Yanga yakoleza utamu mbio za ubingwa

0
950

NA THERESIA GASPER

-DAR ES SALAAM

TIMU ya Yanga imefanikiwa kuvuna pointi tatu baada ya kuichapa KMC mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Yanga ilitoka nyuma na kusawazisha baada ya KMC kutangulia kuandika bao la kuongoza dakika ya 16 kupitia kwa Mohamed Rashid.

Mabao ya Yanga yalifungwa na Papy Tshishimbi dakika ya 37 na Ally Ally aliyejifunga dakika ya 67.

Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 67 na kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, baada ya kucheza michezo 27, ikishinda 21, sare nne na kupoteza miwili. 

Mchezo huo ulianza kwa kasi huku Yanga ikimiliki mpira na kutengeneza mashambulizi yaliyoliweka lango la KMC katika wakati mgumu takribani dakika 10 za mwanzo.

Dakika ya 13, mlinda mlango wa KMC, Jonathan Nahimana, alipangua mkwaju mkali wa Feisal Salum na kuzaa kona ambayo haikuzaa matunda.

Dakika ya 16, Mohamed Rashid aliindikia bao la uongozi KMC, akitumia vema makosa ya Thabani Kamusoko aliyeshindwa kuondosha mpira wa hatari na kumwacha mfungaji akimchambua kipa Klaus Kindoki.

Dakika ya 23, Kamusoko nusura aisawazishie Yanga kupitia mpira wa adhabu baada ya shuti lake kugonga nguzo.

Dakika ya 37, Tshishimbi aliisawazishia Yanga baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya Gadiel Michael.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika kwa timu hizo kufungana bao 1-1.

Kwa ujumla kipindi cha kwanza timu hizo zilishambuliana kwa zamu.


Kipindi cha pili, Kocha wa KMC, Etienne Ndayiragije, alifanya mabadiliko katika eneo la mlinda mlango, alimtoa  Jonathan Nahimana na kumwingiza Juma Kaseja.

Dakika ya 46, Ally Ramadhani aliipenya ngome ya Yanga na kuachia mkwaju mkali uliogonga mwamba kabla ya mpira na kutoka nje.

Dakika ya 52, Hassan Kabunda wa KMC alilimwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu Mrisho Ngassa.

Dakika ya 59, Ndayiragije alifanya mabadiliko mengine alimtoa Charles Ilamfia na kumwingiza James Msuva.

Dakika ya 61, Mohamed Rashid alipoteza nafasi ya wazi ya kuiandikia KMC bao la pili, kwani akiwa anatazamana na Kindoki, mabeki wa Yanga walitokea na kuondosha mpira kwenye hatari.

Dakika ya 62, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, alifanya mabadiliko aliwatoa Kamusoko na Deus Kaseke na kuwaingiza
Ibrahim Ajib na Amisi Tambwe.

Dakika ya 67, Yanga iliandika bao la pili, baada ya beki Ally Ally kuutumbukiza mpira wavuni akiwa katika harakati za kuokoa mpira wa krosi uliopigwa na Ajib.

Dakika ya 72, Ramadhani wa KMC alilimwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu Paulo Godfrey.

Dakika ya 81, KMC ilifanya mabadiliko alitoka George Sangija na kumwingiza Abdul Hilary, wakati huo huo Zahera alimtoa Ngassa na kumwingiza Said Juma.

Dakika ya 87, Abdallah Shaibu wa Yanga alilimwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu Emanuel Mveyekure.

Pamoja na mabadiliko hayo, dakika 90 za pambano hilo zilikamilika kwa Yanga kuchomoza na ushindi wa mabao 2-1.

Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo, Mwadui FC ikiwa uwanja wa nyumbani wa Mwadui Complex, mkoani Shinyanga, iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mbeya City.

Yanga: Klaus Kindoki, Paulo Godfrey, Gadiel Michael, Kelvin Yondani, Abdallah Shaibu, Feisal Salum, Mrisho Ngasa, Papy Tshishimbi, Herieter Makamb, Thaban Kamusoko, Deus Kaseke.

KMC: Jonathan Nahimana, Aaron Lulambo, Ally Ramadhan, Ally Ally, Kalos Kirenge, Ally Msengi, George Sangija, Emanuel Mveyekure, Charles Ilamfia, Hassan Kabunda na Mohamed Rashid.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here