24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

ZIJUE DILI ZILIZOJIFICHA ZENYE PESA NDEFU – 2

Na ATHUMANI MOHAMED

NI Jumamosi nyingine tena tumepata bahati ya kukutana kwenye kona hii ambayo lengo lake ni moja tu, kubadilisha akili za watu kuwa zenye mitazamo ya kimafanikio.

Siku zote tumekuwa tukikutana hapa na kujadiliana namna tunavyoweza kuyabadili maisha yetu kupitia mbinu mbalimbali zinazopendekezwa na wajasiriamali waliofanikiwa.

Bila shaka kuna mengi unajifunza na maisha yako yanabadilika. Lakini kama ni mara ya kwanza kuanza kusoma safu hii, karibu sana na ninakuhakikishia kwamba hutajutia uamuzi wako wa kuanza kuwa mdau wa kona hii kila Jumamosi.

Mada ya leo ni kama inavyojieleza hapo juu ambayo ilianza wiki iliyopita. Kuna dili gani mjini ambazo unaweza kuzifanya kwa kumfuata mteja alipo bila ya kuwa na ofisi? Ndiyo mada inayoendelea.

Kumbuka, wakati fulani watu wanaweza kuwa na fedha nyingi, lakini wakakosa muda. Tumia fursa hiyo kama mtaji wako wa biashara. Ndiyo msingi wa mada yetu ya leo.

UREMBO/MITINDO

Hii ni fursa nyingine ya kutengeneza fedha. Inawezekana umesomea mambo ya mitindo na urembo au unapenda na una ujuzi wa mitindo na urembo lakini hujapata kazi na huna uwezo wa kufungua ofisi mahali ili uendeshe huduma hii, usijali, ofisi ni wewe mwenyewe.

Kwa kutumia mfumo uleule wa mitandao ya kijamii unaweza kujitangaza. Wapo watu wengi wako busy na kazi, lakini wanapenda mtu maalum ambaye atamfuata ofisini kwake au nyumbani na amshauri namna ya kuvaa na kujipodoa kulingana na mwili na ngozi yake.

Kama ulikuwa hujajua, basi nimekupa dili hilo, shtuka na uchangamkie hiyo fursa haraka itakutoa.

MSHAURI BIASHARA

Wengi hufanya kazi hii kwenye ofisi zao au walipoajiriwa, lakini kama wewe ni mtaalamu wa masuala ya kibiashara na hujapata kazi mpaka sasa, naweza kusema kazi ni kwako! Wapo watu wanaopenda kuwezeshwa mawazo kazini kwao.

Pengine kuna kampuni inahitaji kuwapa wafanyakazi wao semina ya biashara lakini wana tatizo la muda, nafasi ni yako.

Acha kuwa na tamaa ya kufikiria kupata fedha nyingi. Kwa kuanzia toza fedha kidogo, lakini namna unavyotoa huduma yako, inaweza kukutangaza na kupata watu wengi zaidi na kama ufanisi utakuwa mkubwa vya kutosha.

Siyo ajabu baadaye ukafungua kampuni yako kubwa na kuwaajiri wengine wenye utaalamu kama wako. Wajasiriamali wakubwa huendelea kuingiza fedha nyingi kwa kuzungumza tu, tena kwa hesabu za dakika.

Kila dakika moja inalipiwa. Kwanini wewe usifanye hivyo, unabaki kusubiria kuitwa kwenye usaili? Tumia akili yako ya ziada.

UPISHI

Sherehe kila siku haziishi, kuna kipaimara, birthday, harusi nk lakini siyo wote wana fedha nyingi za kuandaa vyakula. Wengi wanapowaza kuhusu hafla na hasa zile za kufanyikia kwenye kumbi mawazo yao huenda kwenye bajeti ya chakula.

Siyo wote wana uwezo mkubwa, hivyo kwa kutambua hilo, wewe mwenye ujuzi wa mapishi unaweza kutengeneza fedha nyingi kwa kutafuta oda kwenye sherehe mbalimbali.

Unaweza kuanza kidogokidogo, lakini baadaye sifa zako zitasambaa na utaweza kuwa na oda nyingi kwa wateja wengi zaidi.

DILI NI NYINGI

Kuna dili nyingi za kufanya na hizo nimekupa chache kati ya nyingi ambazo zinaweza kubadilisha historia ya maisha yako. Kwa kumalizia nitakutajia dili nyingine kama huduma ya ususi wa nywele, kutengeneza nywele za kike, kuwapamba maharusi, ubunifu mavazi, teknolojia ya mawasiliano na nyingine nyingi.

Acha mazoea ya kulalamika kila wakati. Kazi zipo nyingi tu ila wengi hatuzifikii. Ukishughulisha ubongo wako, utakuwa wa tofauti na maisha yako yatabadilika.

Kwa leo mimi naishia hapa, hadi wiki ijayo panapo majaliwa ya Mola. Wako katika mafanikio, naitwa Athumani Mohamed, wasalaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles