27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga sasa yakwama

Wachezaji wa Yanga, Thaban Kamusoko (kushoto), Matheo Anthony, Donald Ngoma na Mbuyu Twite, wakiwania mpira wakati walipokuwa wakifanya mazoezi katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam jana. Picha na Jumanne Juma.
Wachezaji wa Yanga, Thaban Kamusoko (kushoto), Matheo Anthony, Donald Ngoma na Mbuyu Twite, wakiwania mpira wakati walipokuwa wakifanya mazoezi katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam jana. Picha na Jumanne Juma.

*Yafeli kupata video za Mo Bejaia

*Mwambusi atamba watakufa hivyo hivyo

NA THERESIA GASPER, DAR ES SALAAM

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, Yanga, wamekwama kupata video za wapinzani wao, Mo Bejaia ya Algeria ili kuweza kuwasoma kabla ya mchezo wao wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, unaotarajia kuchezwa nchini humo Juni 17.

Yanga imetinga hatua hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Esparanca ya nchini Angola, ambapo mchezo wa awali uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam walishinda mabao 2-0 kabla ya kufungwa bao 1-0  ugenini hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1.

Kutokana na kukwama huko, Yanga ambao pia ni mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliomalizika, wamejipanga kuingia katika mchezo huo kwa tahadhari kwa kuwa hawajui wanakwenda kukutana na mpinzani wa aina gani.

Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kumaliza mazoezi kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi, alisema wamefanya jitahada za kusaka video za timu hiyo lakini hawakufanikiwa, hivyo lazima waingie wakiwa na tahadhari kubwa kuhakikisha wanapata ushindi.

“Tunakwenda kucheza ugenini hivyo lazima tuongeze nguvu ya ziada ya kuwakabili wapinzani, tumeanza mazoezi kwa kasi ukizingatia tunaenda kucheza na timu ambayo hatufahamu mfumo wao, lakini tutahakikisha tunashinda hivyo hivyo.

“Ni lazima tuwe makini, hata hivyo wachezaji wote wanaonekana kuwa imara licha ya kutoka kwenye mapumziko, hili litatupa urahisi katika kuongeza nguvu ya kujiandaa,” alisema Mwambusi.

Kocha huyo alisema wameanza mazoezi mapema na wachezaji waliowasajili msimu huu kwa sababu wanataka kuwapima na kutengeneza kombinesheni nzuri katika kikosi chao.

“Tuna mpango wa kuwatumia kwenye mashindano, naamini wachezaji hawa wapya watafanya vema kwenye michezo inayotukabili licha ya kutokuwa na uzoefu na mechi za kimataifa kutokana na uwezo wao mzuri uwanjani,” alisema.

Wakati huo huo, idadi kubwa ya wachezaji Yanga tayari wameripoti katika mazoezi ya timu hiyo isipokuwa Simon Msuva anayedaiwa kuumwa malaria, Benno Kakolanya aliyesajiliwa hivi majuzi, Salum Telela na Paul Nonga ambao wanadaiwa huenda wakatemwa kwenye kikosi cha mabingwa hao.

Yanga inatarajia kujichimbia jijini hapa kujiandaa na mchezo huu licha ya kuzoeleka kwenda kuweka kambi nje ya Dar es Salaam, awali ilidaiwa wataweka kambi nchini Uturuki lakini wamebadilisha maamuzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles