31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

WAZO: HONGERA KARIA, TUPE FARAJA YA MAENDELEO SOKA LA TANZANIA

Na MOHAMED MHARIZO

UCHAGUZI wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), umefanyika juzi mkoani Dodoma na Wallace Karia, kuchaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho hilo kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Kuchaguliwa kwa Karia katika uchaguzi huo kunaonyesha kuwa wajumbe walikuwa na imani naye na ndiyo sababu ya kumchagua kwa kura 95 huku akiwaacha kwa mbali wapinzani wake, Ally Mayay, aliyepata kura 9, Richard Shija kura 9, Imani Madega kura 8, Fredrick Mwakalebela kura 3 na Emmanuel Kimbe kura 1.

Katika kampeni zako kabla ya uchaguzi ulikuwa na sera za ushawishi kama vile uwazi, uadilifu, uwajibikaji na maendeleo, hivyo wajumbe wamekuelewa na wamekupa kura ili uweze kuiongoza TFF katika kipindi cha miaka minne na kutuletea maendeleo.

Imani ya wajumbe kwako, Makamu wa Rais, Michael Wambura na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni kiashirio kuwa inastahili kuiongoza TFF katika kipindi hiki, hivyo wadau wa mchezo huu wanatarajia kuona makubwa kutoka kwenu.

Binafsi nakupongeza Karia pamoja na wajumbe wako wa Kamati ya Utendaji, kwa hakika mna majukumu mazito mbele yenu, msimamo wako ndio utakuwa dira ya maendeleo ya soka la Tanzania.

Kwa muda mrefu tumekuwa wanyonge katika soka, hatufiki mbali katika kusaka maendeleo, badala yake tumekuwa wasindikizaji kwa wengine, sasa hebu tupe faraja tuondokane na unyonge huu, tupambane na hali yetu nasi tutembee kifua mbele tukijivunia timu yetu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kwa kufika mbali zaidi.

Tumekuwa watumwa wa timu za Taifa za wenzetu, tumekuwa tukithamini wachezaji wa nchi nyingine kwa kuvaa jezi zao nyuma ya migongo yetu, kwani sisi hatufikii kucheza Fainali za Afrika (Afcon) na Kombe la Dunia.

Mapenzi ya timu yetu ya Taifa yameporomoka kama vile tunavyoporomoka katika viwango vya ubora vinavyotolewa kila mwezi na Shirikisho la Soka la Dunia (Fifa), kwani kwa mwezi Julai tuliporomoka kutoka nafasi ya 114 hadi 120 huku Uganda wakiongoza katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati wakiwa nafasi ya 73 wakati Kenya wakishika nafasi ya 82.

Hali hii inatupoteza katika mwelekeo wa soka duniani, turudishie heshima ya soka letu kwa kupambana kuhakikisha tunakuwa mfano katika ukanda huu, Karia naamini una uzoefu katika soka la Tanzania kwa muda mrefu, hili bila shaka ndilo limewapa imani wajumbe wakuchague.

Ifanye TFF iwe chombo chenye nidhamu, kwa kuonyesha uwazi katika utendaji, uadilifu, uwajibikaji ili maendeleo yapatikane katika zama hizi ambazo soka linazidi kupiga hatua na kupendwa zaidi duniani, hatutarajii kuona migogoro inaibuka chini ya utawala wako.

TFF ni taasisi kubwa, waaminishe wadhamini ili waone kuwa hapo ni sehemu salama kuwekeza, tusitegemee kuwa soka letu litakuwa kama hakutakuwa na uwekezaji.

Usiwe mpole sana katika majukumu yao, wala usikubali kuburuzwa na watu, simamia katiba ya TFF na usipende kusikiliza majungu kwani hayajengi bali yanabomoa, usikubali watu wafanye kijiwe katika ofisi za shirikisho hilo.

Fanya kazi kwa kusimamia misingi, kanuni na taratibu ili kupeleka mbele soka letu, fanyia kazi mazuri ya mtangulizi wako, Jamal Malinzi kama uwekezaji wa soka la vijana kwa mustakabali wa timu ya Taifa, hasa ufanye maandalizi ya uhakika ya Fainali za Vijana Afrika chini ya miaka 17, ambazo Tanzania itakuwa mwenyeji. Nikutakie kila la kheri Karia katika uongozi wako.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles