23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wizara Mambo ya Ndani yagutuka baada ya dhahabu kurejeshwa

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, amesema ni aibu kusikia nyara za Serikali ikiwamo madini zinatoroshwa na kukamatiwa nchi za jirani na kuagiza ulinzi wa kutosha katika viwanja vya ndege nchini.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku moja baada ya Rais Dk. John Magufuli kupokea dhahabu kutoka Kenya, ambayo ilitoroshwa nchini kupitia viwanja vya ndege vya Mwanza na Kilimanjaro na kukamatiwa Nairobi, Kenya.

Akipokea dhahabu hiyo juzi, Rais Magufuli alisifu vyombo vya ulinzi vya Kenya huku akieleza kusikitishwa na vya Tanzania kushindwa kukamata.

Masauni jana mara baada ya kukagua usalama wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, alisema kupokea madini ya dhahabu kutoka Kenya kumemuhuzunisha yeye na Rais Magufuli.

Alisema jambo hilo halitavumiliwa kuendelea, ni lazima jitihada za makusudi zichukuliwe na ndiyo maana ameanza kukagua usalama wa viwanja huku akiwataka Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na Polisi wafanye kazi kwa pamoja.

“Hatua ya jana (juzi) ya Rais imeshtua sana na kuna haja ya kufanya kazi kwa muunganiko mkubwa kati ya Jeshi la Polisi, TRA, TAA ili kuhakikisha kunakuwa na usalama.

“Nimekagua kwa kuanza na huu uwanja mkubwa, nitaendelea katika viwanja vingine ili kuhakikisha naangalia maeneo ya usalama na hakuna mtu kupitisha dawa za kulevya, nyara za Serikali na vitu vingine visivyo halali,” alisema.

 Masauni alisema wataongeza kikosi cha askari wa kutosha na wenye sifa wenye mbwa kukagua mizigo na kubaini vitu ambavyo si halali ikiwemo dawa za kulevya.

Alisema ulinzi unatakiwa kuimarishwa, hasa kwa abiria wanaosafiri kwa kulinda mali zao, abiria wanaoingia nchini, mizigo na kuangalia usalama wa mali mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukamata wale wanaosafirisha dawa za kulevya na nyara za Serikali pia.

Naye Kaimu Meneja wa Jengo jipya la tatu JNIA, Barton Komba, alisema usalama katika jengo hilo umeimarika ikiwemo mifumo ya kiusalama.

Alisema uwanja huo ni mkubwa na mzuri kuliko viwanja vyote Afrika, hivyo hafikirii kama kutakujakuwa na changamoto ya kiusalama.

“Uwanja huu utakuwa unasafirisha abiria milioni sita kwa mwaka na kumefungwa jumla ya kamera za kisasa 293, hivyo kutakuwa na ulinzi wa kutosha,’’ alisema Komba.

Kamanda Polisi wa Viwanja vya Ndege (ACP), Jeremia Shila, alisema hatasita kumchukulia hatua yeyote askari atakayekengeuka na kufanya kazi kinyume na maadili ya kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles