30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Masauni ajihami kutumbuliwa na JPM

NA MWANDISHI WETU – ZANZIBAR

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, amesema hayupo tayari kuona kuwa anatumbuliwa na Rais John Magufuli kutokana na uzembe wa kusimamia suala la dawa za kuevya Zanzibar.

Masauni aliyasema hayo jana, mbele ya waandishi wa habari visiwani humo, huku akimtaja Katibu wa Tume ya Dawa za Kulevya Zanzibar, Heriyangu Mgeni kuwa ni mmoja wa wanaokwamisha na kwamba atatoa mapendekezo mamlaka husika kumwondoa.

Alisema Mgeni, mwenye cheo alichokitaja cha Senior Assistant Commissioner of Polisi, hakuwekwa hapo kwa bahati mbaya, lakini hatimizi wajibu wake.

Alisema hivi karibuni kulikuwa na kikao kilichokutanisha tume mbili za dawa za kulevya, moja ikiwa ni ile inayofanya kazi za Bara na nyingine Zanzibar.

Alisema katika kikao hicho, ambacho Mgeni aliwakilisha kwa upande wa Zanzibar, Masauni alitaka kujua kinachoendelea dhidi ya mapambano ya Dawa za Kulevya Zanzibar, lakini Katibu huyo pamoja na mambo mengine alielekeza malalamiko yake kwa Jeshi la Polisi kwa asilimia 99.

“Kwamba matatizo na changamoto za upambanaji wa dawa za kulevya Zanzibar na Jeshi la Polisi lina mchango mkubwa. Hayo ni maelezo yaliyotolewa katika kikao kikubwa ambacho Waziri Mkuu ni Mwenyekiti wake.

“Mimi nikiwa na dhamana, mara kadhaa nimekuwa nikimwita Katibu nikishauriana naye kwa kuwa suala la dawa za kulevya linaniumiza roho, ni mpaka leo Kisiwa cha Zanzibar chenye watu milioni 1.3 kinashindwa matatizo ya dawa za kulevya kwa kiwango kinachostahili,” alisema Masauni.

Alisema katika kikao hicho alipongeza kwamba wameanza kufikia pazuri, kwasababu kulikuwa na kusukumiana mara DPP, Mahakama, Polisi.

Alisema kutokana na tuhuma kuelekezwa jeshi hilo, ambalo liko chini ya Wizara anayoiongoza, aliomba kupatiwa majina ya wanaokwamisha juhudi hizo.

 “Maazimio ya kikao ilikuwa ni kushughulika na watu hao ambao Katibu alisema anawafahamu kuwa wanamkwamisha. Nilimweleza mbele ya kikao kuwa nataka unipatie data nikashughulike, naacha Bunge nakwenda Zanzibar kwa shughuli hii, siwezi kusubiri Rais John Magufuli anitumbue mimi kwasababu ya uzembe wa watu wachache. Nipatie majina tutawatumbua wao kwanza, hatuwezi kubakia na askari ambao hawatimizi majukumu yao, hawana maadili. Ni kitu cha mara moja, nipatie majina Jumatatu tukafanye shughuli, liishe, na nakuahidi hautasikia mahali kuwa umenipa hizo taarifa,” alisema Masauni.

“Lakini ukifanya mambo ambayo ni kinyume na makubaliano yetu, nitaamini kuwa wewe ndio kikwazo nambari moja. Kama itafika Jumatatu nakuja pale hizo taarifa ulizitoa mbele ya kikao kikubwa, haujanipatia, nitapata mashaka na wewe. Nimekuja hapa toka Jumamosi, na shughuli yangu ilikuwa niifanye Jumatatu asubuhi ili niwahi kuondoka kurudi bungeni, nimekuwa nikibembeleza taarifa kwa Katibu huyu hadi tunapozungumza sasa hivi sijazipata,” alisema Masauni.

Alisema katika hali kama hiyo, haoni kama Zanzibar kuna nia ya dhati ya kupambana na dawa za kulevya kwa aina ya Katibu yule.

“Nina mashaka makubwa, kwa hiyo kwasababu si mamlaka yangu kusema atoke kuwa Katibu Mtendaji, nitawasilisha mapendekezo kwa mamlaka husika iangalie namna ya kutafuta mwingine,” alisema Masauni.

Alisema hata hivyo, aligundua kuna mapungufu ya baadhi ya askari kwa kuwa wapo wanaoharibu kesi za dawa za kulevya makusudi kwa kuchukua rushwa kutoka kwa wauzaji wa dawa hizo wanaojulikana na kuwaachia mitaani.

Alimwelekeza Katibu wa Wizara hiyo kuunda tume maalumu itakayokuja kufanya kazi Zanzibar kuwabaini askari wanaozorotosha jambo hilo na hatua za haraka zichukuliwe.

Katika mkutano huo wa waandishi, Masauni alikuwa na karatasi ya majina ya washukiwa wa dawa za kulevya, ikiwa na kurasa tano wa visiwani Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles