24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

‘WENYE ‘TATTOO’ RUKSA KUCHANGIA DAMU’

NA VERONICA ROMWALD– DAR ES SALAAM          

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi, amesema damu ya watu waliojichora michoro mwilini (tattoo)ni salama.

Kutokana na hali hiyo, wanaruhusiwa kuchangia damu kwa wenye uhitaji kwani kisayansi hakuna mahala ambako inaeleza kuwa mtu mwenye tattoo hastahili kuchangia damu.

Ufafanuzi huo wa kitabibu wa Profesa Janabi umekuja baada ya mjadala mkali ulioibuka katika mitandao mbalimbali ya kijamii juu ya watu wanaochora tattoo, kwamba damu yao si safi na haifai kuwaongezea wenye uhitaji.

Profesa Janabi alisema watu wanapotoa damu haimaanishi inachukuliwa na kumwekea mtu mwingine hapo hapo, ila inachunguzwa na kuangaliwa magonjwa mengi yakiwamo Ukimwi, malaria, homa ya ini na mengine ambayo yanaambukizwa kupitia damu.

“Tattoo si ugonjwa, lakini wataalamu huwa waangalifu wanapochukua damu kwa kuichunguza kabla ya kumwongezea mgonjwa.

“Tunakuwa waangalifu, inategemea huyo mtu kachanjwa namna gani, kwa sababu magonjwa ya kuambukiza ya damu ikiwa vifaa vilivyotumika kumchora hizo tattoo havikuwa vizuri (safi) na vilitumika kwa watu wengi uwezekano wa kuambukizana magonjwa huwa mkubwa.

“Wote damu zao zitachunguzwa na si ajabu kukuta damu ya mwenye tattoo haina tatizo, lakini ya mtu ambaye hana tattoo ikawa na tatizo, kwa sababu kinachoambukiza pale si tattoo bali wale wadudu ambao wapo ndani ya damu,” alisema.

Pamoja na hilo, mkurugenzi huyo aliwataka Watanzania kujitokeza kuchangia damu kufanikisha matibabu ya watoto waliozaliwa na magonjwa ya moyo ambao wanasubiri kufanyiwa upasuaji.

“Tunakusudia kuwafanyia upasuaji watoto 140 hadi 150 ambao tayari wamelipiwa matibabu yao na kituo cha utangazaji Clouds na Taasisi ya Baps, lakini ili kufanikisha upasuaji huo, tunahitaji kiasi cha chupa kati ya 900 hadi 1,000,” alisema.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Plaxeda Ogweyo, alisema ili kutosheleza mahitaji ya hospitali hiyo huhitajika chupa 100 hadi 120 za damu kila siku.

“Lakini huwa tunapata chupa 60 hadi 70. Hali hii inatupa changamoto kwani huwa tunalazimika kuwasubirisha wagonjwa ambao hawahitaji huduma ya dharura wodini na kuwahudumia wale ambao huhitaji huduma hiyo ya haraka,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alizitaka hospitali zote zilizopo ndani ya wilaya hiyo kuweka utaratibu mzuri wa kuwahamasisha watu kujenga utamaduni endelevu wa kuchangia damu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles