30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga yashindwa kuikamata Azam

01(3)NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
TIMU ya Yanga jana ilishindwa kuwakamata vinara wa Ligi Kuu ya Vodacom, Azam FC walio kileleni kwenye msimamo baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Ndanda ya Mtwara, mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Sare hiyo imeifanya Yanga kufikisha jumla ya pointi 19 ikizidiwa pointi mbili na vinara Azam, Mtibwa Sugar ni ya tatu ikiwa na pointi 18 sawa na Polisi Morogoro na JKT Ruvu zilizo nafasi ya nne na tano, Simba yenyewe ipo nafasi ya saba kwa pointi 16.

Mchezo huo ulikuwa mkali kwa dakika zote 90, lakini timu zote zilikosa nafasi nyingi za wazi hasa washambuliaji wa Yanga, Kpah Sherman na Danny Mrwanda, waliokosa nafasi nyingi za kuipatia ushindi timu yao.

Mfano katika dakika ya nane winga wa Yanga, Simon Msuva, alikosa bao la wazi akiwa na kipa wa Ndanda, Wilbert Mweta, baada ya shuti alilopiga kudakwa na kipa huyo, Msuva alipata nafasi hiyo kufuatia pasi safi aliyopewa na Mrisho Ngassa.

Yanga ilizidi kupoteza nafasi za wazi baada ya Ngassa kukosa nafasi nyingine dakika ya 12 baada ya shuti alilopiga kumlenga kipa huyo na kulidaka vema kufuatia pasi safi ya beki wa kulia, Juma Abdul.

Ndanda nayo ilikuja juu dakika ya 15 baada ya Masoud Ally kuwapiga chenga wachezaji wa Yanga, lakini shuti alilopiga lilidakwa vema na kipa wa wanajangwani hao, Ally Mustapha.

Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, naye alishindwa kuipatia Yanga bao la uongozi baada ya kupata nafasi nzuri dakika ya 28 akiwa ndani ya eneo la 18 lakini alipiga shuti kali lililopaa juu ya lango la Ndanda.

Cannavaro alipata nafasi hiyo kufuatia kona aliyopiga Msuva kuokolewa vibaya na mabeki wa Ndanda. Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza kinamalizika timu hizo zilitoka suluhu.

Kipindi cha pili kilianza tena kwa kasi na almanusura Yanga iandike bao dakika ya 52, lakini mshambuliaji wake kutoka Liberia, Kpah Sherman, alishindwa kumalizia vema krosi ya Msuva baada ya kupiga kichwa kilichotoka nje ya lango wakati akitazamana na kipa wa Ndanda.

Dakika ya 57 mwamuzi wa mchezo huo, Martin Saanya kutoka Dar es Salaam alimwonyesha kadi ya njano Sherman baada ya kujiangusha ndani ya eneo la 18 ili aipatie penalti timu yao. Dakika tatu baadaye Sherman alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Amissi Tambwe.

Ndanda nayo ilimtoa Masoud Ally dakika ya 62 na kuingia Rajab Isihaka, pia ikamtoa nahodha wake, Paul Ngalema na kuingia Shukuru Chachala.

Dakika ya 72, Tambwe aligongana kichwa na mchezaji wa Ndanda, Zabron Raymond, wakati wakiwania mpira, ambapo Tambwe alichanika kichwani na kufungwa bendeji, huku Raymond akishindwa kuendelea kabisa na mchezo huo na nafasi yake ikachukuliwa na Hemed Khoja.

Kocha wa Yanga aliiongezea nguvu sehemu yake ya kiungo baada ya kumtoa, Hassan Dilunga na kumwingiza kiungo mkabaji, Said Juma, ambaye dakika chache baadaye alionyeshwa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi Stamil Mbonde.

Kama kuna mchezaji wa Yanga ambaye hatausahau mchezo huo basi ni mshambuliaji, Danny Mrwanda, aliyekosa bao la wazi dakika ya 78 baada ya kupaisha juu shuti alilopiga huku langoni kukiwa hamna kipa, Mrwanda alipata nafasi hiyo kufuatia pasi safi ya Msuva.

Ndanda walipata pigo dakika ya 90 baada ya beki wake, Ernest Mwalupani, kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi ikiwa ni ya pili ya njano kutokana na kuchelewesha kupiga mpira mbele alioachiwa aupige na kipa wake.

Licha ya Ndanda kucheza pungufu kwa takribani dakika tano zilizoongezwa na mwamuzi wa akiba, Yanga ilishindwa kutumia pengo hilo na mpira kumalizika kwa suluhu.

Kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani wenyeji Ruvu Shooting walifanikiwa kushinda mabao 2-1 dhidi ya Stand United ya Shinyanga, mabao ya Ruvu yalifungwa na Juma Mpakala (dk 4) na Yahya Tumbo (dk 89), huku bao la Stand likifungwa na Hamis Thabit.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles