24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI: WALIOKULA MAMILIONI VETA WATAKATWA MSHAHARA

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amewajia juu viongozi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) kwa kuwataka kurejesha haraka masurufu ya fedha Sh milioni 600 ambazo hazionekani kwenye kumbukumbu wala zimetumikaje.

Alisema wale wote waliotumia fedha hizo wazirejeshe katika akaunti ya Veta, ili zifanye kazi iliyokusudiwa, vinginevyo zikatwe kwenye mishahara yao.

Agizo hilo alilitoa jana mjini hapa, alipokuwa akizungumza na viongozi wa Veta, wakiwamo wakurugenzi, wakuu wa kanda na vyuo nchini.

Kutokana na hali hiyo, alimwagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Veta, Peter Maduki, kuhakikisha fedha hizo zinarudishwa mara moja na waliohusika kujilimbikizia masurufu hayo awachukulie hatua za kinidhamu.

“Ripoti ya ukaguzi iliyotolewa Agosti, mwaka huu, inaonesha kwamba kuna ubadhirifu wa fedha katika mamlaka hiyo na hivyo wahusika lazima warudishe fedha hizo na wawajibishwe.

“Ripoti hiyo imetanabahisha wazi kuna viashiria vya upotevu wa fedha, inaonyesha makusanyo mengine yalikuwa hayafikishwi benki, vifaa vilivyonunuliwa havionekani wapi viliandikwa na manunuzi mengine hayaoneshi kufanyika,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, Profesa Ndalichako aliagiza wale watakaoshindwa kurejesha fedha hizo wakatwe kwenye mishahara yao, kwani fedha hizo ni za walipa kodi, hivyo zinatakiwa kurudishwa haraka kwenye akauti ya Veta.

Alikerwa na utendaji usio na ubunifu wa mamlaka hiyo, hivyo aliitaka kuanza kutoa mafunzo yenye ubunifu yanayoendana na karne ya sayansi na teknolojia.

Alisema  sasa mitaala iliyopo imepitwa na wakati na inatoa mafunzo ambayo hayaendani na wakati.

“Mamlaka ihakiki wafanyakazi na kukamilisha uhakiki, inakuwaje watumishi wanaendelea kulipwa mishahara ya kodi za wananchi, huku uhakiki haujakamilika?

“Naagiza Mwenyekiti wa Bodi kufanya uchunguzi wa uwezo wa menejimenti ya mamlaka katika ngazi mbalimbali, kwani haiwezekani kiongozi anakuwa kwenye idara au nafasi hiyo kwa miaka miwili au mitatu na hakuna maendeleo au matokeo chanya ya kazi yaliyopatikana,” alisema Profesa Ndalichako.

Naye Maduki alisema taasisi hiyo imejipanga kufanya mapitio ya mwongozo wa ugatuaji madaraka ambao upo tangu mwaka 2007, ili kuendana na wakati.

Mwisho

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles