Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA imetangaza bei kikomo ya petroli nchini.
Bei hiyo itaanza kutumika kuanzia leo pamoja na kutambua bei kikomo ya petroli nchi nzima.
Taarifa iliyotolewa na EWURA jana ilieleza kwamba bei ya mafuta ya aina zote yanayoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imepungua ikilinganishwa na toleo lililopita.
“Bei ya jumla na rejareja kwa mafuta ya aina zote (petroli, dizeli na mafuta ya taa) yaliyoingizwa nchini kupitia bandari ya Dar es Salaam imepungua ikilinganishwa na toleo lililopita la Januari 2, 2018.
“Kwa Februari 2019, bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa imepungua kwa Sh 175/lita (asilimia 7.61), Sh 144/lita ( asilimia 6.48) na Sh 156/lita ( asilimia 7.08), mtawalia.
“Vilevile ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimepungua kwa Sh 174.03/lita ( asilimia 8.02), Sh 143.65/lita (asilimia 6.84) na Sh 155.32/lita ( asilimia 7.47), mtawalia.
“Kwa kiasi kikubwa, kupungua kwa bei za mafuta katika soko la ndani kunatokana na kuendelea kushuka kwa bei za mafuta hayo katika soko la dunia.
“Kwa mikoa ya kaskazini, bei ya petroli, dizeli na mafuta ya taa itaendelea kuwa ile ile ya Januari 2019.
“Hii inatokana na ukweli kwamba pamoja na kuwa kuna shehena ya mafuta iliyopokelewa nchini Januari 2019 kupitia bandari ya Tanga, mafuta hayo ni kidogo na hayatoshelezi mahitaji ya mafuta kwa mikoa yote ya kaskazini,” ilieleza taarifa hiyo
Hata hivyo taarifa hiyo ya EWURA ilieleza kwamba ghala ya kuhifadhia mafuta mkoani Tanga bado ina kiwango kikubwa cha mafuta yaliyopokelewa Desemba 2018 ambayo yatatosheleza mahitaji ya mafuta kwa mikoa ya kaskazini.
“Kwa hiyo, bei hizi za kuanzia Februari 6, 2019 zimezingatia gharama za mafuta yaliyoingizwa nchini Desemba 2018 kupitia Bandari ya Tanga,” ilieleza taarifa hiyo