24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Zanzibar yazindua mkakati kuimarisha sekta ya afya

Khamis Sharif – Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imezindua mkakati wa afya ya jamii wenye lengo la kuhakikisha huduma za afya zinaimarika zaidi, kuanzia ngazi ya familia, jamii na taifa kiujumla.

Mpango mkakati huo umezinduliwa na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali wakati wa mkutano wa 12 wa kutathmini shughuli za sekta ya afya Zanzibar huko Mtoni mjini Unguja.

Waziri Amina alisema Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kusambaza huduma za afya mijini na vijijini, lakini kuzinduliwa kwa mkakati huo kutapunguza changamoto za maradhi kwa wananchi zinazoendelea kujitokeza na kuongeza ufanisi katika sekta za afya.

Alisema Serikali itafanya kila juhudi ili kuhakikisha mkakati huo unakuwa endelevu, kwani unagusa nyanja mbalimbali, ikiwamo kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wakati wa kujifungua.

Aidha Balozi Amina aliwataka wafanyakazi watakaoshughulikia mpango huo kuhakikisha wanatumia nafasi hiyo kuona malengo yaliyowekwa yanafikiwa.

“Nielekeze shukurani kwa washirika wa maendeleo kuainisha michango yao mikubwa, hii ni hatua njema na uimara wa uhusiano wetu kwao, kwani mbali ya kusaidia kuimarisha sekta ya afya, pia michango yao huonekana katika sekta nyingine za elimu, maji, miundombinu na umeme,” alisema Balozi Amina.

Akizungumzia kuhusu mafanikio yaliyofikiwa katika sekta ya afya, Katibu Mkuu Wizara Afya Zanzibar, Asha Ali Abdalla alisema hatua kubwa imefikiwa katika kuimarisha Hospitali ya Mnazi Mmoja kutoka kuwa hospitali ya kawaida na kufikia kuwa ya rufaa na moja ya hospitali zinazotoa mafunzo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Alisema Serikali imefanya juhudi kuongeza madaktari bingwa na wafanyakazi wa kada nyingine za afya na kuongeza vitendea kazi muhimu katika hospitali na vituo vya afya ambavyo vinaongeza ufanisi wa kutoa huduma kwa sasa.

Aliongeza kuwa hatua zilizochukuliwa na Serikali pamoja na wananchi kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo Zanzibar imeweza kudhibiti maradhi ya malaria ambayo yalikuwa yakiwasumbua wananchi wengi na kuathiri nguvu kazi ya kuimarisha uchumi.

Alisema pia juhudi nyingine iliyochukuliwa ni ile ya  kudhibiti kuenea kwa virusi vya Ukimwi na kupunguza maradhi ya malaria pamoja na mengine nyemelezi nchini.

Mwakilishi wa Shirikiala la Afya Duniani (WHO) Zanzibar, Dk. Ghirmay Andemichael aliisifu SMZ kwa kufanikiwa kudhibiti malaria na kupunguza kusambaa kwa kipindupindu – magonjwa ambayo kwa miaka kadhaa iliyopita yalikuwa tishio kwa wananchi.

Alisema uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuongeza bajeti ya Wizara ya Afya kila mwaka, umeleta mafanikio makubwa katika kuwapatia huduma wananchi.

Dk. Andemichael alieleza kwamba washirika wa maendeleo wataendelea kushirikiana na SMZ katika kuimarisha huduma mbalimbali za kijamii, ikiwamo utoaji wa huduma katika sekta ya afya nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles