25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Zahera, Ndayiragije kumaliza ubishi

MOHAMED KASSARA, DAR ES SALAAM

KIKOSI cha Yanga leo kitashuka dimbani kusaka pointi tatu dhidi ya KMC, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga inaongoza katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 64, baada ya kucheza michezo 26, ikishinda 20, sare nne na kupoteza miwili.

Wanajagwani hao, watashuka dimbani wakitoka kuichapa Alliance FC bao 1-0, katika mchezo wa mwisho wa ligi hiyo uliochezwa Uwanja wa Kirumba, Mwanza.

KMC wanayokutana nayo, inashika nafasi ya nne, ikiwa na pointi 41, baada ya kucheza michezo 28, ikishinda tisa, sare 14 na kupoteza mitano.

Timu hiyo inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni katika Jiji la Dar es Salaam, itashuka dimbani ikitoka kulazimishwa suluhu na Biashara United, mchezo wao wa mwisho uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Yanga itaingia uwanjani kuikabili KMC, ikiwa na kumbukumbuku nzuri ya kupata ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza dhidi ya KMC uliochezwa Oktoba 25, mwaka jana, kwenye uwanja huo.

Hata hivyo, mchezo huo hautakuwa rahisi kwa wababe hao wa Jangwani, kwani kocha wa KMC, Etienne Ndayiragije, hajawahi kupoteza michezo yote miwili dhidi ya timu kongwe za Simba na Yanga, wakati huo akiinoa Mbao FC.

Ndayiragije aliweka rekodi hiyo kwa misimu miwili mfululizo.

Kuelekea mchezo huo, kikosi cha Yanga kitakuwa kimekamilika kutokana na viungo; Thabani Kamusoko, Raphael Daud na Juma Mahadhi, kurejea baada ya kupona majeraha.


Akizungumza na MTANZANIA jana, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, alisema mipango yake ni kushinda mchezo huo ili kujipatia pointi tatu zitakazowafanya wazidi kuwakimbia washindani wao wa karibu, Azam na Simba.

“Tunatakiwa kufanya kazi kubwa ili tupate pointi tatu, KMC ni moja ya timu tishio kwenye ligi, itatubidi kufanya kazi ya ziada kushinda, tuliwafunga katika mchezo wa kwanza, hivyo najua watakuwa wamekuja kwa nia ya kulipa kisasi, hivyo mchezo utakuwa mgumu.

Tunatakiwa kutumia kila aina ya silaha tuliyonayo kupata pointi tatu, tuliteleza kidogo na kufanya vibaya katika michezo iliyopita, hatutaki kurudia tena makosa hayo na kutoa mwaya kwa wapinzani wetu kupunguza wigo wa pointi, ndiyo maana tumeweka nguvu zote kuhakikisha tunashinda,” alisema Zahera.

Kwa upande wake, Ndayiragije, alisema kikosi chake kimejipanga vema kwa ajili ya kuhakikisha kinaichapa Yanga  ili kurudisha pointi zao tatu walizopoteza katika mchezo uliopita.

“Tumepanga kuja kivingine kabisa katika mchezo huo, tutabadili staili yetu kidogo, nimefanya hivyo kutokana na namna nilivyowafuatilia Yanga wanavyocheza, nimekuja na mikakati kabambe kwa ajili ya kuhakikisha tunashinda mchezo huo ili kulipa kisasi cha kupoteza mchezo wa kwanza.

“Tulipoteza mchezo wa kwanza kutokana na makosa madogo tuliyofanya, jambo la kwanza la kufanya ni kusahihisha mapungufu katika michezo yetu iliyopita, tutachukua tahadhari kwa ajili ya kuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo huo, nimewaambia washambuliaji wangu wawe makini kutumia nafasi zitakazopatikana kwa kuwa mchezo huo utaamuliwa na matumizi ya nafasi,” alisema kocha huyo raia wa Burundi.

Mbali na mchezo huo, patashika nyingine ya ligi hiyo itakuwa kati ya Mwadui FC itakayokuwa nyumbani kuumana na Mbeya City katika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles