33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

ZITTO ATOKA KORTINI NA TAMKO ZITO

PATRICIA KIMELEMETA NA JANETH MUSHI-DAR ES SALAAM, ARUSHA


MBUNGE wa Kigoma Mjini na Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema katika kongamano lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) juzi na kuchambua miaka mitatu ya Rais Dk. John Magufuli, ameona ukasuku wa watu kwa kushindwa kueleza jinsi hali halisi ya nchi yetu ilivyo mbaya.

Zitto alitoa kauli hiyo kuhusu kongamano hilo Dar es Salaam jana, baada ya kupandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka matatu ya uchochezi.

“Nimesikitika, limenipita, lakini kupitia kongamano hilo tumeona ukasuku wa watu kushindwa kueleza jinsi hali ya nchi yetu ilivyo mbaya, naamini tutapata muda mwafaka wa kuweza kufafanua kwa sababu ni lazima tuweze kutoa tafsiri mbadala wa kile walichokifanya wao jana (juzi). Naamini tunaweza kukifanya kwa pamoja. Nawataka Watanzania lazima tujenge mshikamano, tujenge ushirikiano mpana kwa ajili ya kubadilisha hali ya nchi yetu namna inavyokwenda.

“Hatuwezi kuwa na hali hii ambayo takribani viongozi wakubwa wote wa kisiasa katika nchi yetu wanakwenda mahakamani kila siku na maana yake ni kwamba hawawezi kufanya shughuli zao za kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Katiba, huu ni wito kwa sababu kila mtu ameshaumia, wafanyabiashara wameumia kwa kubambikiwa kesi,” alisema.

Pia akiwa nje ya Mahakama hiyo, baada ya kupata dhamana, aliwashukuru wapinzani wenzake kuungana naye tangu alipokamatwa Jumatano wiki hii na kusota rumande kwa siku mbili, hadi alipofikishwa mahakamani na alisema kitendo hicho kimeonyesha mshikamano.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwakilishwa na mawakili waandamizi wa Serikali, ambao ni Mutalemwa Kishenyi na Tumaini Kweka, huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na mawakili, Peter Kibatala, Omary Msemo, Jeremiah Mtobesya na Stephen Mwakibolwa.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, Wakili Kweka, alidai kuwa kati ya Oktoba 28, mwaka huu katika eneo la Kijitonyama, Dar es Salaam zilipo ofisi za Makao Makuu ya ACT-Wazalendo, akiwa anazungumza na waandishi wa habari, Zitto alitoa maneno ya uchochezi yaliyokusudia kugombanisha wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi.

Alidai maneno hayo ni pamoja na: “Watu waliokuwa na majeraha katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi wakiwa wamekwenda hospitali kupata huduma za matibabu katika Kituo cha Afya Nguruka, polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali Kituo cha Nguruka kupata matibabu, wakawafuata kule wakawauwa.”

Alidai maneno hayo ni kinyume cha sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016.

Pia alidai shtaka la pili linalomkabili Zitto ni kutoa maneno ya uchochezi kwa nia ya kuleta chuki kwa wananchi dhidi ya jeshi hilo.

Maneno hayo ni: “Lakini tumefuatilia kwa kina jambo hili, taarifa ambazo tumezipata kutoka Kijiji cha Mpeta-Nguruka Uvinza ni mbaya, ni taarifa ambazo zinaonyesha wananchi wengi wameuawa na Jeshi la Polisi pamoja na kwamba Afande Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, amekwenda kule halijatoa taarifa yoyote kuhusu wananchi kama hawa Wanyantuzu walivamiwa eneo la ranchi, kuna taratibu za kisheria za kuchukua na si kuwaua, wananchi wengi sana wamekufa.”

Shtaka la tatu ni pamoja na kutoa maneno ya: “Tulikuwa tukifuatilia kwa kina yanayojiri Uvinza tangu kuuawa kwa askari polisi wetu, tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza, zinaogofya mno. Tunaambiwa kuwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na polisi na wengine wakisemwa kuuawa hata wakiwa katika matibabu hospitali baada ya kujeruhiwa katika purukushani na Jeshi la Polisi.”

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Kweka, alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na wamewasilisha hati ya maombi ya zuio la dhamana kwa mshtakiwa huyo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo za kiusalama na kuiomba mahakama hiyo kuipokea.

Alidai kuwa, hati hiyo imetolewa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, John Malulu, aliyeiomba mahakama hiyo isitoe dhamana kwa mshtakiwa huyo kwa madai kuwa anaweza kuvuruga uchunguzi wa suala hilo kwenye maeneo husika.

Alidai kwa sababu upelelezi bado unaendelea katika maeneo husika ili kuangalia tukio la mauaji yaliyotokea na ikiwa atapewa dhamana, anaweza kuingilia upelelezi huo.

Hata hivyo, upande wa utetezi ukiongozwa na Kibatala ulipinga hoja hiyo kwa madai kuwa hati ya maombi ya dhamana haijakamilika kisheria.

Alidai kuwa, mashtaka yanayomkabili Zitto yanadhaminika na kitendo cha kumnyima dhamana si sawa, kwa sababu hati hiyo haijakidhi matakwa ya kisheria na kuiomba mahakama kuitupilia mbali.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili za Jamhuri na utetezi, Hakimu Shahidi alisema hoja ya kuzuia dhamana iliyotolewa mahakamani hapo haina mashiko, licha ya kuwasilisha hati ya maombi ya kuzuia dhamana.

Alisema unapotoa hati ya pingamizi za dhamana uwe na sababu za msingi zitakazoishawishi mahakama ili kuzuia mshtakiwa asipewe dhamana, lakini maelezo yaliyopo katika hati hiyo hayajitoshelezi kumnyima dhamana mshtakiwa huyo.

Alisema ushahidi wa kimaandishi hauna sababu za msingi zilizoeleza hadi mahakama ijiridhishe na kuzuia dhamana.

“Suala la kusema ataingilia uchunguzi wa mauaji yanayotamkwa na upande wa Jamhuri hayana msingi, kwa sababu hati ya maombi ya dhamana haijajitosheleza kumnyima dhamana mshtakiwa,” alisema.

Hakimu Shahidi alisema kutokana na hali hiyo, mahakama imemtaka mshtakiwa huyo kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya Sh milioni 10 pamoja na vitambulisho vinavyotambulika kisheria.

Zitto alikidhi masharti ya dhamana na kuachiwa na Hakimu Shahidi aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 26, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, amewaomba viongozi wakuu wa vyama vya upinzani vyenye wabunge viitishe mkutano wa dharura Dar es Salaam au Dodoma na wabunge wote wa upinzani wakutane kujadili namna ya kutafuta njia sahihi ya kupigania uhuru wa maoni, demokrasia na kuzungumza.

 

Akizungumza mjini hapa jana na waandishi wa habari, alisema: “Kupitia kikao hicho uwe mwanzo wa kukataa uonevu wa tabia hii na kama wanafikiri huo mkutano watazuia iwe chanzo cha kufanya kitendo cha kimageuzi ambacho kitatujengea uwezo wa Katiba kuheshimika, sheria na uhuru wa maoni katika taifa hili kwa sababu hatuwezi kuishi hivi, unaogopa kusema mtu akiuawa au kuonewa ili usikamatwe na kushitakiwa.

“Wabunge wa upinzani, huu ni wakati wa kuamka kikamilifu kupigania uhuru wetu wa kutoa maoni, hatuwezi kuwa wabunge  ambao maoni yetu yanachukuliwa kama mashitaka, yanachukuliwa kama uhalifu, mateso au dhihaka kwetu, nashauri jambo hili lifanyike kwa haraka.

“Watanzania wasipochoka wakati wenzao wanapotea, wanauawa, wasipochoka mambo haya wanawavunja moyo wanaojitolea, tunakoelekea Serikali kuwanyamazisha wapinzani watakuwa wameweza kuisaidia Serikali kutawala vizuri, ukimya ni usaliti mkubwa.”

Lema, ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alisema hali ya taifa imefika pabaya.

“Na kama Rais Dk. John Magufuli anafikiri maisha ni maendeleo ya vitu, basi anafanya makosa makubwa, maendeleo ni utu, haki na upendo kwa sababu hata ukijenga barabara kilomita milioni moja, shule ya kata ukaweka uwanja wa ndege, halafu watu wakaendelea kupotea, basi hivyo vitu vinapoteza thamani,” alisema.

Pia alivionya vyombo vya dola kuacha kuwasumbua wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa kwa kile alichodai kuwa kitendo hicho kitasababisha wengine kuhofia kuendelea kuwekeza hapa nchini, huku akitolea mfano wa kesi inayomkabili mfanyabiashara Akram Azizi, anayekabiliwa na mashitaka 75 ya uhujumu uchumi, ikiwamo ya kukutwa na nyara za Serikali, silaha 70, risasi 6,496 na kutakatisha Dola 9,018 za Marekani.

Alisema kitendo hicho kinaweza kukwamisha uchumi wa viwanda na kusababisha uchumi kuporomoka hadi kufikia wa nchi kama Zimbabwe.

Alisema watu mbalimbali, ikiwamo wawekezaji, hawana amani na alishawahi kushauri bungeni na anarudia tena kushauri kuwa kama kulikuwa na jambo baya kuhusu ubadhirifu wa mali za umma, Magufuli akutane na watu hao na wakubaliane namna ya kusonga mbele bila kuleta sura mbaya inayoonekana kwa sasa.

“Rais aweke kumbukumbu ya maneno yangu ndani ya mwaka mmoja kutoka sasa nchi hii inaweza ikaelekea mwelekeo wa Zimbabwe ulipo, maisha yatakuwa ni magumu, fedha zitakuwa hazipo na zitakuwa zimesababishwa na kitu kimoja cha msingi, hofu, wala si TRA, hofu imekuwa kubwa katika nchi hii kuliko kawaida, unaona wawezekezaji wanakamatwa.

“Ni kweli hakuna uhalifu mdogo, lakini mazingira yanatia shaka, nimeona mtu anaitwa Akram ambaye wanasema ni mdogo wake Rostam Aziz, amekamatwa na bunduki nyingi, fedha na vitu vingine, nimefuatilia kama Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ili niipongeze Serikali, lakini nimekuja kugundua siwezi kuipongeza.

“Lile suala lingekuwa ni hivyo jana (juzi) katika lile kongamano hizo kauli zingekuwa nyingi, lakini ikifika mahali nchi hii unakutwa na Dola 9,000 za Marekani ndani unapewa kesi ya utakatishaji fedha haramu kwa mfanyabiashara ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya uwindaji anapewa kesi,” alisema.

Pia alisema hofu iliyojengeka kwa Watanzania na wawekezaji itasababisha wakawezeke nje ya nchi na kuchangia kushuka kwa mapato nchini.

“Mtu mmoja anapofanyiwa uovu au jambo lake linaposhindwa kufanywa kwa usahihi tusipopiga kelele litakuja kwao, ni kama sisi tulipokuwa tunafanyiwa, akina Mo hawakupiga kelele, wamevuna walichopanda na hawa ni marafiki wa Serikali, ni walipa kodi wakubwa, mapato yatashuka, watapeleka fedha Dubai, Rais atakuja kugundua mbona ile sera yangu ya viwanda imeshindwa kufanya kazi, ni kwa sababu purchasing power hakuna tena.

“Nimeona barua ya kampuni ya uwindaji ile barua kama ingekuwa inapotosha, nilitarajia yule anayesambaza ambaye pengine ni msemaji wa kampuni hiyo awe amewajibishwa, haya yanafanyika kishabiki, ila nimwambie Magufuli hii dalili ya kusema twende na maendeleo mwaka 2020 aangalie, pengine kuna watu wanamhujumu ili aonekane ameshindwa kutawala au aonekane anafanya kazi kwa bidii,” alisema.

Alisema inawezekana Magufuli anapelekewa taarifa na watendaji wake kuonyesha wanafanya kazi, ila kazi hizo hazifanyiki kwa usahihi kwa sababu watu wanaumia na wengine wanateseka.

“Upelelezi wa kesi kama hii unaweza kukamilika baada ya miaka 10, kuna wakili Median Mwale ana mashitaka kama hayo, upelelezi haujakamilika huu mwaka wa nane, kuna jambo linasemwa lililopo mahakamani tusiingilie, hatuingilii, ila tunaingilia haki ya mtu, tunasema hivi, Polisi, Idara ya Usalama na Takukuru wanapofanya kazi ya kukamata watu ina impact kubwa,” alisema na kuongeza:

“Unajiuliza huyu amekamatwa na fedha ndani mfanyabiashara wa uwindaji, anapewa kesi ya utakatishaji fedha, ni nani nchi hii, Mhindi, mzungu, mswahili, Mchaga, Mkibosho, Mmarangu ataweka fedha Tanzania wakati anaweza akapita mpaka wa Namanga akaweka fedha huko, nakuhakikishia ukiangalia fedha ambayo imetoka Tanzania kwenda Kenya ni mabilioni mengi kwa sababu watu wana hofu. “Hivi labda mimi nimehongwa na Spika wa Botswana, ni mwanamke au nimehongwa na waziri wa biashara wa Botswana, ni mwanamke amenipa dola 10,000 unanikuta nazo ndani, unasemaje nimetakatisha fedha?

“Hatusemi polisi, Usalama wa Taifa wasifanye kazi kulinda rasilimali za nchi, ila hizi kazi zikifanywa bila uadilifu, busara, zinaleta hofu na ukileta hofu uwekezaji utakwama na watu wataondoka.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles