31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga wazibwa mdomo, Simba wajiachia

dsc_5658

WINFRIDA NGONYANI NA ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM.

JOTO la mchezo wa watani wa jadi ‘Kariakoo Derby’, limeendelea kupanda ambapo uongozi wa klabu ya soka ya Yanga umechimba mkwara mzito na kutangaza adhabu kali kwa wachezaji wa timu hiyo watakaozungumzia kambi yao kuhusu mchezo wa kesho dhidi ya Simba ambao utachezwa Uwanja wa Taifa Dar es salaam.
Wakati Yanga wakipigwa mkwara huo, wachezaji wa Simba walijiachia kwa kila mmoja kuzungumzia mchezo huo unaovuta hisia za watu wengi barani Afrika.
Wachezaji hao wametamba kuwa wapo kamili kuwakabili watani wao Yanga, wakidai kuwa wana uhakika wataibuka na ushindi kutokana na maandalizi waliyoyafanya.

Akizungumza na MTANZANIA jana, mshambuliaji hatari wa Simba, Laudit Mavugo, alisema amejiandaa vema kuhakikisha anaifunga Yanga na kuwataka mashabiki wakae mkao wa kupokea pointi hizo muhimu kwao.
“Ni kama tulivyofanya kwa Majimaji na sasa Yanga….tuko na morali sana na hatuwaangusha mashabiki wetu kabisa, tunajua kama mchezo ni mgumu sana lakini tutashinda, nikipata nafasi ya kucheza sitamwangusha kocha wangu nitafuata yale yote aliyonielekeza,” alitamba Mavugo.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Mavugo kushiriki kwenye pambano la watani wa jadi hao wenye historia nchini tangu atue Simba msimu huu akitokea Vital’O ya Burundi, na katika mchezo huo atakutana na Mrundi mwenzake, Amissi Tambwe, wote wakiwa wamefunga mabao matatu katika ligi.
Kwa upande wake Shiza Kichuya alisema, mchezo huo una presha ya hali ya juu, kwa hiyo hana uhakika kama atabahatika kutikisa nyavu.
“Siwezi kujiaminisha kuwa nitafunga kwa sababu mchezo utakuwa na presha kubwa ya mashabiki, sioni kama kuna sababu ya kujiamini asilimia 100 za kufunga, inabidi tuombe Mungu atusaidie,” alisema Kichuya.
Nahodha Jonas Mkude alisema msimu huu yanga hatoki, si kwa mechi ya Jumamosi tu bali hata kwenye mzunguko wa pili.

“Tumekamilika kila idara, kikosi kimejaa wachezaji wazuri na makini, kocha mzuri anayeijua vilivyo ligi na pia anafahamu wachezaji wote wa Yanga uwezo wao, hivyo atapanga kikosi kulingana na wachezaji na kiwango cha wapinzani wao,” alisema Mkude.

Meneja wa Simba, Musa Hassan ‘Mgosi’, aliliambia MTANZANIA kuwa kila mchezaji amepewa maelekezo ya nini cha kufanya siku hiyo kutoka kwa kocha Joseph Omog, kinachosubiriwa ni mchezo tu.

Kwa wachezaji wa Yanga, imeelezwa yeyote atakayethubutu kuongea atakatwa nusu ya mshahara na kufungiwa michezo mitatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Chanzo cha uhakika ndani ya kambi hiyo, kimeeleza lengo la tahadhari hiyo ni kupunguza presha iliyopo ndani na nje ya klabu hiyo.
“Kwa sasa tuna utawala mpya, hivyo umesisitiza utatoa adhabu kali kwa mchezaji yeyote atakayezungumza na watu nje ya kambi yetu kuhusu mchezo wa kesho dhidi ya Simba,” kilisema chanzo hicho na kuongeza kuwa hakuna mchezaji yeyote aliyepokonywa simu kutokana na onyo hilo.
Simba tayari imerejea jijini Dar es Salam jana kutoka mafichoni mkoani Morogoro, ilipopiga kambi kwa ajili ya kuwavutia na mchezo huo, wakati Yanga nao wamerejea na kujifungia katika hoteli ya Ledger Plaza (Bahari Beach).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles