23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

YANAYOJIRI CHADEMA NDIYO HALI HALISI?


Na. M. M. Mwanakijiji

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema kiko kwenye matatizo. Matatizo yanayotishia uhai wake na uwepo wake kama chama cha siasa nchini. Kuna uwezekano mkubwa kwamba hadi hivi sasa siyo viongozi wala wanachama wa chama hicho ambao wametumia muda wa kutosha kuweza kuangalia ni tatizo gani linawakabili.

Tatizo hili ukiwasikiliza wana Chadema na hasa viongozi wao linahusishwa moja kwa moja na utendaji, sera na mwelekeo wa Rais John Magufuli kisiasa nchini. Rais Magufuli analaumiwa si tu kwa kudumaza upinzani bali pia kwa kile kinachotafsiriwa kama nia yake ya kuua kabisa upinzani.

Kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa kwa vyama vya upinzani, kusitishwa kwa haki ya kuipinga serikali kwa njia ya maandamano, na kuzuiwa kwa wanasiasa kufanya siasa nje za majimbo yao kunatajwa kama ishara na ushahidi wa wazi wa nia hiyo ya Rais Magufuli.

Zaidi pia tuhuma za wanasiasa wa upinzani hasa kwenye maeneo ambayo upinzani umejijenga kununuliwa na hatimaye kuachia nafasi zao za kuchaguliwa kunatajwa kama mkakati wa wazi wa Chama cha Mapinduzi-CCM, ambacho Magufuli ni Mwenyekiti wake kuiua Chadema.

Miezi kadhaa sasa viongozi mbalimbali wa Chadema hasa madiwani wamekuwa wakiachia nafasi zao ambazo walizigombea miaka miwili tu nyuma na kukimbilia CCM wakidai kuwa wanaunga mkono Serikali ya Rais Magufuli.

Pamoja na hayo matukio mbalimbali ambayo yametokea yakihusisha viongozi wa upinzani na wanachama wake yanatajwa kama ushahidi mwingine usiopingika wa Serikali kudhamiria kuumaliza upinzani kuelekea mwaka 2020. Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na kukamatwa kwa viongozi wa upinzani, kufunguliwa mashtaka na wengine kukaa jela kwa muda huku wakikabiliwa na kesi mbalimbali.

Matukio mengine ambayo yametishia upinzani na ambayo wapinzani hasa Chadema wanayatumia kuonyesha lengo, nia na dhamira ya Serikali ya Rais Magufuli kuumaliza upinzani ni pamoja na mauaji ya nyota iliyokuwa imeanza kung’ara ya kiongozi wa chama hicho kanda ya magharibi aliyekuwa anaibuka kwa umaarufu Alphonce Mawazo. Tukio la mauaji ya Mawazo lilihusishwa na siasa ambalo upinzani umeendelea kudai kuwa uchunguzi wa kina haujafanyika.

Hata hivyo, tukio kubwa zaidi ambalo limewafanya wapinzani waone kuwa wamelengwa na vyombo vya dola ni jaribio la mauaji dhidi ya Mbunge Singida Mashariki na Mnadhimu Mkuu wa upinzani bungeni Tundu Lissu ambaye alishambuliwa na wale walioitwa “watu wasiojulikana” ndani ya makazi ya wabunge mjini Dodoma mchana wa jua kali. Kama tukio lile lingefanywa na wahalifu wa kawaida ni wazi polisi ingefanya kila jitihada kuhakikisha wahusika wanakamatwa, wanadai wapinzani.

Haya yote yanatajwa kama mipango ya serikali kuuvuna upinzani kabisa nchini huku wengine wakiona ni njama haramu za kuirudisha nchi kwenye utawala wa chama kimoja. Viongozi mbalimbali wa kisiasa hasa kutoka upinzani wameshaanza kuzungumza dhidi ya kile wanachokiona kama mpango wa kufuta upinzani ili ubakie jina tu ila usiokuwa na nguvu ya kuitikisa CCM.

Na hapa ndio hoja ya hamahama inayoendelea upinzani kwenda CCM inatolewa maelezo. Tayari kumedaiwa kutolewa hata ushahidi wa watendaji wa Serikali wakifanya majaribio ya kile kinachodaiwa kununua viongozi wa upinzani. Hili lilitokea huko Arusha ambapo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Alexander Mnyeti ilidaiwa alirekodiwa kwa siri akitoa dau kwa kiongozi wa Chadema. Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari na yule wa Arusha Mjini Godbless Lema waliwasilisha ‘ushahidi’ huo kwa viongozi wa Takukuru lakini baada ya siku chache Takukuru walitangaza kupuuzia ushahidi huo kwa kile walichokidai kuwa viongozi wa upinzani walileta siasa. Serikali haikuzungumzia tuhuma za matendo yaliyokuwemo kwenye mkanda huo.

Kutokana na hilo na tuhuma nyingi za hivi karibuni maelezo pekee ambayo yamekuwa yakitolewa na viongozi wa Chadema ni kuwa viongozi hao “wananunuliwa”. Maelezo haya kwa namna fulani yanaweza kuwa na ukweli kwani ikumbukwe siyo mageni sana kwenye siasa zetu na kuna dalili za huko nyuma ambapo viongozi wa upinzani walishawishiwa kuingia chama tawala wengi wakiahidiwa nafasi mbalimbali.

Swali kubwa ambalo linapaswa kuulizwa; je kununuliwa kwa madiwani na wabunge peke yake kunatosha kuelezea kinachoendelea Chadema? Je, kuna uwezekano kuna jambo jingine ambalo linaendelea ndani ya chama hicho ambalo viongozi wake ama kwa hofu ya kufungua sanduku la pandora wanaogopa kuona kilichomo kwani hawataweza tena kulifunga? Je, inawezekana kuna vitu vingine ambavyo wanachama wa kawaida hawajaambiwa na kinasumbua ndani ya Chadema?

Tukio la aliyekuwa mgombea wa Chadema kwenye Urais na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kwenda kukutana na Rais hivi juzi kimewaumiza wanachama wengi na baadhi ya viongozi walikutwa hawakujiandaa na taarifa hizo. Baadhi ya wanachama na hata viongozi wameanza mara moja kutaka Lowassa aondolewe au aondoke huku wengi wakionekana sasa hivi hawamtaki tena. Kwa baadhi yetu hii inashangaza kwani miaka miwili tu nyuma viongozi na wanachama wale wale ambao walikubali kubadili gia angani walizungusha mikono na kuimba “mabadiliko-Lowassa, Lowassa – Mabadiliko”. Kwa Lowassa kwenda kukutana na Magufuli amekuwa tena si nuru, kimbilio, tumaini na nyota ya mabadiliko?

Tayari tumemsikia Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye akianza kumtaja hadharani Tundu Lissu aliyeko kwenye matibabu Ubelgiji kama mtu ambaye anapaswa kubeba bendera ya Urais mwaka 2020. Hii itakuwa kinyume kwani tayari Chadema walishaanza kumtaja Lowassa kama mgombea wao tena? Je, watambadilishia gia Lowassa na kumchukua Lissu ambaye anaonekana kama anaweza kweli kupambana na umaarufu wa Rais Magufuli? Na swali jingine ambalo wapo wanaoweza kuliuliza ni je; Lissu atakuwa na tofauti ya kiutawala kumlinganisha na Rais Magufuli? Watatofautiana nini hasa? wengine wanaweza kuhoji.

Licha ya hilo, Lissu pia anatajwa kama mtu sahihi wa kurithi mikoba ya Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe ambaye ndani ya uongozi wake Chadema inajikuta mara nyingi kwenye mgogoro mkubwa wa kisiasa. Swali linaloweza kuwagawa tena Chadema ni je, wale wanaomuunga mkono Mbowe watakuwa tayari kuhamisha utii wao kwenda kwa Lissu? Je, inawezekana tena ukatokea mgogoro kama ule uliotokea wakati aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe alipotaka kugombea nafasi ya uenyekiti ndani ya chama na kukutana ugumu ambao uliacha doa kubwa ambalo hatimaye lilimlazimisha kujiondoa na chama hicho na kwenda kuanzisha ACT-Wazalendo.

Zitto sasa ni mbunge wa Kigoma Mjini na yeye kama ilivyo Chadema anakabiliwa na kukimbiwa na viongozi wa chama chake ambao wamechukuliwa na Serikali ya Magufuli akiwemo aliyekuwa mgombea wake wa Urais Anna Mghwira, ambaye amepewa Ukuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. Alifuatiwa na mmoja wa waanzilishi wa ACT ambaye walitoka na Zitto Chadema Dk. Kitila Mkumbo ambaye aliitwa na serikali na kupewa nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Kijana mwingine wa chama hicho na Mwanasheria anayepanda kila kukicha Albert Msando. Mara baada ya kujiunga na CCM Msando aliingizwa kwenye kamati ya Mwenyekiti Magufuli ambayo ameiunda ndani ya chama kwenda kufuatilia mali za CCM nchi nzima.

Ni wazi kuwa pamoja na zile zinazoonekana juhudi na mkakati wa dhati wa Serikali kudhoofisha upinzani – kitu ambacho si kigeni mahali popote duniani kwa vyama tawala kufanya na Magufuli si wa kwanza nchini.  Inawezekana kuna mambo mengine ambayo hayajafunguliwa vizuri na ambayo yanachangia viongozi wa upinzani walioonekana ni wapinzani kweli kujiondoa kwenye vyama vya upinzani. Ni mambo gani haya? Je, viongozi wa upinzani wanaweza kukaa chini na kuangalia wao wenyewe wanaongozaje, na wanafanya nini ndani ya vyama vyao kufanya wazidi kuaminiwa na wanachama na viongozi wenzao?

Je, upinzani ambao haujawa na uthubutu wa wazi wa kujitokeza kuendesha upinzani wa kweli bado unasubiria huruma na hisani ya serikali kufanya upinzani bado utaweza kuhimili mitikisiko ya miaka mitatu ijayo? Je, viongozi wa Chadema watakaobakia wataweza kweli kusimama na kufanya upinzani? Je, hawana mbinu nyingine au wamekubali masharti ya wao kufanya siasa nje ya yale yaliyowekwa na sheria na Katiba?

Wapo watu wanaoohoji kama viongozi wakiwamo kina Nelson Mandela, Martin Luther King (ambaye siku yake ya kuzaliwa inaadhimiwa Januari 15), kina Mahatma Ghandi na wengine wangekubali kuacha siasa kabisa na kujikunyata pembeni wangeweza kweli kuleta mabadiliko kwenye nchi zao? Je, viongozi wote walioambiwa wasiandamane wangekubali kutokuandamana je, Serikali za nchi zao zingeangushwa kama ilivyotokea Zimbabwe, Tunisia na Misri?

Au yawezekana viongozi wetu wa upinzani walichimba shimo ambalo sasa wao wenyewe hawawezi kutoka; shimo la kuvunja uaminifu na sasa wanapata shida ya kuaminiwa tena?

Au kuna jingine?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles