23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Ndalichako aitumbua bodi TCU

Profesa Joyce NdalichakoNA RAMADHAN HASSAN, DODOMA

WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako,  amevunja bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu  Tanzania (TCU)  kutokana na kudahili wanafunzi  486 wasiokuwa na sifa katika Chuo Kikuu cha St. Joseph.

Vilevile,  amewatumbua maofisa waandamizi wa TCU kwa kushindwa kusimamia na kutekeleza vema wajibu wa Tume hiyo na kuwateua makaimu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Profesa Ndalichako, alisema kutokana na hali hiyo amelazimika kumsimamisha kazi Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya.

Alisema Profesa Mgaya amesimamishwa kazi kwa  kushindwa kuisimamia  shughuli za TCU   na  wajibu wake kama mtendaji kuu wa taasisi hiyo.

Profesa Ndalichako aliwataja wengine waliotumbuliwa kuwa ni Mkurugenzi wa Ithibati,  Rose Kiishweko aliyekuwa Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka na Kaimu Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka,  Kimboka Instambuli.

“Kwa mamlaka niliyopewa na Mheshimiwa Rais natangaza kuivunja Bodi ya TCU  sababu kubwa ni kudahili wanafunzi wasiokuwa na sifa wa Chuo Kikuu cha St. Joseph. Haiwekekani mwanafunzi mwenye D nne akawa na sifa za kusoma ‘degree.’

“Rais anahangaika kutafuta fedha na ameniagiza wote niwasimamishe kazi na mimi nawasimamisha kazi. Haiwezekani wale ambao hawana sifa ndiyo wapewe na wale wenye sifa wakose, hiyo ni sawa na wafanyakazi hewa,’’ alisema.

Kwa uamuzi huo, Waziri Profesa Ndalichako, amemteua Profesa Eleuther Mwageni kukaimu nafasi ya Katibu Mtendaji wa TCU.

Profesa Mwageni  alikuwa Naibu Makamu Mkuu (Utawala na Fedha) wa Chuo Kikuu cha Ardhi.

Waziri pia amemteua Dk. Kokubelwa Mollel,  kukaimu nafasi ya ukurugenzi wa udahili na nyaraka.

Dk. Mollel kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi wa udhibiti ubora wa Chuo Kikuu cha Dar salaam.

Profesa Ndalichako alisema kuwa wanafunzi 424 waliokuwa wakisoma katika Chuo Kikuu  cha St. Joseph wametafutiwa vyuo vingine.

Alisema  baada ya wanafunzi hao kujiunga na vyuo vingine walionekana wapo nyuma katika masomo kwa tofauti ya mwaka mmoja.

Profesa Ndalichako alisema wanafunzi waliopelekwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)  ambao katika Chuo Kikuu cha St Joseph walikuwa mwaka wa tatu walirudishwa nyuma kwa mwaka mmoja.

Pia alisema wale waliotoka Tawi la Songea na kuhamishiwa katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA)   Morogoro, walionekana na udhaifu katika masomo yao hali iliyofanya uongozi wa chuo hicho kuwapa masomo ya ziada.

“Februari mwaka huu Serikali ilifanya ukaguzi katika Chuo Kikuu cha St. Joseph na kubaini elimu waliyokuwa wakiitoa ilikuwa na upungufu mkubwa na kukifungia chuo kisha wanafunzi tukawahamishia na tuliwapeleka UDOM na wengine SUA  lakini walikuwa na uwezo mdogo.

‘’Jambo la kushangaza kuliko yote ni mwanafunzi mwenye ‘division 4’ kupata mkopo… jambo la kushangaza mtu kasoma masomo ya biashara lakini anakuwa na sifa  kusoma masomo ya sayansi, ni jambo la ajabu kabisa,’’ alisema.

Waziri  alitoa tahadhari kwa vyuo ambavyo havina sifa kuwa serikali itavifunga huku wanafunzi waliochukua mikopo wakitakiwa kuirejesha kwa wakati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles