30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga yanoga Mwanza

Ni baada ya Yondani na wenzake waliokuwa Stars kutua kambini

DAMIAN MASYENENE- MWANZA

BEKI kisiki wa Yanga, Kelvin Yondani ameamsha ari katika kambi ya timu hiyo jijini Mwanza, baada ya kuungana na wachezaji wengine wa kikosi hicho kinachojiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco United .

Yondani alikuwa sehemu ya kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, kilichoumana na Burundi na kuibwaga kwa , katika michezo  miwili ya kusaka tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Qatar mwaka 2022.

Stars ilitinga hatua ya makundi, baada ya kuitwanga Burundi mikwaju ya penalti 3-0, ikianza kulazimisha sare ya bao 1-1 ugenini jijini Bujumbura kabla ya kupata matokeo kama hayo Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kushinda kwa penalti.

Yanga itashuka dimbani Jumamosi hii kuumana na Zesco ya Zambia, katika mchezo wa raundi ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa Uwanja wa Taifa.

Mbali na Yondani,wachezaji wengine wa Yanga waliokuwamo Stars  ni kipa Metacha Mnata na viungo Abdulaziz Makame na Mohamed Banka (Mo Banka).

Wachezaji hao waliungana na kikosi cha Yanga jijini Mwanza juzi.

Ikiwa Mwanza kwa kambi ya wiki moja, Yanga imecheza michezo miwili ya kirafiki, ikianza kutoka sare ya bao 1-1 na Pamba, kabla ya jana kuikabili Toto Africans, yote  ikichezwa Uwanja wa Kirumba jijini hapa.

Timu hiyo itaondoka Mwanza leo usiku kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya maandalizi ya mwisho kabla ya kushuka dimbani Jumamosi kuikabili Zesco inayonolewa na kocha wa zamani wa Wanajagwani hao, George Lwandamina.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mratibu wa kikosi hicho, Hafidh Saleh alisema kambi yao ina morali ya juu kuelekea mchezo wao na Zesco.

“Ni kweli tayari wachezaji wetu waliokuwa timu ya taifa wameungana na wenzao, kuja kwao kumekamilisha kikosi chetu kuelekea mechi yetu dhidi ya Zesco, hata hivyo wachezaji hawa hawatakuwa shemu ya mechi ya kirafiki dhidi ya Toto Africans kwa kuwa wanatakiwa kupumzika,”alisema .

Salehe alisema kikosi chao kitaimarika zaidi katika mchezo huo, kutokana na  kuipata huduma ya kipa Farouk Shikalo ambaye tayari amepata leseni (ITC) ya kuitumikia timu hiyo kwenye michuano ya kimataifa kutoka Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf).

Shikalo aliikosa michezo miwili ya hatua ya awali dhidi ya Township Rollers ya Botswana kutokana na kuchelewa kwa ITC  yake, lakini sasa huko huru kuitumikia Yanga kwenye michuano ya kimataifa ukiwemo mchezo wa Jumamosi dhidi ya Zesco.

Katika hatua nyingine, mashabiki timu hiyo wametakiwa kuondoa shaka na kikosi chao kwani upo uhakika wa kupata ushindi katika mchezo huo wa kwanza nyumbani.

 Kauli hiyo inakuja baada ya kikosi cha Yanga  kulazimishwa sare ya 1-1 Uwanja wa Taifa na Township Rollers, katika mchezo wa kwanza kabla ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini na kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa bao 1-0.

Timu hiyo pia ilipoteza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu mbele ya Ruvu Shooting, baada ya kuchapwa bao 1-0, na kisha kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Pamba Uwanja wa CCM Kirumba.

Tumaini hilo lilitolewa jijini hapa na Mjumbe wa Kamati Utendaji ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti Kamati ya Mashindano Yanga, Saady Khimji wakati akizungumza na wanahabari, baada ya mazoezi ya timu hiyo juzi Uwanja wa Nyamagana.

 “Sisi Viongozi tumejipanga kuhakikisha tunaiwakilisha vema Tanzania, ikumbukwe kuwa ni timu pekee inayoshiriki Ligi ya Mabingwa, hatutaki kuwaangusha Watanzania, tunataka kuionyesha Afrika kuwa Yanga ni timu ya namna gani kwahiyo ushindi ni lazima,” alisema.

Khimji ambaye pia ni mkuu wa msafara wa timu hiyo ziarani Mwanza, alisema viongozi wa timu hiyo wanafanya kazi wa ukaribu zaidi na benchi la ufundi.

Alisema benchi lao la ufundi limemhakikishia kuwa wataibuka na ushindi wa kuanzia mabao mawili katika mchezo wao huo.

“Viongozi tunafanya kazi kwa ukaribu sana na benchi la ufundi na ndiyo maana kila ilipo timu na  mimi nipo, na kocha Mwinyi Zahera amenihakikishia kwamba mchezo huo tunashinda si chini ya mabao mawili na kuendelea.

“Lakini pia mimi naona mwenendo mzima wa timu mazoezini na nidhamu kambini nina uhakika tutafanya vema.

“Benchi letu la ufundi yapo mambo ambayo wanayafanyia kazi kwa sasa ikiwemo tatizo sugu la ukame wa mabao, mazoezi ya leo yalikuwa kulenga goli, kupenyeza mipira ili kufunga, nimeshuhudia na nimejiridhisha timu yetu iko vizuri na lazima ishinde,” alisema Khimji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles