26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga kumaliza unyonge kwa Singida United leo?

Mohamed kassara – Dar es salaam

KIKOSI cha Yanga leo kitashuka dimbani kusaka pointi tatu dhidi ya Singida United, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kwenye  Uwanja wa Namfua, Singida.

Yanga itaikabili Singida, ikiwa na hasira za kupoteza mechi mbili mfululizo zilizopita, ikianza kubamizwa mabao mabao 3-0 na Kagera Sugar 3-0, kabla ya kuchapwa bao 1-0 na Azam FC 1-0, michezo yote ikichezwa  Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu hiyo itaingia uwanjani kusaka ushindi kwa sababu mbili, kwanza kumaliza hasira za kupoteza michezo hiyo miwili iliyopita, lakini kupunguza pengo la pointi kati yao na watani zao, Simba walio kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

Yanga inashika nafasi ya saba ikiwa na pointi 25, baada ya kucheza michezo 14, ikishinda saba, sare nne na kupoteza tatu,  ikiwa nyuma kwa pointi 16 dhidi ya Simba iliyocheza michezo 16 hadi sasa.

Singida kwa upande mwingine, inashika nafasi ya 19 ikiwa na pointi 10, baada ya kucheza michezo 16, ikishinda miwili, sare nne na kupoteza 10.

Itaikabili Yanga, ikiwa na morali ya hali juu inayotokana na kutoka kuvuna ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting, katika mchezo wao uliopita uliochezwa kwenye uwanja huo.

Mchezo huo ni mtihani mwingine kwa kocha wa kikosi cha Yanga, Luc Eymael ambaye tangu achukue mikoba ya kuliongoza jahazi hilo, hajafanikiwa kuvuna ushindi katika michezo miwili iliyopita.

Kikosi cha Yanga chini ya Eymael hakijafanikiwa kufunga bao, huku pia kikiruhusu wavu wao kutikiswa mara nne, wastani wa kufungwa mabao mawili kila mchezo.

Rekodi zinaonyesha kuwa, tangu Singida ipande Ligi Kuu Bara msimu wa 2017/18, haijawahi kufungwa na Yanga nyumbani katika michezo miwili.

Msimu wa 2017/18, mchezo wa kwanza uliozikutanisha timu hizo Uwanja wa Namfua, ulimalizika kwa suluhu, matokeo kama hayo yalitokea tena msimu uliopita.

Rekodi za jumla zinaonyesha kuwa, hadi sasa  timu hizo zimekutana mara nne katika misimu miwili iliyopita, Yanga ikishinda mchezo mmoja, huku mitatu ikimalizika kwa sare.

Ushindi pekee iliyowahi kuupata Yanga mbele ya Singida ulikuwa wa mabao 2-0, katika mchezo wa mzunguko wa kwanza msimu uliopita uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ugumu wa mchezo huo utachagizwa na uwepo wa nyota wa zamani wa Yanga, Athuman Idd ‘Chuji’ na Haruna Moshi ‘Bobab’, ambao wamejiunga na Singida
dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15, mwaka huu.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga , Hassan Bumbuli, alisema baada ya matokeo yasiyoridhisha huko nyuma wamejidhatiti kwa mapambano lengo likiwa kupata pointi tatu.

Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Singida United, Cales Katemana alisema wanatambua Yanga ni timu bora na ina wachezaji wenye uzoefu, lakini hilo haliwapi mashaka ya kushindwa kuvuna pointi tatu katika mchezo huo.

Mbali na mchezo huo, kivumbi kingine cha ligi hiyo kitatimka katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mwadui itakuwa nyumbani kuikabili Azam FC.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles