23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Yaliyomkuta askari aliyezima moto matanki ya mafuta

Na FARAJA MASINDE -DAR ES SALAAM

IKIWA ni siku nane tangu usiku wa Januari 8, mwaka huu, moto ulipozuka katika hifadhi ya mafuta inayomilikiwa na Kampuni ya Lake Oil eneo la Vijibweni, Wilaya ya Kigamboni, Dar es Salaam, imebainika kuwa askari aliyejitoa mhanga kuzima moto huo, alipitia machungu mbalimbali.

Machungu hayo ni pamoja na kukosa matibabu katika hospitali mbili alizoenda usiku huo baada ya kuzima moto, huku joto kali lililokuwapo eneo hilo na harufu kali ya petroli vilikuwa vimeonekana kumdhuru.

Akizungumza na gazeti hili, askari huyo Station Sagent, Willison Mwageni, ambaye alipata cheo hicho baada ya ujasiri wake wa kuzima moto huo, alisema mikasa ilianza wakati wa kutoka nyumbani kuwahi eneo la tukio.

Mwageni alisema baada ya kupata taarifa za moto huo akiwa nyumbani kwake Pugu, alichukua pikipiki ili kufika eneo la tukio kwa haraka.

Alisema akiwa njiani, alisimamishwa na askari wa usalama barabarani – trafiki, ambaye licha ya kumwelewesha uharaka aliokuwa nao, bado hakumwelewa jambo lililofanya amwache dereva wa bodaboda na yeye kutembea kwa miguu.

Mkasa huo haukuwa wa mwisho, kwani baada ya kuzima moto kwenye mazingira magumu yaliyohatarisha maisha yake, alitafuta matibabu usiku huo hospitali mbili tofauti huku kote akikwama kuhudumiwa.  

Alisema kabla ya kuingia eneo la matanki na kuzima moto huo, alijua hatari iliyokuwa mbele yake na uwezekano mdogo wa kutoka huko akiwa salama, hivyo aliaga kabisa na kutaka mke wake ambaye ni mjamzito kutunzwa.

Mwageni alisema alifanya hivyo kwa sababu alibaini kuwa moto huo usipodhibitiwa mapema na ukafika eneo la matanki na mitungi ya gesi, madhara yake yangeweza kufika hata mikoa ya jirani – nje ya Dar es Salaam.

 “Nilichokifanya nikaaga, nikasema jamani mimi nakwenda, kama nikifa basi naomba mnipelekee salamu kwa familia yangu, na mke wangu mjamzito mwambieni nimekufa kwa ajili ya kuokoa taifa, kwani inatakiwa muda mwingine kuwa mzalendo kwa ajili ya wengine kuweza kupona bila kujali utapata nini.

“Nilichofanya nikachukua fire extinguisher, nikafungua pini kisha nikapiga sehemu ile kwa ajili ya kukata moto sababu isingekuwa hivyo zile gari na watu wote wasingetoka. Baada ya moto kupungua nikalazimika kuingia ndani kabisa ya moto kwa kupanda ngazi.

“Kule juu kulikuwa na joto kali, hewa hakuna zaidi ya kusambaa kwa petroli, ilitakiwa kuwa na ujasiri wa hali ya juu kuweza kuingia.

“Katika wale wenzangu sita ambao tuliteuliwa awali wakakataa, wawili walikuja wakati huo mimi natafuta koki, wakaniambia aisee koki iko huku.

“Wakati naingia, wahusika waliniambia kuwa tanki namba saba ndiyo ilikuwa inafanyiwa kazi muda mfupi uliopita, nikamwambia mwenzangu aigonge ile koki ili ilegee, lakini alipoona joto linazidi wote wakakimbia.

“Ikabidi niwaambie wawe wananipiga na maji mgongoni ili kusaidia kupunguza joto na kupata hewa. Kweli walifanya hivyo, nilivyoingia kule ndani ikanibidi niwe navuta hewa kwa ndani, nikawa navuta kidogo tu huku nafunga ile koki,” alisema Mwageni.

KUKOSA HUDUMA HOSPITALI

Alisema baada ya kukamilisha kuzima moto huo, ikabidi Katibu Tawala (DAS) Wilaya ya Kigamboni, Rahel Mhando, aagize apelekwe kupata matibabu jambo ambalo alikubaliana nalo.

Mwageni alisema kuwa alipelekwa Hospitali ya Tungi kwa kutumia gari la wagonjwa.

Alisema baada ya kufika hapo, hakupata huduma na daktari alimwambia asubiri kwanza kwa sababu ana wagonjwa wengi wa dharura.

Askari huyo alisema hakuridhika na maneno hayo na kuamua kurudi eneo la tukio ambako alimkutana Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri, ambaye alipobaini hajatibiwa akaagiza apelekwe Hospitali ya Mnazi Mmoja.

“Kufika pale bado nikaambiwa kuwa natakiwa kuwa na bima ya afya au nitibiwe, kesho yake niende kulipa.

“Nikaona bado wananivuruga, nikatembea hadi kituo chetu cha Fire nikiwa sina shati wala viatu, nilipofika pale kuna mfanyakazi mwenzetu nikamwomba anipatie nguo, akanipa na viatu japo vilikuwa vya kike, nikavaa na kuondoka kwenda nyumbani,” alisema Mwageni.

Mwandishi wa MTANZANIA alimtafuta Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni Vijibweni, Dk. Saumu Kumbisaga, ambaye alisema taarifa kuhusu tukio zima lililoendelea hospitalini hapo anazo, lakini hawezi kuzitoa hadi apate idhini kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa.

“Ni kweli kwamba taarifa za tukio zima tunazo kwani kanda ya video (CCTV) ilinakili kila kitu kilichoendelea, lakini ninyi waandishi wa habari si mnajua utaratubu ulivyo, kwamba lazima mpate kibali kutoka kwa Mkurugenzi,” alisema Dk. Saumu.

Aidha, mwandishi pia alifika katika Hospitali ya Manazi Mmoja kutaka kupata ufafanuzi wa jambo hilo, lakini ilishindikana kutokana na Mganga Mkuu kuwa na shughuli za kiofisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles