwadhibiti wabunge hasa wanaoiwajibisha Serikali na hatujawahi kuliona Bunge likiyakana maelekezo hayo ya Rais kwa Spika,” alisema Zitto.

Alisema kitendo cha Bunge kuhariri hotuba za kambi ya upinzani kwa kushinikiza  kuondolewa kwa vipengele vinavyoikosoa Serikali hasa wakati wa Bunge la Bajeti ni kielelezo kingine.

Hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Mambo ya Ndani Nchi, Godbless Lema, iliamriwa kuondolewa maneno yanayohusu kashfa ya mkataba wa Lugumi.

Pamoja na hali hiyo alisema kauli ya Rais Magufuli ya Novemba 4, mwaka jana wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuwa “mzizi wa mhimili wa serikali ni mrefu zaidi kuliko mihimili mingine” mara baada ya kuulizwa juu ya matumizi ya Serikali nje ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge, unaonyesha dhahiri fikra ya mkuu huyo wa nchi kuwa juu ya ukuu wa mhimili wa Serikali dhidi ya Bunge.

“Kitendo cha ripoti ya Kamati ya Bunge ya Tanzanite na Almasi kusomwa  nje ya Bunge na kuwasilishwa kwa Waziri Mkuu na baadae kwa Rais bila kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni ili kuwekewa azimio la Bunge, kinaifanya kamati hiyo kuonekana kuwa ya Serikali badala ya Kamati ya Bunge.

“Kauli ya Rais kuwa Spika alimpigia simu kumuuliza juu wajumbe wa  kuwaweka kwenye Kamati za Bunge za Tanzanite na Almasi inaonesha dhahiri kuwa Spika anafanya kazi kwa maelekezo ya Rais. Bunge na  Spika hawajawahi kuikana kauli hii ya Rais.

“Kwa mara ya kwanza kwenye historia ya nchi yetu tumeshuhudia  mbunge akishambuliwa kwa risasi wakati mkutano wa Bunge ukiwa  unaendelea.

“Haijapata kutokea katika historia ya Bunge letu, wabunge kukamatwa ovyo mbele ya mageti ya Bunge na kusafirishwa usiku usiku bila hata Spika kujulishwa kama taratibu za mabunge ya jumuiya ya  madola zinavyotaka.

“Kitendo cha ‘watu wasiojulikana’ kummiminia risasi zaidi ya 30 Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) wakati akitoka bungeni kuelekea kwenye makazi yake.

“Ni dharau ya hali ya juu kwa mhimili huu. Ni tukio linalolenga kuliziba mdomo Bunge. Makala yangu ya nani alitaka kumwua Tundu Lissu (kwa lugha ya kiingereza) naiambatanisha katika maelezo yangu haya.

“Kitendo cha Serikali kutowasilisha ‘taarifa za utendaji wa robo mwaka’ kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti kama inavyotakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya mwaka 2014 ni dharau kubwa kwa mhimili wa Bunge,” alisema.

Zitto alisema ni dharau zaidi kwamba Serikali ilileta Muswada wa sheria kuondoa kifungu kinacholazimisha Waziri wa Fedha kutoa Taarifa hizo, na Bunge kupitisha kuwa Sheria,” alisema Zitto.

Katika hoja yake ya 10 alisema bajeti ya Bunge kutowekwa kwenye Mfuko wa Bunge kwa mujibu wa sheria na Spika kutakiwa kuomba vibali vya safari za wabunge kwa mkuu wa nchi hali ya kuwa ni mhimili unaojitegemea.

Mbunge  huyo wa Kigoma Mjini alisema ana mifano mingi ya kuonesha kama ushahidi wa jambo hili, ambapo kwa mujibu wa Katiba inatambua uwepo wa mihimili mitatu ya dola ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama.

Alisema tangu kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tano, kumekuwepo na kauli na matendo ya viongozi wa Serikali na Bunge yanayoashiria uelekeo wa Serikali kuminya na kuingilia uhuru wa Bunge.

Hata hivyo alimsifu Mwenyekiti wa Kamati, George Mkuchika kuwa ni miongoni mwa wazee anaowaheshimu kutokana na malezi yake kwa kipindi chote alichokuwa bungeni.

Alisema maoni yake yalilenga kulinda hadhi, haki, heshima na madaraka ya Bunge pamoja na kulinda heshima ya Spika, ili azitumie nguvu  alizonazo kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Bunge kulinda heshima na hadhi ya Bunge isiporomoke.

“Ni maoni yaliyolenga kuonesha imani niliyokuwa nayo juu yake (Spika), ni maoni yaliyolenga kulizindua Bunge juu ya hali ya kukosa mshawasha/msisimko ambao Watanzania wameuzoea.

“Tafsiri kuwa maneno yangu kwamba Spika hajafikia viwango vya maspika waliotangulia kabla yake kuwa ni kumdharau si sahihi. Maoni yangu yalilenga kutaka Bunge liyalinde yale mambo mazuri yaliyosimikwa na maspika hao wa nyuma katika kuisimamia Serikali. Ni ahadi ya Spika wetu, ndugu Ndugai, wakati wa kikao maalum cha Bunge cha msiba wa Spika wa Bunge la 9, Samuel John Sitta.

“Hivyo ni dhahiri, mimi kukumbushia ahadi hiyo ya Spika mwenyewe haiwezi kwa namna yoyote ile kuwa ni kudhalilisha Bunge na kumdhalilisha Spika,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles