30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Ziara ya JPM yaja na uamuzi, mapendekezo nane

Na MWANDISHI WETU

ZIARA ya Rais John Magufuli aliyoifanya katika mikoa Mwanza na Dodoma mapema wiki hii kabla ya kurejea Dar es Salaam juzi, imesababisha kufanyika kwa  maamuzi na kuja kwa mapendekezo makubwa nane.

Miongoni mwa mapendezo hayo yapo yale ambayo yanaweza kusababisha kukafanyika marekebisho katika baadhi ya sheria nchini yatakayosaidia kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani.

Pia katika kile kinachoonekana kuwa ni matokeo ya ziara hiyo, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Biswalo Mganga, pamoja na wenzake Wizara ya Katiba na Sheria, wameanza kuzunguka kwenye magereza mbalimbali kuzungumza na wafungwa na kuachia wale waliobambikiwa kesi, watoto na wengineo.

Katika magereza ya Kanda ya Ziwa, tayari wafungwa na mahabusu zaidi ya 300 wameachiwa na sasa viongozi hao wamesema watapita pia kwenye magereza yote nchini.

 Lakini pia kauli ya Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma ya kupendekeza kufanyika kwa marekebisho ya sheria yatakayoruhusu watuhumiwa wa makosa yote yakiwamo ya mauaji kupewa dhamana ni matokeo ya kauli na maagizo aliyoyatoa  Rais Magufuli  akiwa katika ziara hiyo.

Akiwa mkoani Mwanza miongoni mwa kero ambazo Rais Magufuli alikutana nazo ni pamoja na msongamano wa wafungwa na gerezani ambapo akiwa katika Gereza la Butimba, alizungumza na wafungwa na mahabusu ambao baadhi walilalamikia kubambikiwa kesi na wengine rufaa zao kuchelewa.

Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli aliliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza chini ya Kamanda Jumanne Muliro kuhakikisha wanakamilisha upelelezi wa kesi za mahabusu zaidi ya 900 walio kwenye Gereza hilo.

Pia aliagiza Wizara ya Katiba na Sheria, na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama vinavyohusika na Mahakama kupita magereza yote,  kuzungumza na watuhumiwa walioko mahabusu ili wale ambao hawapaswi  kukaa huko waachiwe kwa mujibu wa sheria.

Akionekana kutafuta njia ya kuondokana na tatizo hilo akiwa Kongwa Dodoma, Rais Magufuli aliwaambia polisi waache kuwaonea raia wanyonge kwa kuwabambikia kesi.

Alisema mtu anashitakiwa amegombana na mkewe au ameiba kuku anawekwa mahabusu lakini hapelekwi mahakamani.

Alitolea mfano kijana aliyemkuta katika Gereza la Butimba akiwa amepewa kesi ya mauaji wakati ukweli ni kwamba alikamatwa na madumu ya mafuta dizeli na polisi wakataka wapewe rushwa ya Sh milioni moja, kijana huyo aliposema anaweza kutoa Sh laki moja pekee, akapewa kesi ya mauaji.

Baada ya Rais kuguswa na changamoto hizo, huku akisema hawezi kuongoza nchi ya machozi kutokana na vitendo kama hivyo, sasa viongozi wameonekana kuchukua hatua.

Katika gereza la Butimba watuhumiwa 75, waliachiwa Wilaya ya Bariadi 100, Mugumu Serengeti 52, Tarime sita, Bunda 24 na Kahama 43.

Miongoni mwa kesi ambazo zilifutwa na DPP ni pamoja na ile  Uhujumu Uchumi ya mwaka 2019 iliyokuwa ikiwakabili askari Polisi nane waliohusishwa na utoroshaji wa madini kilo 319 yenye thamnai ya Sh bilioni 27.

Tayari Rais Magufuli ameagiza askari hao warudishwe kazini ingawa ameonya iwe fundisho kwa askari wengine wapenda rushwa.

JAJI MKUU

Pengine katika mwendelezo wa kufanyia kazi agizo la Rais Magufuli la kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani, juziJaji Mkuu, Profesa Juma alipendekeza kufanyike marekebisho ya sheria yatakayoruhusu watuhumiwa wa makosa yote wapate dhamana.

Mapendekezo hayo ya Jaji Mkuu iwapo yatapokelewa na kufanyiwa kazi, yatasababisha kufanyika kwa marekebisho makubwa kwenye sheria nchini.

Jaji Mkuu pia alishauri mhimili wa mahakama uachiwe haki ya kusimamia dhamana yaani sheria isifunge dhamana na masharti ya dhamana yalegezwe kwa kuwa sasa watu wana vitambulisho vya Taifa.

Zaidi alipendekeza katika marekebisho hayo ya sheria  watu waruhusiwe kujidhamini wenyewe.

Aidha alishauri mamlaka zinazokamata kutofautisha jinai na mikataba.

Akitolea mfano mhandisi aliyeshindwa kukamilisha kazi mwenye mamlaka anaamrisha tu akamatwe na kuwekwa ndani.

Jaji Mkuu pia alishangaa kutotekelezwa kwa tangazo lilitolewa na DPP  linalokataza kukamata mtu kabla upelelezi haujakamilika kuwa ni miongoni mwa yanayochangia msongamano magerezani .

Pamoja na hilo alisisitiza kuharakishwa kwa upelelezi kwa kesi za mauaji, dawa za kulevya, uhujumu uchumi na ubakaji upelelezi wake huchukua muda mrefu kukamilika.

Alisema sababu nyingine inayofanya magereza yajae ni watu kupenda kutoa adhabu kali badala ya adhabu mbadala.

MAAGIZO YA JPM

Aidha agizo la Rais Magufuli kuhusu uharakishwaji wa ujenzi wa meli mpya na sambamba kuitaka Wizara ya Fedha na Wizara ya Uchukuzi kuhakikisha msamaha wa kodi ya makontena 56 ya vifaa kwa ajili ya ujenzi wa chelezo.

Alisema hadi Julai 20 (jana) vifaa hivyo viwe vimefika jambo ambalo limetekelezwa.

Pia Rais aliagiza ifikapo Machi 31 uundaji wa meli mpya, ukarabati wa meli za Mv Victoria na Mv Butiama sambamba mradi wa ujenzi wa chelezo uwe umekamilika.

Agizo jingine alilolitoa Rais Magufuli ni utiliwaji wa saini makubalino ya mkataba wa ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi linalopita juu ya Ziwa Victoria .

Katika hilo aliwataka  Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wakala wa Barabara nchini ( Tanroads) kutiliana saini ili mradi huo uanze kufanyika.

Pia Rais Magufuli alitoa maagizo kwa Mkoa wa Mwanza  kuhakikisha wanakamilisha jengo la wodi ya wanaume katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana ya Butimba  ifikapo Julai 30, 2019.

Kwa upande wa Halmashauri ya Sengerema kupitia Baraza la Madiwani, aliagiza kufanya marekebisho yatakayowawezesha kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami baada ya kubaini halmashauri ina bajeti ya karibu Sh bilioni 29 ambazo ni mapato ya ndani na ruzuku kutoka serikali kuu.

Pia aliagiza Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela kutoa bilioni nne kwa ajili ya ujenzi wa jengo la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles