Ziara ya Majaliwa Kagera yaondoka na kigogo wa polisi

0
525

 

Na FERDNANDA MBAMILA – DAR ES SALAAM


SIKU moja baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutuhumu polisi wa Wilaya ya Kyerwa kusindikiza kahawa za magendo kwenda nchi jirani, Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Justin Joseph, amehamishwa kituo cha kazi.

Juzi Majaliwa alimwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi kuwachukulia hatua askari polisi wote wa Wilaya ya Kyerwa wanaotuhumiwa kusindikiza kahawa ya magendo pamoja na OCD Joseph.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana,  Kamanda Msaidizi wa Polisi, ACP Barnabas Mwakalukwa alisema kufuatia maelekezo ya Waziri Mkuu, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro ametuma timu ya upelelezi kutoka makao makuu ili kujua ukweli wa suala hilo.

“Kufuatia uchunguzi huo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kyerwa, Mrakibu wa Polisi Justine Joseph, atahamishiwa kituo kingine cha kazi na kuwa chini ya viongozi wengine  kwa kipindi chote cha uchunguzi ili kuipa nafasi timu hiyo kufanya uchunguzi kwa uhuru na haki na hatimaye kupata ukweli juu ya tuhuma hizo,” alisema ACP Mwakalukwa.

Alisema watakaobainika kuhusika na tuhuma hizo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu za polisi.

“Inspekta Jenerali wa Polisi (Sirro) amesikitishwa na tuhuma hizo kwa askari na kuwataka askari polisi wote nchini kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za polisi bila kusahau misingi na kanuni za maadili,” alisema Mwakalukwa.

Alisema pia IGP Sirro ametoa rai kwa wananchi na waganga wa kienyeji kuacha kupiga ramli chonganishi kwani vitendo hivyo vimekuwa vikisababisha uhalifu na uvunjifu wa amani.

Juzi Majaliwa baada ya kukagua kiwanda cha kukoboa kahawa cha Nkwenda wilayani Kyerwa, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Kagera, alisema; “Askari polisi wa Wilaya ya Kyerwa pamoja na OCD wao, wanatuhumiwa kusindikiza kahawa inayosafirishwa kwa njia ya magendo kwenda nchi jirani kupitia njia zisizo rasmi zikiwemo za Kumisongo, Kashaijo na Omukatoma.”

Waziri Mkuu alisema ni jambo la hatari kama askari polisi wanasindikiza kahawa inayouzwa kwa magendo, hivyo akaagiza jambo hilo lidhibitiwe haraka.

 

MINADA YA KAHAWA

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema kuanzia msimu ujao wa kahawa, minada yote ya kahawa inayozalishwa mkoani Kagera itafanyika ndani ya mkoa huo badala ya kufanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.

Alisema minada yote ya kahawa ikifanyika mkoani Kagera itawawezesha wakulima kulipwa fedha zao kwa muda mfupi na pia itapunguza makato yasiyokuwa ya lazima ambayo ni kero kwa wakulima.

“Wanunuzi watafuata kahawa ilipo, utaratibu huu utawawezesha wakulima kulipwa fedha zao kwa wakati. Mnada ukifanyika katika maeneo ya uzalishaji utamwezesha mkulima kujua bei, tofauti na unavyofanyika Moshi kwani ni rahisi mkulima kuibiwa,” alisema.

Aliwataka wananchi kuendelea kuwa na imani na Serikali yao ambayo imedhamiria kuwaletea maendeleo na kwamba itahakikisha kila mmoja anapata haki yake wakiwemo wakulima.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here