31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga haikamatiki

3BNA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
TIMU ya soka ya Yanga jana iliendeleza ubabe wake katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kuzidi kuusogelea ubingwa baada ya kuichakaza Ruvu Shooting kwa mabao 5-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo, Yanga imefikisha pointi 52 na sasa inahitaji kushinda mechi moja tu kati ya tatu zilizobakia ili kutangazwa mabingwa wapya.
Mchezo ambao Yanga ikishinda itatwaa ubingwa wa ligi msimu huu ni ule utakaochezwa Jumatatu dhidi ya Polisi Morogoro katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo wa jana, Yanga walikosa bao dakika ya sita baada ya Simon Msuva kufanya shambulizi kali akiunganisha kwa kichwa pasi safi ya Oscar Joshua lakini hesabu zake hazikutimia baada ya mpira kutoka nje.
Msuva aliendeleza kasi yake na kufanikiwa kuipatia timu yake bao la kuongoza dakika ya 14 kwa kichwa, akiunganisha vema pasi ya mpira wa adhabu uliopigwa na kiungo Haruna Niyonzima.
Makosa yaliyofanywa na kipa Abdallah Rashid wa Ruvu Shooting dakika ya 24 yaliiwezesha Yanga kupata bao la pili kupitia kwa Mliberia, Kpah Sherman aliyeunganisha mpira wa kona iliyochongwa na Msuva na kuwaacha mabeki wakishangaa.
Dakika 26, mwamuzi, Isihaka Shirikisho wa Tanga alimuonya kwa kadi ya njano George Osei wa Ruvu baada ya kumpiga kiwiko winga machachari wa Yanga, Mrisho Ngassa, huku mpira ukiwa tayari umetoka nje.
Dakika 38, Msuva alikosa bao baada ya shuti la mpira wa adhabu aliopiga akiwa nje ya eneo la hatari kugonga mwamba na kutoka nje kabla ya dakika 43 kufanya tena shambulizi kali lililopaa juu ya lango akiunganisha pasi ya Niyonzima.
Yanga waliendelea kufanya mashambulizi langoni mwa Ruvu ambapo dakika 45, Msuva aliandika bao la tatu kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Niyonzima na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa Ruvu kuwapumzisha Baraka Mtuvi na Abdulrahman Mussa na kuwaingiza Juma Mapakala na Mwita John, huku Yanga wakiwatoa Kpah Sherman, Oscar Joshua na Said Juma na nafasi zao kuchukuliwa na Hussein Javu na Edward Charles na Mbrazil, Andrey Coutinho.
Mshambuliaji Amissi Tambwe aliandika bao la nne kwa Yanga baada ya kuambaa na mpira na kuwapiga chenga mabeki wa Ruvu na kipa kabla ya kuachia shuti lililojaa moja kwa moja wavuni.
Beki wa Yanga, Juma Abdul na Yahaya Tumbo, walionywa na kadi za njano baada ya kuzozana uwanjani wakiwa wanagombea mpira wa adhabu uliokuwa ukielekezwa langoni kwa Ruvu.
Dakika 67, Sherman aliifungia timu yake bao la tano baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Ruvu ambao walifanya shambulizi dakika ya 74 kupitia kwa Mwita John aliyepiga shuti lililopaa juu ya lango akiunganisha pasi ya Ally Khan.
Dakika za mwisho Ruvu walipambana kusaka bao la kufutia machozi na kujaribu kulisakama lango la Yanga lakini juhudi zao hazikufanikiwa kuzaa matunda.
Countinho ambaye aliingia dakika ya 85 kuchukua nafasi ya Said, alionywa kwa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi Michael Aidan wa Ruvu.
Kutokana na mabao mawili aliyofunga katika mchezo wa jana, Msuva amefikisha idadi ya mabao 16 na kuwaacha kwa mbali Tambwe mwenye mabao 11, Emmanuel Okwi wa Simba, Didier Kavumbagu wa Azam na Rashid Mandawa wa Kagera Sugar waliofunga mabao 10 kila mmoja ambao pia wanawania ufungaji bora msimu huu.
Yanga: Ally Mustapha ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua/Edward Charles, Rajab Zahir, Kelvin Yondani, Said Juma/Andrey Coutinho, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Mrisho Ngassa na Kpah Sherman/Hussein Javu.
Ruvu Shooting: Abdallah Rashid, Michael Aidan, Abdul Mpambika, George Osei, Hamis Selemani, Salvatory Ntebe, Raphael Kyala, Ally Khan, Yahya Tumbo, Baraka Mtuwi/Juma Mapakala na Abdulrahman Musa/Mwita John.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles