23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

WENZETU WALIKWAMA, SISI TUTAFIKA?

 NA MARKUS MPANGALA                |            


TANGU nchi yetu iingie kwenye orodha ya nchi zinazomiliki ndege za kisasa aina ya Boeing Dream-liner, kuna mambo kadhaa nayatafakari, kubwa ni jinsi ya kuepuka hasara au kufilisika.

Zipo nchi barani Afrika zinamiliki ndege za aina hiyo, mathalani Ethiopia, Rwanda na Kenya, kwa kuzitaja chache.

Uamuzi wa kununua ndege unapaswa kupongezwa, kwani ni hatua ya awali kabisa kusonga mbele, na kuwa chachu ya kuongeza ndege nyingine katikati ya changamoto ya kuzitunza, kuwezesha uendeshaji na faida.

Ikumbukwe kuwa, ilani za vyama vya siasa nchini kuanzia Chama tawala CCM, Umoja wa Katiba ya Wananchi – Ukawa unaoongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema na ACT-Wazalendo katika uchaguzi wa mwaka 2015, vyote vilisisitiza mahitaji ya kufufua upya Shirika la Ndege Nchini -ATCL.

Kwenye ilani ya CCM kifungu cha 41, kinazungumzia kuanzisha mpango wa usafiri wa anga pamoja na ukarabati na ujenzi wa viwanja vya ndege nchini kote.

Aidha, kwenye ilani ya Chadema kifungu cha 37 kuhusu miundombinu, kinasema kuwa “Shirika la Ndege Tanzania lilikuwa shirika lenye ufanisi mkubwa katika usafiri wa anga barani Afrika. Hata hivyo shirika hili kwa sasa linachechemea, likiwa na watumishi wengi na likitegemea Hazina kulipa mishahara”.

Mwaka 2016, ACT -Wazalendo kupitia aliyekuwa Mwenyekiti wake, Anna Mghwira, kilisema shirika la ndege nchini linatakiwa kutoa huduma kwa abiria, mathalani kuhudumia mizigo yote ya ndege, kuhudumia vyakula ndani ya ndege na kumbi (Lounge) zote za daraja la kwanza (first class) na huduma ya ukatishaji wa tiketi (Booking) za ndege (Galileo).

Ili kumudu jukumu hili, ACT-Wazalendo waliiomba serikali kuunda kitengo cha uwezeshaji wa huduma za chini (Air Tanzania Ground Support Company), ambacho kinatakiwa kuwa na maeneo yafuatayo; Cargo Handling (utunzaji wa mizigo), Ramp – Handling, Passengers Handling (utunzaji wa abiria), Computer Reservation Systems (Galileo), Clearing & Forwarding (usafirishaji na upokeaji mizigo), Airport Shuttle Buses (Usafiri wa mabasi wa kwenda na kutoka kwenye viwanja vya ndege), Security (Mfumo wa usalama viwanjani), Travel Agency na kitengo cha uhandisi kwa ajili ya kutengeneza ndege zinazoharibika.

Ni dhahiri wanasiasa na vyama vyote walitambua na kuona umuhimu wa kuhakikisha nchi yetu inakuwa na shirika la ndege imara zaidi pamoja na kuchochea uchumi wetu.

Licha ya vyama hivyo kuwa na ajenda hiyo kama msingi wa kuimarisha uchumi wa nchi, bado shirika la ndege haliwezi kuwa tegemeo peke yake. Kuna mambo mengine pia muhimu ambayo yanatapaswa kufanyika kupitia shirika hilo, kisha kuingiza faida kwingine.

Hivi sasa nchi yetu ina Dreamliner moja tu. Kuna mashirika mengi yanamiliki ndege za ina hiyo, lakini yamekuwa yakitangazwa kupata hasara au kufilisika. Yapo maswali, ikiwamo; Ni kwanini mashirika mengi ya ndege duniani yanafilisika. Je; njia zipi zinatakiwa kutumika ili kuepusha hali hiyo.

Tuangazie baadhi ya mashirika mengine nini kilitokea. Kwa mujibu wa jarida la Flight International, toleo la Aprili 10, 1969 (Ukurasa wa 583), Shirika la Monarch Airlines lilianzishwa mwaka 1967 na wafanyabiashara wawili, Bill Hodgson na Don Peacock.

Taarifa za mwaka 2017 zinaonyesha kuwa, shirika hilo lilikuwa na ndege 34, liliajiri watumishi 3,750, wengi wakiwa raia wa Uingereza na wengine 600 walikuwa idara ya uhandisi wa shirika hilo. Monarch Airlines lilikuwa shirika la tano kwa ukubwa nchini Uingereza kihistoria hadi kufilisika kwake.

Mwaka 2017 lilipofilisika watu wengi walipoteza ajira, licha ya shirika lenyewe kutafuta njia mbadala kunusuru ajira hizo pamoja na kuwarudisha nyumbani abiria waliokuwapo katika nchi za Tunisia na Misri ambao walishalipia tiketi za ndege hiyo kwenda na kurudi.

Kuna sababu kubwa tatu zilizochangia Monarch Airlines kufilisika, ambazo kimsingi zimekuwa zikiyakumba mashirika au kampuni mbalimbali zinazofanya biashara ya ndege.

Mosi, kupanda bei ya mafuta mwaka 2016 kuliipiga kofi la uso Monarch Airlines. Kutokana na mapato kidogo na kupanda gharama za uendeshaji, zilisababisha Monarch Airlines kushindwa kumudu hali hiyo, hivyo likaanguka.

Pili, ushindani miongoni mwa mashirika mengine ya ndege yalichangia kuliporomosha shirika hilo. Kwa mfano, Monarch Airlines ilikumbana na ushindani kutoka kwa kampuni ya EasyJet (Wizz).

Licha ya maboresho mbalimbali pamoja na sapoti waliyopata Monarch Airlines, bado haikufua dafu, ndipo mwaka 2017 likatangazwa kufilisika.

Tatu, Monarch Airlines lilifanya kazi ya zaida, haikutegemea uuzaji wa tiketi za abira 20 au zaidi. Ilibeba mizigo, vifurushi na kadhalika.

AIR waibua hasara ijayo 2030

Taarifa ya utafiti wa mpito iliyotolewa na Airline Insolvency Review Julai mwaka huu, ikiwa ni miezi 9 baada ya kufilisika Monarch Airlines Oktoba 2017, unaonyesha kuwa abiria mmoja kati ya 200 wataathirika miaka 15 ijayo kutokana na kufilisika kwa mashirika na kampuni za ndege duniani.

Mwenyekiti wa Airline Insolvency Review, Peter Bucks, katika utangulizi wa taarifa ya ripoti hiyo, anasema: “Miezi 9 iliyopita sote tulishuhudia mwisho wa shirika kubwa la Uingereza lijulikanalo kwa jina la Monarch Airlines, lilisitisha biashara zake, likaacha makumi kati ya maelfu ya abiria wakiwa ng’ambo. Ili kulinda haki za abiria hao, serikali ya Uingereza ilianzisha mpango wa kuwasaidia kuepuka usumbufu wa kusafiri kwa kipindi cha wiki mbili kwa gharama ya pauni milioni 60 (sawa na Sh bilioni 180). Katika kipindi hicho hicho, Serikali ya Ujerumani ilikuwa inatekeleza mpango kama huo ili kuiokoa Kampuni ya Air Berlin (Niki 2003), iliyokumbwa na matatizo kama ya Monarch Airlines.

Serikali ya Ujerumani ilitoa msaada wa kifedha kuhakikisha uongozi unaendesha kampuni hiyo bila mafanikio. Pande zote, serikali na uongozi wa kampuni, ulifanya kazi kuhakikisha abiria waliopo ng’ambo wanapata usafiri mbadala kwa kutumia kodi za wananchi. Utafiti huu unaibua mjadala juu ya nini kinachofuata inapotakiwa kuwalinda abiria katika kipindi ambacho kampuni husika haina mwelekeo na inaelekea kufungwa, na kwa vipi tunaweza kupunguza matumizi makubwa ya kodi za wananchi kwa kampuni kama hizo.”

Ripoti kamili inatarajiwa kutolewa mwishoni mwa mwaka huu, lakini taarifa ya awali inabainisha kuwa, karibu abiria 900,000 wataathirika pale kampuni na mashirika ya ndege yatakapofilisika. Ripoti hiyo inasema wakati Monarch Airlines lilipofilisika kulikuwa na abiria 110,000 nje ya Uingereza ambao walishalipia tiketi zao kurejea makwao.

Utafiti huo unagusia pia hatua ya Serikali ya Denmark kulipia asilimia 20 ya tiketi kunusuru abiria wa kampuni ya ndege ya Cimber Sterling.

Wawekezaji wa biashara ya ndege kwa sasa hawajafikia kiwango cha kuikomboa sekta hiyo, ambayo gharama zake zinazidi kuongezeka kila kukicha. Kampuni nyingi  zinaachana na biashara ya ndege kwa sababu ya matatizo ya kifedha kwa sababu matokeo chanya hayapatikani haraka wala soko lao halikui kwa kasi wanayotegemea, hali ambayo inatishia uhai wao wa kuendelea na biashara hizo.

Ongezeko la kodi ni miongoni mwa sababu za kampuni na mashirika ya ndege kushindwa kuendelea na biashara zao, husasan yale madogo. AIR wanasema abiria wengi wanalalamikia bei za tiketi kuwa kubwa pamoja na tozo katika maeneo mbalimbali huchangia kudorora kwake.

Kwamba ifikapo mwaka 2030, takribani abiria milioni moja wataathiriwa na hatua za kufilisika biashara ya ndege.

AIR wametahadharisha kwamba, pamoja na serikali kukwamua mashirika na kampuni za ndege, hali ya sekta hiyo itakuwa mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 15 ijayo.

Wanasema mabadiliko ya uongozi kwenye mashirika na kampuni husika hayawezi kuleta ufanisi iwapo sababu zilizochangia kufilisika kwake ni za kisoko zaidi.

“Ushahidi tuliobaini sasa kati ya sababu zinazofilisi, kampuni za ndege kwa kuzingatia mfumo, sheria na taratibu, bado yapo mengine tunaendelea kutafiti. Hata hivyo, kuna sababu ya kuamini kuwa, kanuni za biashara ya ndege katika Bara la Ulaya zinachangia ugumu kwakuwa washindani, hasa pale mengine yanapotegemea ruzuku kushindana. Kuna uwezekano kuwa hata fedha zinazotolewa kwa ajili ya kukwamua shirika au kampuni ya ndege zitakuwa na wakati mgumu kwa asilimia 6 mwaka ujao hadi asilimia 13 kwa miaka 15 ijayo.”

Wanaongeza: “Serikali inaweza kuhisi kuwajibika kwa madhumuni ya kuwatetea wananchi na kulinda sera zake, licha ya kampuni au shirika la ndege kushindwa kuwa na maadili ya kuwalinda wateja wake. Uamuzi huo huibua misuguano ya kisiasa, hali ambayo inaweza kuepukwa. Iwapo serikali inakwamua kampuni ya mashirika ya ndege bila kuziadhibu, inatakiwa kuangalia maeneo haya; kuna athari gani ambayo abiria na walipa kodi wanaipata kwa ndege kushindwa kufanya kazi? Kwanini njia zinazohitajika kuwarejesha abiria nyumbani hazipo kwenye soko la ndege?

Nchi yetu ipo katika dunia hii. Kufilisika kwa mashirika na kampuni mbalimbali barani Ulaya ni somo ambalo tunapaswa kujifunza kwalo.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mtaalamu wa biashara ndani na nje, Gabriel Mwang’onda, anasema: “Mashirika na kampuni za ndege hapa duniani zilizopo na zilizokufa ziliingia kwenye mtego wa kudhani kuwa biashara ya ndege ni kuuza tiketi za abiria tu. Shirika letu la ATCL likiwa na mtizamo huu, basi litakuwa linajichimbia kaburi lake lenyewe, halitadumu kabisa,

“Kwa ATCL kuendesha biashara ya ndege, inatakiwa wazingatie yafuatayo; kwanza kubadilisha vitengo kama overall catering, lounges, ground handling, engineering, IT, trainings na vingine vingi, kutoka kuwa vituo vya kugharimia hadi kuvifanya vituo vya uwekezaji, yaani kupunguza gharama kubwa za uendeshaji wa hili shirika kwa kuvifanya viwe vinatengeneza faida vyenyewe. Fedha za kukiendesha zitatoka kwake chenyewe, mashirika mengi ya ndege husafiri na tumbo la ndege huwa tupu, mafuta ni yaleyale, mwelekeo ni uleule, kwahiyo huu ni mtazamo finyu kibiashara.”

Akizungumzia hoja za upendeleo katika utafiti wa Airline Insolvency Review, Mwang’onda anasema: “Mashirika ya ndege ya Marekani yamekuwa yakilalamika miaka nenda miaka rudi kuhusu ruzuku na upendeleo wa mashirika ya nchi za Kiarabu, lakini wao hakuna mtu amewakataza kufanya hivyo, lakini sababu zao ni za msingi, kwa maana soko haliwezi kuwa lenye haki wakati wote. Wengine wataanguka, nasi tulione hilo”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles