24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mkuu: Wanaotoa taarifa za kupotosha kuhusu corona wachukuliwe hatua

Mwandishi wetu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufuatilia watu wote wanaofanya upotoshaji kwa kupitia mitandao ya kijamii kuhusu ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Machi 21, alipokuwa akizungumza na wakuu wa mikoa yote nchini, makatibu Tawala wa mikoa na waganga wakuu wa mikoa kwa njia ya video kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.

Amesema kuanzia sasa taarifa hizo zitatolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na ikilazimika zitatolewa na yeye mwenyewe na ikilazimika sana zitatolewa na viongozi wakuu wa nchi ili kuepusha mikanganyiko.

“Watu wote wanaopotosha umma na kuleta taharuki kuhusu ugonjwa wa corona badala ya kuelimisha namna ya kujikinga, wafuatiliwe na kuchukuliwa hatua.

“Wakuu wa mikoa kila mmoja ahakikishe eneo lake linakuwa salama na endapo kutakuwa na mgonjwa tumieni zahanati ambazo bado hazijaanza kutumika kwa ajili ya kutolea huduma kwa wagonjwa wa corona,” amesema.

Aidha amewataka wakuu hao wa mikoa kuimarisha utoaji wa elimu kwa umma na ikiwezekana watumie magari ya matangazo ili wananchi waelewe athari za ugonjwa huo na namna ya kujikinga pamoja na kuwaondolea hofu ili waweze kuendelea na shughuli zao za kimaendeleo.

 “Nendeni kwenye maeneo ya mikusanyiko, vituo vya mabasi kutoa elimu kwa umma na kuwaondoa hofu. Upande wa maofisini, viwandani na kwenye mgodi kuwe na utaratibu wa kutoa elimu kwa wafanyakazi kila siku asubuhi watumie hata robo saa kabla ya kuanza kazi waelekezwe namna ya kujikinga,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles