23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

YANGA HAKUNA KINACHOSHINDIKANA

MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, Yanga leo itakuwa na kibarua kigumu ugenini cha kukabiliana na Pyramids ya Misri, katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika,  utakaochezwa Uwanja wa June 30 jijini Cairo.

Mchezo wa kwanza kati ya timu hizo ulichezwa Oktoba 27, Uwanja wa CCM Kirumba, ambako Pyramids iliiliza Yanga mabao 2-1.

Ili kusonga mbele hatua ya makundi, Yanga itahitaji ushindi wa kuanzia mabao 2-0 dhidi ya Pyramids.

Hata hivyo, kazi haiwezi kuwa rahisi kwani Pyramids wanayokutanayo ina rekodi ya kufanya vizuri inacheza nyumbani.

 Michezo miwili iliyopita imefanikiwa kushinda mmoja na kutoka sare mmoja.

Ujanja inaoweza kuutumia Yanga ni kuhakikisha inapachika mabao ya kutosha ili kuwang’oa wapinzani wao hao.

Rekodi zinaonyesha Pyramids,  imeruhusu bao kwenye kila mchezo iliocheza nyumbani, ikianza na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Etoile Du Congo ya Congo Braville hatua ya awali, kabla ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na CR Belouizdad ya Algeria,  raundi ya kwanza.

Safu ya ushambuliaji ya Yanga ina rekodi ya kufunga bao moja kila mchezo iliocheza ugenini kwenye michuano ya kimataifa msimu huu.

Timu hiyo ilianza kushinda bao 1-0 ugenini lililoisukuma nje Township Rollers ya Botswana, hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kabla ya kufunga bao jingine ilipochapwa mabao 2-1 na Zesco United ya Zambia.

Huo ulikuwa mchezo wa  raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa ambapo Wanajangwani hao walifurushwa.

Rekodi zinaonyesha, Yanga imeshakanyaga nchini Misri na kucheza michezo nane dhidi timu tatu  za Al Alhly, Zamalek na Ismalia na kupoteza saba na kuambulia sare moja.

Yanga itashuka dimbani kuivaa Pyramisd bila ya beki wake mzoefu, Kelvini Yondani anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata mchezo wa kwanza.

Hata hivyo, pengo lake litazibwa na Lamine Moro anayerejea kikosini, baada ya kumaliza adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata wakati wa mchezo dhidi ya Zesco uliochezwa Ndola.

Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema amekiandaa kikamilifu kikosi chake ili kuhakikisha kinapata ushindi utakaowavusha hatua nyingine.

Alisema anafahamu watu wa Yanga wana hofu kuwa watapoteza mchezo huo, lakini amewataka wawe na imani na timu yao.

“Mimi nina imani ya  kushinda na kusonga mbele,  kama kwenye michezo mingine tumefanikiwa, kwanini tushindwe huu.

“Hakuna mchezo rahisi, yote ni migumu ila matokeo ndiyo yanayoamua nani mshindi,” alisema.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Fredrick Mwakalebela, alisema morali ya kikosi chao iko juu.

“Maandalizi yanaendelea vizuri na wachezaji wote wana morali ya juu ya kutaka ushindi, wapenzi wa Yanga wasiwe na wasi wasi, watuombee,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles