30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wenger kiongozi asiyetaka kukosolewa

ARSEN

ADAM MKWEPU NA MITANDAO,

MASHABIKI wa timu ya Arsenal wamebaki midomo wazi wasijue cha kufanya baada ya kocha wa timu hiyo, Arsene Wenger, kumtimua kocha wa timu ya vijana, Thierry Henry, kwa sababu tu ameponda uwezo wa mshambuliaji wa Arsenal, Olivier Giroud.

Tukio hilo lilitokea katika michuano ya mwaka huu ya Euro 2016, ambapo Wenger alikuwa mchambuzi kwa wiki tatu katika televisheni ya beIN Sport ambayo mara kadhaa humwita kufanya uchambuzi hasa michezo ya kimataifa wakati Ufaransa inapocheza.

Lakini jukumu la Wenger si kutoa vikwazo kupitia maoni yake katika michezo hiyo bali ilikuwa kutoa mwanga juu ya mchezo husika, maamuzi  na uhakiki wa michezo ijao.

Wenger ni mtu ambaye mara nyingi alikuwa akilalamika kuhusu vyombo vya habari vinavyotumia kutoa maoni lukuki katika kuiponda Arsenal, lakini hakusita kutoa maoni yake juu ya wengine huku akipata ushirikiano wa kutosha katika studio kwa kucheka wakati akitoa uchambuzi wake huo.

Kutokana na alichokishuhudia Wenger kupitia kitendo cha kuwa mchambuzi ndio sababu ya kutomruhusu Thierry Henry kuwa kocha wa timu ya vijana ya Arsenal chini ya miaka 18 wakati ambapo alikuwa akijitolea kama sehemu ya leseni ya Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA) huku akiwa mchambuzi wa televisheni ya Sky.

Wenger anasema kwamba, Henry kuendelea kuwa kocha huku akiwa mchambuzi ni unafiki na kamwe hatakuwa mkweli kwa kile anachokifanya, hivyo anatakiwa kuchagua kati ya uchambuzi au ukocha.

Kutokana na kauli ya Wenger, Henry hataendelea kujitolea kuwa kocha wa timu hiyo tena baada ya kuchagua kuwa mchambuzi wa soka ambako analipwa kwa mwaka pauni milioni 4.

Pia Wenger alichukizwa sana msimu uliopita wakati Henry akiwa kwenye televisheni ya Sky akiichambua timu ya Arsenal na kudai kwamba hakuwahi kuwaona mashabiki wa timu hiyo wakikosa furaha kama ilivyo sasa.

Kauli hiyo haikuwa ya chuki dhidi ya kocha wake wa zamani wala klabu yake hiyo bali kwa mtu yeyote angeguswa na hali hiyo kama angepata nafasi ya kuhudhuria maandamano yaliyofanywa na mashabiki hao.

Kama alikosea, Henry atatakiwa kuomba msamaha kwa Wenger na klabu yake ya Arsenal pamoja na mashabiki wa klabu hiyo.

Lakini katika hilo, Henry hakuwahi kukosea kwani koo lake linapita katika njia sahihi  inayotumika na Graeme Souness au Jamie Redknapp ambapo anajaribu kuweka sawa kati hasi na chanya.

Chanzo cha habari ndani ya klabu hiyo kinadai kwamba, Henry (38), aliaminika kushindwa kutenganisha kati ya kitendo cha uchambuzi na ukocha kitu ambacho Wenger alikipiga vita kipindi hiki ambacho anakaribia kumaliza mkataba wa kuifundisha timu hiyo.

Ipo dhana inayodaiwa kwamba, Wenger hataki mtu yeyote anayefanya naye kazi amkwaze kwa kumkosoa wakati mambo yanapokwenda kombo katika timu hiyo.

Henry alitakiwa kujiandaa kumkumbusha Alexis Sanchez kwamba hata kama ni bora kiasi gani anatakiwa kuwahi mazoezi kwa wakati, pia kumuuliza Mesut Ozil kama atakwenda ‘gym’ badala ya kujiunga na wanzake kwenye mazoezi ya ziada.

Baada ya kuondoka ni nani atazungumza na vijana wa chini ya umri 17, ni namna gani ya kufanya kuwa zaidi ya Henry? Na nani atawapa hamasa kwa wachezaji makinda na wa kubwa zaidi ya nyota huyo ambaye ameweka rekodi ya kufunga mabao mengi katika timu hiyo ambaye anakwenda kukaa mbali na wachezaji hao.

Lakini Wenger anabaki kuwa na kauli kubwa ndani ya klabu hiyo, televisheni na uwanja wa mazoezi kutokana na kitendo cha Henry kuoneshwa mlango wa kutokea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles