28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wizara yaeleza sababu kondomu kuadimika

Na VERONICA ROMWALD

 – DAR ES SALAAM

BAADA ya kuwapo kwa malalamiko ya upungufu wa kondomu katika baadhi ya maeneo nchini, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, amesema wana taarifa juu ya suala hilo na kwamba hatua za haraka zimeanza kuchukuliwa.

“Changamoto imetokea, baada ya kubadilisha mfumo uliokuwapo kwa wale wasambazaji wa taasisi binafsi, jukumu hilo limerudi ndani ya wizara, hivyo kuanzia sasa ndiyo itakuwa inasimamia manunuzi, usambazaji wa mipira ya kiume.

“Utaratibu uliokuwapo (awali) kulikuwa na baadhi ya taasisi ambazo zilikuwa zinapewa fedha na kununua mipira kisha kuisambaza kwa bei nafuu, ndiyo maana zilikuwa zinapewa majina mbalimbali kupitia hizo taasisi.

“Utaratibu wetu Serikali tutakuwa tunanunua mipira hiyo na kuigawa kwenye vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya na kwenye jamii

“Hivyo tumelibaini hilo tatizo katika kipindi hiki cha mpito, kwa kushirikiana na wenzetu tutahakikisha tuna kondomu za kutosha ndani ya wiki moja, kuanzia sasa zitakuwa zimeanza kupatikana,” alisema.

Alisema si kweli kwamba zimepanda bei na Serikali itaendelea na utaratibu kuhakikisha zinapatikana za kutosha na kuzisambaza ili watu waendelee kujikinga.

“Taarifa hii kwetu ni nzuri, inaonesha matumizi yapo na mahitaji yapo, tumebaini na tunashughulikia hili,” alisema Dk. Ndugulile.

Baadhi ya maeneo yanayodaiwa kuwa na upungufu huo ni mji wa Njombe.

Njombe ndiyo mkoa wenye kiwango cha juu cha maambukizi ya VVU kwa asilimia 11.4 ukifuatiwa na Iringa wenye asilimia 11.3 kulingana na takwimu za Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids).

MGANGA MKUU

Mganga Mkuu wa Makambako, Ernest Kiyungu, alithibitisha kuwapo kwa changamoto hiyo ndani ya mkoa huo.

“Zilikuwa zinasambazwa na wizara na wadau mbalimbali, wale (wadau) walikuwa wanaleta lakini bei yao ilikuwa nafuu, boksi moja lilikuwa linauzwa Sh 5,000. Walikuwa wanazileta na kuzisambaza kwa wasambazaji wakubwa, ule ulikuwa ni mradi wa PSI.

“Walikuwa wanatoa kiwandani wanaleta kwa hao wasambazaji wao wakubwa na wasambazaji wakubwa wanapeleka kwa wale wasambazaji wadogo ambao nao wanasambaza kwa wateja, ndiyo unakuta wanapeleka kwenye gesti, mahoteli na sehemu nyinginezo,” alisema Kiyungu.

TACAIDS WANENA

MTANZANIA lilimtafuta Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk. Leonard Maboko ambaye alisema hawezi kuzungumza jambo lolote kuhusu sakata hilo kwani bado hajapokea taarifa rasmi ofisini kwake.

“Tacaids haihusiki kwenye kununua wala kusambaza kondomu, hili ni jukumu la Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, umeniambia Naibu Waziri (Dk. Faaustine Ndugulile) amelitolea ufafanuzi pia, ikiwa umemsikiliza vizuri, yeye ndiye mtu sahihi kabisa wa kulizungumzia kwa sasa.

“Ninachofahamu mimi ni kwamba fedha zipo kwa ajili ya uagizaji, kama kuna mahala popote ambapo mchakato umekwama sijui, ndiyo maana umeniuliza nikakuambia lazima na mimi niulize kwa sababu mimi ndiye mratibu wa sekta zote ikiwamo hata ninyi watu wa media (vyombo vya habari).

“Kila mmoja namuuliza anafanya nini katika nafasi yake kuhusu masuala ya ukimwi, inapokuja suala la kondomu wahusika ni Wizara ya Afya, kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, ndiyo maana huwa wanaagiza, hawajaniambia kama wamekwama popote.

“Inawezekana Njombe zimeadimika, lakini sina uhakika maana wizara ndiyo inayosambaza kupitia MSD (Bohari Kuu ya Dawa), wakishazinunua wanazipeleka kama dawa kwenye maduka yao ya kanda, sasa kama kuna mahala kuna ‘crisis’ hawajaniambia, lazima niulize, siwezi kusema chochote kile hivi sasa.

 “Tacaids tupo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi upo chini ya wizara ambayo ndiyo ina jukumu la kununua na kusambaza.

“Kimsingi sisi ni waratibu wa kazi zote za Serikali, tunaratibu upande wa Ukimwi tu, tunamuwajibisha kila wizara, tunafuatilia inafanya nini, tukiwaita waandishi nanyi tunawauliza mchango wenu mnafanya nini katika kudhibiti Ukimwi, wizara ina mambo ya kinga na matibabu,” alisema.

MSD

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema kwa upande wao hakuna tatizo lolote.

Alisema kondomu zinazosambazwa na MSD huwa haziuzwi na kwamba huwa zinapelekwa moja kwa moja katika ofisi zao za kanda na pia kuna mfumo maalumu wa kuzipeleka katika vituo vya afya na hospitali ambazo huwa zinautumia kuomba.

“Kondomu zetu zinaitwa Zana, hizi haziuzwi, MSD hatuuzi kondomu, huwa zinagawiwa bila malipo, wateja wetu ni vituo vya afya, hospitali za umma, sisi huwa tunazipeleka moja kwa moja kwenye vituo vya afya na hospitali ambazo huwa zinaomba kwenye mfumo wetu, haziuzwi.

“Kuhusu zile zinazouzwa sisi hatuhusiki nazo, zetu haziuzwi, na kwa upande wetu hakuna tatizo lolote na wiki iliyopita pale Makambako tumepeleka kondomu 50,000 na Mafinga tumepeleka kondomu 15,000,” alibainisha.

SIKIKA

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Sikika, Irenei Kiria, alisema ni muhimu suala hilo kushughulikiwa mapema kwani ni hatari ikiwa watu wataendelea kujamiiana bila mipira kwa sababu wamekosa wakajikuta wameambukizwa.

“Sidhani kama lilipaswa litokee, suala la kuzuia maambukizi ni kipaumbele katika sekta ya afya, ni jambo linalotakiwa kufanyiwa utatuzi kwa haraka sana, hatujui (Sikika) nini kimetokea, nani hakutekeleza jukumu lake sawa sawa, labda tufanye ufuatiliaji kwenye mfumo mzima, kwamba ni mahali gani hapakwenda sawa sawa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles