29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri wa Magufuli anusuru vurugu

Pg 1Jonas Mushi na Veronica Romwald, Dar es Salaam

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye  jana alinusuru kuvunjika kwa mdahalo ulioandaliwa na Jumuiya ya Taasisi za Elimu ya Juu (TAHLISO), baada ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuupinga.

Mdahalo huo ulilenga kujadili hotuba ya Rais Dk. John Magufuli aliyosoma bungeni Novemba 20, mwaka huu wakati akizindua Bunge la 11.

Dosari hiyo ilijitokeza mapema kabla ya Nape kuwasili katika ukumbi wa Nkurumah baadaya Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho (DARUSO), Kataponda Ahadi kusimama na kutoa hoja ya kuwataka wenzake wasusie mdahalo huo kwa sababu haukubeba ajenda na lengo la TAHLISO.

Hata hivyo, alikatishwa mazungumzo yake baada ya kuelezwa muda wa kujadili mada ulikuwa haujaanza, kwa sababu wakati huo  mdhamini wa mdahalo huo ambao ni Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), alikuwa akielezea faida za mfuko huo.

Baada ya malumbano yaliyochukua muda kidogo, wanafunzi hao walikubaliana na hoja ya  kuendelea kumsikiliza mwakailishi wa NSSF aliyekuwa akiwasilisha mada, hadi Nape alipowasili ukumbini hapo.

Katika hotuba yake, Nape aliusifia mdahalo huo na kusema utasaidia wabunge watakapo kwenda bungeni wawe na ajenda za wananchi, badala ya kwenda na ajenda zao ambazo pengine si matatizo wanayopata wananchi.

Alisema hotuba ya rais, imekuja kwa wakati na imeeleza changamoto nyingi, hivyo ni muhimu vijana wakawa sehemu ya mabadiliko yanayotakiwa kwa staha na uwazi.

Aliwataka wananchi waache utaratibu wa kusikiza na kushangilia tu, bali waichambue, waikosoe,washauri na kuwasisitiza kuwa wasiache suala la mabadiliko liwe la Rais Dk. Magufuli tu.

“Lazima tuhakikishe mabadiliko haya yanaingia kwenye mfumo na yasibaki kwa rais peke yake ili siku tukimpata mtu mwingine afuate mfumo huo. Inapaswa tuusukume mfumo ukubali  mabadiliko hayo lakini mfumo ukigoma tutapata matatizo,” alisema Nape.

Baada ya hotuba hiyo, baadhi ya wanafunzi walinyoosha mikono kutaka kutoa hoja ambapo mshereheshaji aliwataka wasubiri mada zitakapowasilizwa wahusika ndiyo wapate muda wa kuzijadili.

Hata hivyo, wanafunzi hao hawakukubaliana na mwongozo huo na walisimama na kusema wana hoja ya kumweleza waziri kabla mada hazijawasilishwa na ndipo mmoja alipopewa nafasi.

Mwanafunzi huyo ambaye hakuweza kufahamika jina lake, alisimama na kuanza kutupa lawama kwa TAHLISO kuwa wameshindwa kusikiliza na kujadili matatizo yanayowakabili wanafunzi wa vyuo vikuu na badala yake wanajihusisha na mijadala ya kisiasa.

“Tunashangaa TAHLISO ambayo ni shirikisho la kuwatetea wanafunzi wa vyuo vikuu, wamekaa kimya kila tunapofikisha matatizo ya wanafunzi, sasa wameona bora wajadili hotuba ya Dk.Magufuli,” alisema mwanafunzi huyo ambaye kabla hata hajamaliza kutoa hoja yake aliamriwa kuketi.

Kitendo hicho kiliamsha hisia kwa wanafunzi wengine, ambao walisimama na kuanza kupaza sauti wakipinga mdahalo huo kwa madai kuwa hauna maslahi ya wanafunzi na kwamba ni wa kisiasa.

Hali hiyo ilimlazimu mshereheshaji kuwaomba askari kuingia ndani ili kuwatoa wanafunzi hao ambao hata hivyo waliamua kutoka wenyewe wakiongozwa na rais wao huku wakiendelea kuituhumu jumuiya hiyo.

Walipofika nje ya ukumbi waliendelea kupiga kelele ambapo iliwalazimu baadhi ya viongozi wa TAHLISO kutoka nje na kuwataka waondoke katika eneo hilo.

Yaliibuka mabishano baina ya viongozi wa pande hizo mbili na baadhi ya wanafunzi ambapo Waziri Nape aliamua kutoka nje na kuacha mdahalo ukiendelea na alipofika nje aliomba kusikiliza hoja zao.

Akielezea malalamiko yao, Rais wa DARUSO Ahadi alisema TAHLISO imeshindwa kusimamia maslahi ya wanafunzi hasa pale wanapoomba kukutana ili kujadili masuala ya wanafunzi wamekuwa hawajitokezi.

“Hawa kwenye mambo yanayohusu wanafunzi wanakaa kimya, mdahalo wameweza kuandaa kujadili hotuba ya Rais Magufuli, zaidi hata huu mdahalo unaofanyika hapa kwetu sisi viongozi wa DARUSO ambao pia ni wajumbe wake hatujapewa taarifa, ndio maana tumeamua kuupinga,” alisema Ahadi.

Kwa upande wake, Waziri wa Mikopo wa DARUSO, Shitindio Venance, alisema: “Kutokana na kitendo cha jumuiya hii kushindwa kutatua matatizo yetu tumeamua kuunda Kamati ya Taifa ya kufuatilia Mikopo ya wanafunzi nchi nzima na hivi tunapozungumza hapa kuna wanafunzi wapatao 80 ambao wanatakiwa wafungashe warudi nyumbani kwa kukosa mikopo na wengine wapo Chuo cha Bagamoyo lakini tunashangaa TAHLISO ipo kimya,”alisema.

Naye Makamu wa Rais wa DARUSO, Irene Ishengoma, alimweleza Nape kuwa pamoja na kusumbuliwa kwa kunyimwa mikopo, bado Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) imekuwa ikiwatoza sh 20,000 za kuiendesha suala ambalo ilitakiwa yenyewe itafute mbinu za kujiendesha.

Akijibu hoja hizo Nape aliwataka viongozi hao kuitisha vikao ili kuwaondoa viongozi wa TAHLISO ambao wameonekana kushindwa kazi kwani wao ndio waliowaweka na hivyo wana mamlaka ya kuwaondoa.

“Unajua tatizo lenu ni dogo…hawa viongozi mmewaweka wenyewe na kwa kawaida mwiba unapoingilia ndipo unapotokea hivyo nyie ndio wakuwatoa, tumbueni majipu kama mnaona yapo,” alisema Nape.

Kuhusu matatizo ya mkopo, Nape aliwaambia tayari yanajulikana na kwamba licha ya kwamba yeye si waziri mwenye dhamana lakini ni kiongozi wa chama kilichopo madarakani hivyo atahakikisha leo watahakikisha, tatizo hilo linakoma.

“Naomba niwahakikishie kuwa ikifika kesho (leo) wanaohusika tutakwenda kuwashughulikia ili wakawajibike kwa sababu inaonekana kuna tatizo maana wanafunzi wakigoma fedha zipo lakini wakikaa kimya hawapewi,” alisea Nape.

insetNape alifanikiwa kumaliza dosari hiyo iliyodumu kwa dakika 20 baada ya kuwaomba wanafunzi hao warudi ukumbini ili kuendelea na mdahalo kwasababu kama ni matatizo yao yamefika sehemu husika ambapo walikubali na kurudi ukumbini.

Ndani ya ukumbi huo mada zilikuwa zinaendelea ambapo akichambua hotuba ya Rais Magufuli, Mtaalamu wa Mambo ya Uchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk. Honest Ngowi alisema kiuchumi suala la elimu bure halipo kwani elimu hiyo inalipiwa kwa ruzuku ya serikali kwa asilimia 100.

Alisema ili kuweza kutekeleza hilo wananchi wanatakiwa kukubali kulipa kodi zilizowekwa kwasababu ndizo zitakazotumika kuendesha sekta hiyo.

Naye Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa (UDSM), Dk. John Jingu alisema hotuba hiyo ilijikita katika dira ya maendeleo ya Taifa ifikapo mwaka 2025 ya kuwa na uchumi wa kati, kwani rais ameweza kuonesha njia na nia ya kutekeleza dira hiyo.

Kwa upande wake Mwanadiplomasia mkongwe, Balozi Christopher Liundi alisema hotuba ya Rais Magufuli imekuwa mfano kwa viongozi wa chini yake, kwani wanaonekana kutenda kwa kasi yake tangu aingie madarakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles