23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wengine wawili wafa kwa corona

AVELINE  KITOMARY – DAR ES SALAAM

IDADI ya watu walikufa kwa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19) nchini  imefikia watatu, baada ya jana watu wengine wawili kutangazwa kupoteza maisha.

Mbali na watu hao waliopoteza maisha, watu wengine saba wametangaza kuthibitika kuambukizwa virusi hivyo na kufanya jumla ya wagonjwa wote kufikia 32.

Kesi za wagonjwa  hao na watu waliopoteza maisha zimebainika ndani ya siku 25 tu tangu kisa cha kwanza kilipotangazwa mchini Machi 16 mwaka huu.

Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, akithibitisha idadi ya vifo na ongezeko la wagonjwa hao jana aliwataja waliofariki kuwa ni  mwanaume mwenye umri wa miaka  51 ambaye  taarifa zake zilitolewa  Aprili 8 mwaka huu  na   mwanaume mwenye miaka  57 aliyetolewa taarifa jana.

Alisema wote wawili ni raia wa Tanzania na Wakazi wa Mkoa wa  Dar es Salaam.

“ Tunasikitika  kutoa taarifa ya vifo viwili  vilivyotolea leo(jana) ni   miongoni mwa wagonjwa waliothibitishwa kuwa  na maambukizi  ya virusi vya  corona nchini, hivyo kufanya idadi ya vifo  kufikia watatu  tangu ugonjwa huu ulivyoripotiwa nchini,”alisema.

Akitangaza ongezeko la wagonjwa waliothibitika kuwa  Covid-19 Ummy alisema jumla yao sasa wamefikia 32 nchini.

Akifafanua alisema wagonjwa watano wamethibitika Tanzania Bara na wawili visiwani Zanzibar.

 “Leo (jana)Waziri wa afya wa Serikali ya Mapinduzi ya  Zanzibar  ametangaza uwepo wa wagonjwa wawili wapya  waliothibitika kuwa na corona (Covid-19) hivyo sasa jumla ya watu waliothibitika kuwa na Covid-19 nchini ni 32 kati ya hawa watano wamepona  na wagonjwa wengine 24  wanaendelea vizuri na matibabu.

Kuhusu wagonjwa watano waliothibitika Tanzania Bara, Ummy alisema; “Ni Watanzania  na wakazi wa Dar es Salaam  wa kwanza ni mwanaume  mwenye umri wa mika 68 wa pili mwanaume mwenye miaka 54 wa tatu ni mwanaume mwenye miaka 57 wa nne ni mwanaume mwenye miaka 41 na wa tano  mwanamke mwenye umri wa miaka 35,”.

Kutokana na ongezeko hilo la maambukizi ya virusi vya  corona, Waziri Ummy  kwa mara nyingine amewasisitiza  wananchi  kuchukua tahadhari ya kujikinga  na ugonjwa  huo kwa njia mbalimbali kupitia elimu inayotolewa na wataalamu wa afya.

WAGONJWA WAPYA ZANZIBAR

Mapema  jana Asubuhi  taarifa iliyotolewa na Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamad Rashid zilithibitisha kuwepo kwa wagonjwa wawili wapya kisiwani humo.

 Hamad alisema  wagonjwa hao wawili wote ni raia wa Tanzania   na hivyo ongezeko hilo kufikisha  jumla ya wagonjwa tisa  kutoka wagonjwa saba visiwani humo.

“Tuna wagonjwa tisa ambao wamelazwa katika kituo cha matibabu cha ugonjwa wa Covid-19  Kidimni  wagonjwa wote wanaendelea vizuri na afya zao zinaendelea kuimarika  siku hadi siku.

“Mgonjwa wa kwanza ni Mtanzania mwenye umri wa miaka 33, mkazi wa Mwanakwetekwe aliripotiwa Aprili saba  akisumbuliwa na homa kali, mafua na kifua  baada ya kuchukuliwa  kipimo  alionekana ameambukizwa  na mgonjwa huyo tayari ameshachukuliwa  na yuko  katika kituo  cha Kidimni  kwa matibabu.

“Mgonjwa wa pili ni Mtanzania Mwenye umri wa miaka 24 ,mkazi wa Mtendeni  aliripotiwa akiwa na mafua na kikohozi  na alichukuliwa sampuli  ambayo inaonesha  kuwa tayari ameambukizwa sasa anaendelea na matibabu,”alibainisha Hamad.

Aidha alisema wagonjwa hao wote hawana historia ya kusafiri  nje ya nchi kwa siku za hivi karibuni.

Alisema Wizara inaendelea kuwafuatilia watu wa karibu  waliowahi kukutana na wagonjwa  hao ili kudhibiti kuenea kwa  maambukizi mapya.

“Hadi kufikia jana (juzi)  mchana  jumla ya watu 86 walikutana na wagonjwa  kwa karibu ,vilevile  kuna watu 252 waliorudi kutoka nje ya nchi  wamewekwa karantini Unguja na Pemba  huku watu 202  wameruhusiwa kutoka karantini baada ya kukaa kwa siku 14  na kutokuonesha dalili yoyote ya maradhi hayo,”alisema.

Hamad aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari  na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya  kuhusu jinsi ya kujikinga na maambukizi  ya Covid-19.

“Hasa kwa kunawa mikono  mara kwa mara na maji titirika  na sabuni  na kuepuka mikusanyiko hasa masokoni , vituo vya daladala  na sehemu nyingine .

“Kinga ni bora kuliko tiba  ni vyema tukachukua tahadhari  sasa kuliko tusubiri hadi maradhi haya yatuathiri  kwa kiwango kikubwa ,tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu  azidi kutulinda na kutuepusha  na maradhi haya,”alimalizia.

HALI    ILIVYO SASA

Hadi sasa jumla ya wagonjwa 32 walithibitishwa kuwa na ugonjwa huo wanatoka katika mikoa ya Dar es Salaam,Mwanza,Arusha,Kagera na Zazibar.

Idadi ya wagonjwa 19 wanatoka katika Mkoa wa Dar es Salaam ,wagonjwa tisa wanatoka Zanzibar ,wagonjwa wawili Arusha ,mgonjwa mmoja  Mwanza na Kagera mgonjwa mmoja.

Jumla ya wagonjwa watano wamethibitishwa kupona huku  watu 280 waliokuwa karibu na wagojwa hao  wanafatiliwa na watu 461 tayari wameshafatiliwa   na wasafiri waliopo karantini ni 120.

Wakati taarifa za hapa nchini zikionyesha hayo, idadi ya vifo duniani inakaribia 100,000  huku kesi za watu walioambukizwa ikifika milioni 1.6 na zaidi ya 361,000  wakiripotiwa kupona virusi hivyo.

Jiji la New York nchini Marekani ndilo linaloongoza sasa duniani kwa kuwa na kesi nyingi za virusi vya corona zinazofikia  87,725 na vifo 5,280.

Aidha wakati pia ugonjwa huo  ukionekana tishio  duniani kutokana na kasi ya maambukizi na vifo , Daktari wa  nchini Uingereza, Amir Khan amechambua juu ya ugonjwa huo akisema watu wenye dalili za kawaida kama kifua kikavu na homa wanaweza kupona pasipo kupata madhara katika miili yao.

Hata hivyo alisema wanasayansi sasa wanaamini kwamba ushahidi umeongezeka hasa kwa watu ambao wamekumbwa na shida kubwa ya kupumua na nimonia kwamba wanaweza kubaki na madhara makubwa na ya muda mrefu kwenye mapafu na hata figo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles