24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga yarudi kileleni kwa kishindo

Pg 32NA JENNIFER ULLEMBO, DAR ES SALAAM

TIMU ya Yanga jana ilifanikiwa kuishusha Simba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kutoa dozi nene ya bao 5-0 kwa African Sports katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Simba imedumu kileleni hapo kwa saa 48, kabla ya kushushwa jana na mahasimu wao waliofikisha pointi 50 na kubaki katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 48, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 47.

Mabao ya Yanga jana yalifungwa na beki Kelvin Yondani (33), Donald Ngoma (37), Amissi Tambwe (51, 72) na Matheo Anthony (59).

Yanga ilianza mchezo huo kwa kasi na kufanya shambulizi kwenye lango la wapinzani wao na dakika ya 5 mchezaji Donald Ngoma alikosa bao la wazi akishindwa kumalizia vema pasi ndefu safi ya Juma Abdul, aliyepiga kichwa na mpira kutoka.

Baada ya kukosa bao hilo Yanga walizidisha kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya 33 lililofungwa na beki wa kati Yondani, baada ya kupiga mpira mita 20 na kujaa wavuni.

Yanga baada ya bao hilo iliendelea kulisakama lango la Wanakimanumanu na dakika nne baadaye, Ngoma aliandika bao la pili baada ya kupiga ‘low tiktak’ akimalizia pasi safi ya Juma Abdul kutoka wingi ya kulia na mpira kujaa wavuni.

Watoto wa Jangwani walitoka mapumziko kifua mbele wakiwa wanaongoza kwa bao 2-0 dhidi ya Wanakimanumanu ambao walishindwa kufurukuta.

Kipindi cha pili kilianza timu zote zikifanya mashambulizi, lakini hali ilibadilika dakika ya 51 kufuatia mabeki wa African Sports kufanya uzembe ambao ulimruhusu Amissi Tambwe kupita na kuuwahi mpira uliotemwa na kipa hivyo kuandika bao la tatu kiulaini.

Baada ya bao hilo mchezaji wa African Sports, Pera Mavuo, alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 52 na mwamuzi Abdallah Kabuzi, baada ya kwenda kumlalamikia mshika kibendera kuhusu bao la Tambwe, huku dakika ya 56, Juma Shemvuni, alipewa kadi ya njano kwa kumchezea rafu Ngoma.

Kocha wa Yanga, Hans Van Pluijm, alifanya mabadiliko dakika ya 58 kwa kumtoa Ngoma na nafasi yake kuchukuliwa na Matheo Antony.

Mabadiliko hayo yalizaa matunda dakika moja baadaye kwa Matheo kuifungia Yanga bao la nne, akiitendea haki pasi ndefu yaThaban Kamusoko.

Kamusoko ambaye ni kiungo hatari, alitoa krosi ndefu dakika ya 72 kwa Tambwe, ambaye naye hakufanya ajizi na kuandika bao la tano akifunga kwa kichwa.

African Sports walifanya mabadiliko dakika ya 73 ili kuongeza nguvu, ambapo walimtoa Omari Issa na nafasi yake kuchukuliwa na Mohamed Mtindi lakini hayakuzaa matunda.

Kamusoko dakika ya 77 alikosa bao la wazi akiwa kwenye nafasi nzuri alipiga mpira usio na malengo ukapaa juu, pasi ndefu ilitoka kwa Tambwe. Dakika ya 78 Yanga walifanya mabadiliko kwa kumtoa Vincent Bossou na kumwingiza Paul Nonga.

Baada ya ushindi huo mnono, Yanga inatarajiwa kuondoka kesho kuelekea Kigali, Rwanda kwa ajili ya mchezo wake wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya APR.

Yanga: Ally Mustafa, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Kelvin Yondani, Vincent Bossou, Pato Ngonyani, Deus Kaseke, Thaban Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Haruna Niyonzima.

African Sports: Kabali Faraji, Mwaita Ngereza, Hamza Kassim, Juma Shemvuni, Rahim Juma Ally Ally, Hussein Issa, Pera Mavuo, Rajab Isihaka, James Mendi na Omari Issa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles