30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto aomba nafuu ya mahakama

TUNU NASSOR – DAR ES SALAAM

KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumwona hana hatia katika mashtaka matatu ya uchochezi yanayomkabili, kwa kuwa vithibitisho vyote vilivyotolewa kwa mahakama vinaonyesha hakuna maneno yenye uchochezi aliyotoa.

Zitto alianza kujitetea kwenye kesi ya uchochezi inayomkabili Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa siku tatu mfululizo, ambazo ni juzi na jana na anatarajiwa kumaliza leo.

Akiongozwa na wakili wa utetezi, Frank Mwakibolwa mbele ya Hakimu  Mkazi Mkuu Huruma Shaidi, Zitto alidai kuwa lengo la kuandaa mkutano wa waandishi wa habari lilikuwa ni kuitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina wa mauaji ya raia yaliyofanyika katika Kijiji cha Mpeta, Uvinza mkoani Kigoma.

Alidai lengo lingine lilikuwa ni kuiomba Serikali na Jeshi la Polisi kutoa taarifa za vifo vya raia tofauti na alivyofanya Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro.

“Hakukuwa na maneno ya uchochezi zaidi ya kuitaka Serikali irekebishe kwenye madhaifu na kuchukua hatua pale panapostahili,” alidai Zitto.

Alisema kwa mujibu wa sheria, kuna taratibu za kufuata wakati wa kuwaondosha watu waliovamia hifadhi hivyo alitaka taratibu hizo zifuatwe.

“Serikali ilikaa kimya bila kutoa taarifa kwa umma juu ya mauaji hayo, ndipo kupitia mkutano wa waandishi wa habari niliiomba kufanya hivyo,” alidai Zitto.

Aliiomba mahakama hiyo kufikia maamuzi kwa kutumia nyaraka ya taarifa kwa vyombo vya habari, video yote badala ya kutumia vipande vilivyonyofolewa na upande wa Jamhuri.

Awali, juzi Zitto aliieleza mahakama kuwa taarifa za mauaji hayo alipata kupitia vyombo vya habari na kutoka kwa Mbunge wa Kigoma Kusini, Husna Mwilima (CCM) ambaye alisema ndani ya Bunge kuwa wananchi wake zaidi ya 20 wameuawa na alitaka uchunguzi ufanywe.

Zitto alidai kuwa maudhui yaliyokuwa kwenye kielelezo namba tatu ambayo ni taarifa aliyosoma kwa waandishi wa habari yalikuwa ni kutaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina wa masuala yaliyotokea Kijiji cha Mpeta, Wilaya ya Uvinza huku akiongezea kuwa lengo lake lilielezwa wazi kuwa baada ya uchunguzi hatua za kisheria zichukuliwe kwa wote watakaobainika na mauaji ya wananchi.

Alidai kuwa hakuna shahidi wa upande wa mashtaka aliyeleta nyaraka kuonyesha kuwa uchunguzi umefanyika na hakuna mtu aliyefariki dunia.

Zitto amenukuu kwenye mahakama hiyo taarifa aliyoitoa kwenye vyombo vya habari Oktoba 28, 2018, akieleza kuwa “wiki iliyopita yalitokea mauaji ya askari polisi. Chama chetu kinatoa pole kwa IGP na kinalaani mauaji hayo na tunataka upelelezi ufanyike. Taarifa tunazipata zinaogofya mno, tumeambiwa raia zaidi ya 100 wameuawa na Jeshi la Polisi. Haiwezekani tukio kubwa kama hilo Serikali imekaa kimya.”

Zitto anatuhumiwa kwa makosa matatu ikiwamo kutoa maneno ya uchochezi anayodaiwa kuyatoa Oktoba 28, 2018.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles