Waziri mkuu atoa siku mbili kwa ofisa elimu

0
454

Na MWANDISHI WETU-KAGERA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ametoa siku mbili kwa Kaimu Ofisa Elimu (Msingi) wa Wilaya ya Muleba  mkoani Kagera, Bukuru Malembo awe amepeleka walimu wawili katika shule ya msingi ya  Kitongoji cha Rwenzige kwa kuwa haina mwalimu hata mmoja.

Shule hiyo yenye madarasa wawili na ofisi moja ya mwalimu ina jwanafunzi 216 wa darasa la awali hadi la nne.

Shule ilijengwa na wananchi huku wanafunzi wake wakifundishwa na mwananchi mmoja aliyejitolea  kuwapunguzia watoto kutembea umbali wa kilomita 16 kwenda kusoma katika shule ya Kijiji cha Kiteme.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana baada ya wanafunzi wa shule hiyo kuwasilisha malalamiko yao kwa   bango wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kiwanja cha Kituo cha Afya Kimeya, baada ya kukagua majengo ya kituo hicho.

“Haiwezekani watoto wadogo wenye umri wa kuanzia miaka mitano wakatembea umbali wa kilomita 16 kwenda shule wakati katika kitongoji chao kuna shule yenye madarasa mawili na chumba kimoja cha ofisi ya mwalimu na ofisa elimu hadi sasa hajapeleka walimu na kumuachia mwalimu Benson (kijana ambaye si mwalimu ila anajitolea kufundisha) akifundisha wanafunzi hao peke yake,” alisema.

Waziri Mkuu alimuagiza ofisa elimu huyo ahakikishe ifikapo leo saa 4.00 asubuhi awe amekwisha kuwapeleka walimu hao katika shule hiyo ya msingi waweze kuwafundisha wanafunzi hao.

Vilevile amemuagiza  Mkuu wa Wilaya hiyo,  Richard Ruyango awasilishe taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo ofisini kwake.

“Walimu wengi mmewaacha katika shule za barabarani huku za vijijini zikiwa hazina walimu,” alisema.

Naye  Benson Bukerebe (29), maarufu mwalimu Benson, alisema yeye  si mwalimu bali ni mhitimu wa kidato cha nne.

Alisema aliamua kuanzisha darasa kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi hao kwa sababu alikuwa akiwahurumia ikizingatiwa  baadhi yao hawakuwa na uwezo wa kutembea umbali wa kilomita 16 hadi iliko shule ya Msingi ya Kiteme.

Kijana huyo alisema kwa muda wote huo ameweza kumudu kuwafundisha wanafunzi hao kwa kutumia vitabu vya kuazima kutoka shule mbalimbali za msingi.

Alisema  lengo ni kuhakikisha watoto wenye umri wa kuanza shule katika kitongoji chao wanapata fursa ya elimu ambayo ni haki yao ya msingi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here