30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI MWAKYEMBE WASANII WANAKUTEGEMEA

NA CHRISTOPHER MSEKENA

MOJA ya mikakati aliyokuwa ameipanga waziri wa zamani wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, ni kuhakikisha tasnia ya filamu inapata sera kabambe itakayopunguza matatizo na kuongeza tija kwa wasanii wa filamu.

Kabla ya kutekelezwa kwa mkakati huo, tumeshuhudia mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri yakifanywa na Rais Dk John Pombe Magufuli. Mabadiliko yaliyopelekea Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kupata waziri mpya, Dk Harrison Mwakyembe.

Waziri wetu mpya tayari amekula kiapo cha kuwatumikia wasanii kwa kusikiliza shida zao na kuwapa mwelekeo wa tasnia hiyo inakotakiwa kwenda.

Nape Nnauye alishaingia vitani kupambana na matatizo yaliyoirudisha nyuma tasnia ya filamu nchini, chini yake tulishuhudia jitihada zake za kukutana na wasanii na kuwasikiliza.

Kuingia mtaani kutazama ukubwa wa tatizo ili ajue namna gani anavyoweza kutumia mamlaka yake kuzuia wizi huo uliowafilisi wasanii wetu kwa miaka mingi iliyopita.

Hiyo yote ilikuwa ni jitihada zake za kuhakikisha anaiinua tasnia ya filamu, ambayo ipo nyuma ukilinganisha na muziki wa Bongo Fleva, ambao unazidi kukata mawimbi kwenye anga la kimataifa, hakika ameacha historia nzuri isiyofutika kwenye sanaa ya Kitanzania.

Kama unavyojua, ukikataa kukubaliana na mabadiliko basi dunia itakuacha, hivyo hatuna budi kwenda sambamba na mabadiliko hayo ya waziri, kwa kuwa lengo letu ni lile lile la kuhakikisha tasnia ya filamu inakuwa juu, tena yenye hadhi.

Karibu Waziri wangu Dk Harrison Mwakyembe kwenye wizara hiyo inayosimamia watu wajanja kama alivyokuwa anaiita, Nape Nnauye. Matumaini makubwa ya wasanii, hasa wa filamu, ni kuhakikisha unaendelea kusimamia yale ambayo mtangulizi wako alikuwa anayafanya.

Najua baada ya taarifa za mabadiliko  haya kwenye wizara wale wezi waliokuwa wanamuogopa Nape kwa uthubutu wake watakuwa wamefurahi na punde wataingia tena kazini kwenda kuwaumiza wasanii, sababu wanajua aliyekuwa anawapa tabu hayupo tena.

Natamani kuona Mwakyembe ukivaa viatu vya Nape ili uweze kwenda sawa na watu unaowaongoza, naamini watakupa ushirikiano na ni lazima uwe mkali kama alivyokuwa Nape, ili wezi wa kazi za sanaa wasipate nafasi ya kuiba.

Jambo lingine kubwa ni sera, wasanii wamechoka ahadi na matumaini yao kwao uharakishe, ili wapate sera nzuri itakayoipa hadhi tasnia ya filamu ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles