29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI KALEMANI AWABANA WAKANDARASI

Na Mwandishi Wetu-Njombe

NAIBU Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, amemtaka mkandarasi aliyepewa kazi ya kujenga vituo vya kupoza umeme na aliyepewa kazi ya kuusambaza katika mradi mkubwa wa usafirishaji Makambako-Songea kukamilisha kazi hizo mwezi ujao.

Dk. Kalemani aliyasema hayo katika Mji wa Makambako mkoani Njombe, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo ambao unahusisha ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme wa msongo wa KV 220, vituo vipya vya kupoza na  upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Makambako.

Akizungumza kuhusu mkandarasi wa Kampuni ya JV Shandong Taikai Power, Dk. Kalemani alisema kampuni hiyo ilipewa kazi kujenga vituo viwili vipya vya kupozea umeme vya kV 220/33 katika Mji wa Madaba na Songea na upanuzi wa kituo cha kupozea umeme cha Makambako cha kV 220/132/33.

“Kampuni hii ilianza shughuli zake miaka mitatu  iliyopita, ilitakiwa kukamilisha kazi Machi mwakani, lakini mpaka sasa hakuna maendeleo yoyote, naagiza msitoke eneo la kazi mpaka kutakapokuwa na hatua za kuridhisha za ujenzi,” alisema Dk.Kalemani.

Dk. Kalemani alimwagiza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhakikisha kampuni hiyo haipati malipo yoyote mpaka itakapoanza kufanya kazi husika na tathmini kufanyika.

Kuhusu kazi ya usambazaji umeme katika vijiji 120 vya mikoa ya Njombe na Ruvuma, Dk. Kalemani alimtaka mkandarasi wa Kampuni ya Isolux Ingenieria kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo ifikapo mwezi ujao kwa sababu alitakiwa kukamilisha kazi Desemba mwaka jana.

Alisema mkandarasi atasambaza umeme katika eneo lenye  urefu wa kilomita 900 na kuunganisha wateja 22,700 mikoa ya Njombe na Iringa.

Kuhusu kazi ya ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme wa msongo wa kV 220 kutoka Makambako hadi  Songea wenye urefu wa kilomita 250, Naibu Waziri alisema kazi inaendelea vizuri.

Kuhusu gharama za mradi, alisema Serikali ya Sweden ilitoa krona milioni 620 na Serikali ya Tanzania imechangia Dola za Marekani milioni 20 ambazo zinakuwa Sh bilioni 7.

Katika hatua nyingine, alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka, kuwasimamia kwa karibu wakandarasi hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles