31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI KAMWELWE ATOA MAAGIZO SEKTA YA MAJI

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe, ameziagiza mamlaka za maji kote nchini kuhakikisha ifikapo mwishoni mwa Juni mwaka 2018, upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya miji mikuu ya mikoa unakuwa ni asilimia 86.

Pia, amewaagiza watendaji wakuu wote wa mamlaka za maji nchini, kuhakikisha wanatekeleza mikakati ya kupunguza upotevu wa maji katika maeneo yao ili kufikia viwango vilivyoainishwa kwenye mkataba wa makubaliano kati ya wizara na mamlaka husika.

Kamwelwe aliyasema hayo juzi mjini hapa, wakati alipokuwa akifungua kikao cha watendaji wakuu wa mamalaka za maji safi na usafi wa mazingira Tanzania Bara.

“Naagiza mamlaka za maji kote nchini kuhakikisha ifikapo mwishoni mwa Juni mwaka 2018, upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya miji mikuu ya mikoa unakuwa kwa asilimia 86,” alisema.

Pia, waziri huyo aliwataka wakurugenzi wa mamlaka za maji na usafi wa mazingira, kuhakikisha katika miji mikuu ya wilaya, miji midogo na maeneo yanayohudumiwa na miradi ya kitaifa, upatikanaji wa maji safi na salama unafikia wastani usiopungua asilimia 70 ifikapo mwishoni mwa Juni mwaka 2018.

Ili kufikia malengo hayo, alisema wahusika lazima wawe na tabia ya kujipima kila mwaka ili kujua wanapiga hatua kiasi gani kufikia lengo kuu.

Aidha, alisema katika kufikia malengo hayo, wanatakiwa kuhakikisha changamoto za upotevu wa maji wakati yakisafirishwa kumfikia mlaji zinadhibitiwa.

“Ripoti za Ewura za tathmini ya utendaji kazi wa mamlaka za maji nchini zinaonesha zaidi ya wastani wa asilimia 30 ya maji yaliyozalishwa yanapotea njiani kabla ya kuwafikia wanachi.

“Kwa hiyo, lazima watendaji wakuu wote wa mamlaka za maji nchini, wahakikishe wanatekeleza mikakati ya kupunguza upotevu wa maji katika maeneo yao ili kufikia viwango vilivyoainishwa kwenye mkataba wa makubaliano kati ya wizara na mamlaka,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso, aliwataka wakurugenzi wa mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira nchini, kutoa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kufikia malengo.

“Peke yetu hatuwezi kufanya kitu ndiyo maana nawaomba mtupe ushirikiano kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kuwahudumia Watanzania wenye mahitaji makubwa ya maji mijini na vijijini,” alisema Aweso.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles