30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga mzuka kila kona

MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

KIKOSI cha Yanga kinatarajia kushuka dimbani leo, kukabiliana na Kariobang Sharks ya Kenya katika mchezo wa kirafiki wa kuhitimisha  tamasha la klabu hiyo lililopewa jina la Wiki ya Wananchi, utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Tamasha hilo ni maalum,  kwa ajili kuwatambulisha wachezaji watakaoitumikia timu hiyo msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano mengine ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wiki ya Wanachi ilianza Julai 27,ambapo mashabiki, wapenzi na wanachama wa klabu ya Yanga wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kuwatembelea wagonjwa hospitali.

Shughuli nyingine iliyofanywa na klabu hiyo ni kuzindua jezi za mpya zitakazotumika msimu ujao.

Kabla ya kurejea Dar es Salaam juzi, kikosi cha Yanga kilipiga kambi mkoani Morogoro, kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya.

Ikiwa huko, Yanga ilifanikiwa kucheza michezo mitano ya kujipima ubavu na kushinda yote.

Ilicheza mchezo wa kwanza na kuichapa Tanzanite mabao 10-1, ikaichapa mabao 2-0 timu ya Moro Kids, ikaikangaa timu ya ATN mabao 7-0, ikailiza Mawenzi Market  bao 1-0, kabla ya kufunga  hesabu kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Friends Rangers.

Kilichonogesha zaidi kambi hiyo ni kitendo cha timu hiyo kufunga mabao mengi, huku wachezaji wapya wakifunga mabao karibu kila mchezo, hatua iliyotoa matumaini mapya kwa mashabiki wa timu hiyo kuelekea msimu ujao.

Miongoni mwa wachezaji wapya waliowika katika michezo hiyo ni Sadney Urikboh, Patrick Sibomana , Juma Balinya na Lamine Moro.

Wengine wanaosubiriwa kwa shauku na  mashabiki wa klabu hiyo ni Issa Bigirimana (Rwanda) Mustapha Suleiman (Burundi) na Maybin Kalengo (Zambia) .

Kwa upande wa wazawa ni  Ally Mtoni ‘Sonso’ (Lipuli FC),Abdulaziz Makame (Mafunzo), Ally Ally (KMC), Mapinduzi Balama (Alliance) Metacha Mnata (Mbao FC) na Muharami Issa( Malindi).

Hata hivyo, mchezaji  anayesubiriwa kukata kiu ya Wanajangwani hao ni mshambuliaji mpya, David Molinga, ambaye anatajwa kama mbadala wa Herietier Makambo aliyejiunga na klabu ya Horoya AC inayoshiriki Ligi  Kuu nchini Guinea.

Molinga alisajiliwa na Yanga dakika za mwisho kabla ya dirisha la usajili kufungwa, hivyo hakupata nafasi ya kuungana na wengine kambini Morogoro.

Mshambuliaji huyo tayari ameanza kuwapa  jeuri mashabiki wa timu hiyo kutokana na rekodi zake za kutisha katika ufungaji mabao katika Ligi Kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),msimu uliopita,akifunga mabao 14, katika mechi 16 alizoshuka dimbani kwenye mashindano mbalimbali.

Baada ya mchezo huo, Yanga itakuwa na kibarua kizito mbele Township Rollers ya Botswana, katika mchezo wa kwanza wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, utakaochezwa kati ya Agosti 8 na 11, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,  huku mchezo wa marudiano ukitarajiwa kupigwa kati ya Agosti 23 na 25, jijini Gaborone.

Kama Yanga itafanikiwa kupenya raundi ya kwanza,  itakutana na mshindi kati ya Green Mamba ya Eswatini na Zesco ya Zambia, katika michezo miwili ya mchujo  ambapo mbabe wa jumla atatinga hatua ya makundi.

Wana jagwani hao wanarejea katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuikosa kwa miaka miwili.

Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Mwinyi Zahera amesema hakuna sababu ya kushindwa kufanya vizuri msimu ujao kutokana na kikosi chake kuimarika zaidi kuliko msimu uliopita.

 “Kuhusu aina ya wachezaji wangu nimewaona kwa ukaribu kuanzia kwenye mechi yao iliyopita na hata mazoezini wote wapo vizuri.

”Wana uwezo wa kumiliki mpira na kutoa pasi kwa wakati hivyo msimu ujao tutakuwa juu zaidi ya msimu uliopita,”alisema Zahera.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles