24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

WEMA ARUDI CCM, AKANWA

  • Atoweka mtandaoni, Polepole atamka masharti mazito, asema chama chao si daladala

Na MWANDISHI WETU

MSANII wa filamu nchini, Wema Sepetu, hatimaye amethibitisha tetesi zilizozagaa hivi karibuni za kurudi Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya jana yeye mwenyewe kutangaza rasmi kuondoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Wema, ambaye alitangaza kukihama chama hicho takribani miezi tisa iliyopita, uamuzi wa kurudi CCM aliusema kupitia akaunti yake ya Instagram jana saa 12 jioni.

“Siwezi kuendelea kuishi kwenye nyumba inayonikosesha amani…Peace of mind is everything for me (amani ya akili ni kila kitu kwangu)…natangaza rasmi kuondoka Chadema na kurudi nyumbani….#There is no Place like home… Feels good to be back (hakuna mahali kama nyumbani, najisikia vizuri kurudi)”,  aliandika kwa kifupi Wema.

Kabla ya Wema  kutangaza kurudi rasmi CCM jana, siku nne zilizopita zilizagaa taarifa kupitia mitandao ya kijamii kwamba yeye na mama yake wanajiandaa kurudi ndani ya chama hicho.

Ingawa si Wema wala mama yake ambaye amekwishathibitisha juu ya taarifa hizo, ilielezwa kuwa sababu kubwa iliyowafanya wafikirie kurudi CCM ni kuokoa nyumba yao ya familia, ambayo ilikuwa ibomolewe na kwamba tayari walikuwa wamekwishapelekewa notisi.

Bado haijajulikana msimamo wa mama yake kama naye atarejea CCM au la, baada ya mtoto wake kutangaza hadharani.

Saa chache baada ya Wema kutangaza uamuzi huo, Taarifa ambazo MTANZANIA Jumamosi ilizipata zilieleza kuwa, alikuwa hapatikani kiasi cha kuzua sintofahamu kwa watu wake wa karibu.

Kitendo cha Wema kutopatikana kwa njia ya simu kiliwafanya marafiki zake hao washindwe kuamini kama ni yeye ndiye aliyeandika ujumbe huo wa kuhamia CCM.

MTANZANIA Jumamosi liliwasiliana na Katibu wa Itikadi  na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, ili kufahamu wamepokeaje uamuzi huo wa Wema.

Polepole alisema hadi jana   chama chao kilikuwa hakijapokea taarifa rasmi  za  kupata mwanachama mpya.

“Hatujapokea mtu na hatutapokea mtu sasa mpaka tujiridhishe mwenendo wake,” alisema Polepole.

Alisema kwa kawaida ili kuhesabiwa kuwa mwanachama halali wa chama hicho, unapaswa kujiunga kupitia katika matawi na si vinginevyo.

“Chama chetu kina utaratibu, chama chetu uanachama wa mtu anajiunga kwenye tawi, ili kuwa mwanachama unatakiwa ujiunge kwenye tawi na si vinginevyo,” alisema Polepole.

Alisema mbali na utaratibu wa matawi, pia chama hicho mwaka huu kimefanya marekebisho ya Katiba yake ya mwaka 1977 kwa kuweka  masharti magumu kwa watu wanaohama na kutaka kurudi ndani ya chama hicho.

“Kwa sasa kabla ya kumpokea tutataka kufahamu sababu zilizomfanya aondoke na kilichomrudisha.

“Masharti ni magumu, lakini lengo ni kujenga nidhamu na kuwa na wanachama wanaoamini katika masharti na imani ya chama, CCM si daladala ambayo mtu anapanda na kushuka halafu anapanda tena,” alisema Polepole.

Hatua ya Wema kurejea CCM ni mwendelezo wa wimbi la viongozi na wanasiasa maarufu wa upinzani, hususan Chadema, kujiunga na chama hicho katika siku za hivi karibuni.

Katika kipindi kisichopungua takribani wiki mbili, vigogo watatu wa Chadema walitangaza kujiondoa ndani ya chama hicho na kujiunga na CCM.

Vigogo hao ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila.

Kabla ya akina Masha na Kafulila kuchukua uamuzi huo, ambao mjadala wake bado haujakwisha sawasawa, madiwani watano wa Chadema mkoani Arusha walitangaza kuachia nyadhifa zao na kujiunga CCM kwa sababu ambazo zote zinafanana, za kumuunga mkono Rais John Magufuli katika mapambano dhidi ya ufisadi.

Kuondoka kwa madiwani hao kuliibua mjadala mkubwa, kama ilivyo sasa baada ya wabunge wawili wa Chadema, Godbless Lema wa Arusha Mjini na Joshua Nassari wa Arumeru Mashariki kuwatuhumu kwa kununuliwa na ushahidi wake kuufikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Hadi sasa Takukuru haijawahi kueleza chochote ulipofikia uchunguzi juu ya ushahidi huo waliokabidhiwa na wabunge hao.

Itakumbukwa Wema alitangaza kujiunga Chadema Februari mwaka huu, akiwa ameambatana na mama yake mzazi, nyumbani kwao Sinza, Jijini Dar es Salaam.

Wema, wakati anatangaza kujiunga Chadema alikuwa ndio kwanza amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutumia dawa za kulevya,  jambo ambalo wengi waliliona kama msingi wa yeye kuhama CCM.

Wakati huo alieleza sababu kubwa ya kuchukua uamuzi huo kuwa ni kupata nafasi ya kupigania demokrasia anayodai kuwa inapotea nchini Tanzania.

Sababu nyingine aliyoieleza Wema ni kutelekezwa na CCM, licha ya kujitolea kutoa mchango wake kwa chama hicho wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kiasi cha kuwa hatarini kumwagiwa tindikali visiwani Zanzibar.

“Kuanzia sasa mimi siyo tena mwanachama wa CCM, na muda mfupi ujao nitachukua kadi yangu ya Chadema… Nimeamua kuingia Chadema kwa sababu nataka kupigania demokrasia, laiti ningejua, ningeingia zamani sana, najua nimewahi kusema kuwa nitakufa nikiwa CCM, lakini sikujua kama itakuwa hivi, laiti ningejua mapema basi nisingesema vile na ningejiunga Chadema muda mrefu sana,” alikaririwa Wema  wakati huo.

“Sijachukua pesa yoyote kutoka Chadema, kama nimechukua hata shilingi 10,000 ya Chadema basi kaburi la baba yangu huko Zanzibar litikisike,” alikaririwa Wema wakati huo.

Baada ya Wema kukabidhi kadi ya CCM, mama yake pia alirudisha kadi ya CCM na kusema watatembea Tanzania nzima kuinadi Chadema.

Kauli hiyo ilikuja baada ya mama huyo kueleza jinsi ambavyo CCM haikumtendea haki mwanawe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles