27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto akutwa na kesi ya kujibu, kuanza kujitetea Machi 17

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amekutwa na  kesi ya kujibu, na mahakama imemfahamisha anatakiwa kufuata utaratibu kwa sababu mahakamani watu wote ni sawa.

Uamuzi huo ulitolewa jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Akitoa uamuzi, Hakimu Shaidi alisema kuwa amepitia ushahidi wote uliotolewa na mashahidi 15 wa upande wa mashtaka.

Alisema upande wa Jamhuri uliwasilisha majumuisho na kuonyesha wamethibitisha mashtaka, hivyo uliomba mahakama imuone mshtakiwa ana kesi ya kujibu.

“Upande wa utetezi katika majumuisho wanasema katika makosa yote matatu wanaona mshtakiwa hana hatia na wanaona Jamhuri hawajathibitisha kosa.

“Suala kwamba hayo maneno ni ya uchochezi ama hapana ni suala la ushahidi na kwamba ushahidi wa upande wa Jamhuri peke yake hauwezi kutosheleza, mshtakiwa lazima atuambie alitoa maneno hayo akiwa na maana gani.

“Aliyesema maneno lazima apewe nafasi ya kusema ili tujue alikuwa anamaanisha nini kutaja maneno hayo na alifanya mkutano na waandishi na akatoa taarifa kwa vyombo vya habari,” alisema Hakimu Shaidi.

Alisema kwa mantiki hiyo, mahakama inaona mshtakiwa ana kesi ya kujibu kwa aliyoyatamka kwa uhalisia wake.

Baada ya uamuzi huo, Zitto alipewa nafasi ya kueleza atajitetea kwa utaratibu upi na alijibu atajitetea kwa njia ya kiapo na ataanza kujitetea Machi 17 hadi 20.

Awali Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka, alidai kesi hiyo ilikuja kwa uamuzi, lakini wanataka kufahamu kwa nini Zitto hakufika mahakamani Februari 10, mwaka huu wakati kesi yake ilipokuja kwa uamuzi.

Akijibu hoja hiyo, Zitto alidai alikuwa anaumwa na alitoa barua za hospitalini kuthibitisha kuumwa kwake.

Wakili Kweka alidai barua hiyo hawaielewi kwani haina nembo wala stempu ya kuonyesha imetolewa hospitali, lakini Zitto aliwajibu kuwa waende ubalozi wa Marekani kujiridhisha na kwamba yeye ni kiongozi hawezi kufanya kitu kibaya.

Akitoa majibu kuhusu hoja hiyo, Hakimu Shaidi alisema barua hiyo haina stempu ya hospitali, lakini kwa sababu alihudhuria mwenyewe mahakamani bila kukamatwa anatakiwa kuzingatia utaratibu.

“Tunakuhitaji mahakamani, tunapokuwa mahakamani watu wote ni sawa, haijalishi una nafasi gani, uzingatie hilo,” alisema Hakimu Shaidi.

Katika kesi ya msingi, Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi ambapo, anadaiwa Oktoba 28, 2018 akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, uliofanyika Makao Mkuu ya ofisi ya Chama cha ACT Wazalendo, alitoa maneno ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.

Inadaiwa kuwa mshtakiwa alitamka; “watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika Kituo cha Afya Nguruka, polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali Kituo cha Afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua.”

Katika shtaka la pili, ilidaiwa Oktoba 28, mwaka huu maeneo ya Kijitonyama, Dar es Salaam katika makao makuu ya chama hicho, Zitto alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi akisema; “lakini tumefuatilia kwa kina jambo hili, taarifa ambazo tumezipata kutoka kijijini Mpeta-Nguruka, Uvinza ni mbaya.

“Ni taarifa ambazo zinaonyesha wananchi wengi sana wameuawa na Jeshi la Polisi pamoja na kwamba Afande Sirro (Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro) amekwenda kule, haijatoa taarifa yoyote kuhusu wananchi. Kama hawa Wanyantuzu walivamia eneo la ranchi kuna taratibu za kisheria za kuchukua na sio kuwaua, wananchi wengi sana wamekufa.”

Ilidaiwa kuwa katika tarehe hiyo hiyo, Zitto alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi akisema; “Tumekuwa tukifuatilia kwa kina yanayojiri yote huko Uvinza, tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno, kwani tunaambiwa kuwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na polisi, wengine wakisema kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na Jeshi la Polisi.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles